Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Sikonge
MAOFISA wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Dodoma wameendelea na ukaguzi wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na kufanya usajili majengo hayo katika wilaya ya Sikonge mkoani Tabora kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa kufuata matakwa ya sheria pamoja na kuzingatia kanuni bora za afya ili kulinda afya za walaji.
Miongoni mwa majengo yaliyofanyiwa ukaguzi na usajili ni pamoja na mighahawa, baa, mashine za kusaga, majengo ya kuuza vyakula na maduka ya vipodozi ambapo zoezi hilo lilianza Machi 29, mwaka huu hadi Aprili 9, mwaka huu katika wilaya za Sikonge.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi wilayani Sikonge, Afisa Uthibiti Ubora wa TBS, mkoani Dodoma, Zena Mushi , amesema katika ukaguzi na usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi katika Wilaya ya Sikonge wamefanikiwa kutoa vibali zaidi ya 100 kwa wafanyabiashara.
Amesema pamoja na changamoto za mtandao zilizopo maeneo ya vijijini, lakini wamefanikiwa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa na kutoa vibali hivyo zaidi 100.
Amesema mwitikio wa wafanyabiashara kusajili majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi ni mkubwa hasa kutokana na elimu iliyotolewa kwa wananchi na wafanyabiashara kabla ya kuanza usajili tangu jukumu hilo likabidhiwe TBS kutoka kwa iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Amesema usajili wa majengo ya vyakula na vipodozi una faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kuwezesha wafanyabiashara kutambulika kuwa wana vibali vya kusajiliwa majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi.
“Lakini wengine kibali hicho kinawasaidia benki wanapokwenda kuomba mikopo , kwa sababu wakati mwingine wakitaka mkopo wanaambiwa leta kibali kinachokutambua kufanya hiyo biashara, kwa hiyo wakiwa nacho wanaweza kupata mkopo bila kikwazo,” amesema Mushi na kuongeza;
“Kuna wafanyabiashara ambao wana tenda za vyakula kwa ajili kulisha taasisi mbalimbali kama vile shule, kwa hiyo wakati wa kuomba hiyo tenda, inabidi waambatanishe na kibali chetu, kwa hiyo inakuwa rahisi kwao kupata zabuni hiyo.”
Anapoulizwa kama wananchi wa Sikonge walikuwa wakijua kama huduma ya usajili majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi inapatikana TBS badala ya iliyokuwa TFDA, Mushi amesema baadhi walikuwa wanajua hilo kwa sababu walikuwa wakiambiwa na maofisa biashara katika maeneo yao.
Kuhusu mkakati wa shirika hilo kufikia wafanyabiashara wote Kanda ya Kati, Mushi amesema mkakati wao ni kufikia wilaya zote za kanda hiyo, kwa sababu wana ratiba ambayo tayari imeandaliwa kwa ajili ya mwaka mzima.
Mushi anatoa mwito kwa wafanyabiashara pale wanapoanza kufuatilia leseni kwa ajili ya kuanza kufanyabiashara , wasifungue biashara zao kabla ya kujisajili TBS na kuwa na kibali cha usajili wa majengo ya bidhaa za vyakula na vipodozi hatua itakayowaepusha na usumbufu.
Kwa upande wake Afisa Uthibiti Ubora wa TBS, Sileja Lushibika, amewataka wafanyabiashara kuchangamkia fursa hiyo, kwani usajili wa majengo ya bidhaa za vyakula na vipodozi una faida .
Ametaja moja ya faida hiyo kuwa ni takwa la kisheria, kwani mfanyabiashara anapokidhi takwa la kisheria hawezi kuwa kwenye mgongano na Serikali na badala yake anafanyabiashara zake kwa uhuru.
“Kwa hiyo wanapofuata taratibu za kisheria wanaepuka kutumia gharama kubwa za uzalishaji ikiwa ni pamoja na kutozwa faini, hivyo wanakuwa huru kwa mamlaka , kwani badala ya kuona maofisa wa mamlaka husika na kuwakimbia wanakuwa wanatamani kuwakimbilia ili wawape elimu,” amesema Lushibika.
Ametaja faida ya pili kuwa ni usalama wa afya. “Sisi tunasema ubora wa bidhaa yoyote ile unategemea mambo makubwa matatu, takwa la kwanza ni la matumizi bora ya kanuni za afya, ambapo wanaangalia kama jengo la biashara linakidhi kanuni hizo,” amesema na kutaja kanuni nyingine kuwa ni ya usindikaji.
Lushibika amesema baada ya ukaguzi na usajili wa majengo ya bidhaa za chakula na vipondozi kumalizika Sikonge na sasa wanaendelea na kazi hiyo wilayani Uyui.
Sheria ya Fedha Namba 8 ya mwaka 2019 ilihamishia TBS majukumu ya usajili wa bidhaa za chakula , vipodozi na migahawa kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba