TBS: Wajasiriamali njooni kusajili
bidhaa, vipodozi, maeneo ya uzalishaji
Na Penina Malundo
WAJASIRIAMALI kote nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kusajili bidhaa zao, vipodozi na maeneo yao wanayozalishia bidhaa za vyakula kabla ya muda wa miezi mitatu waliopewa kumalizike ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza baadaye.
Rai hiyo imetolewa leo na Ofisa Uhusiano Mkuu wa TBS, Rhoida Andusamile, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa.
Amesema shirika hilo limekuwa likishiriki maonesho ya Sabasaba kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ambao wanatembelea maonesho hayo ili waweze kujua utaratibu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozizalisha na kwa walaji waweze kutambua bidhaa bora ni zipi na zisizo na kiwango ni zipi.
Kwa mujibu wa Andusamile katika maonesho ya mwaka huu wamekuja na nguvu ya kuhamasisha wajasiriamali kuhakikisha wanasajili bidhaa zao, vipodozi pamoja na maeneo yao wanayozalishia bidhaa za vyakula.
Amefafanua kuwa mwaka jana Sheria ya Fedha No:8 ya Mwaka 2019 ililipa shirika hilo mamlaka ya kusajili bidhaa za chakula na vipodozi, jukumu ambalo awali lilikuwa linasimamiwa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
“Kwa hiyo tangu Julai 1, mwaka jana tumekuwa tukifanya kazi hii ya kusajili maeneo ya uzalishaji, maeneo ya kuhifadhia vyakula na vipodozi na vile vile kuthibitisha ubora wa bidhaa kazi ambayo tulikuwa tukiifanya tangu awali,” amesema Andusamile.
Amesema wanatumia fursa ya kushiriki kwao maonesho ya Sabasaba kuwahamasisha zaidi wajasirimali kujitokeza kwa wingi kujisajili, kwani bado wanasuasua.
“Na tumeishatoa tangazo hivi karibuni kuwataka wasajili hizo bidhaa za vyakula na vipodozi, lakini bado wengi wanajivuta.
Nitoe wito kwa wajasiriamali waje wasajili na sasa hivi wanaweza kujisajili Online (kwa njia ya mtandao) kama wamekwama basi waje ofisi za TBS tutawasaidia, lakini kama wanaweza kutuma maombi kwa njia ya mtandao ni vema wakafanya hivyo mapema iwezekanavyo ili kuepuka usumbufu unaweza kujitokeza baadaye,” amesisitiza.
Ameongeza kwamba kwa sasa wameishatoa muda wa miezi mitatu ili waweze kufanya hivyo na iwapo muda huo utamalizika, basi wao kama shirika la viwango wataanza kuwatembelea katika maeneo yao ya biashara.
“Tukiona hawajatekeleza maagizo haya basi hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao. Kwa hiyo tunawasihi sana huo muda wa miezi mitatu waliopewa unaisha mwezi huu wa Julai mwishoni, kwa hiyo kuanzia Agosti tutaanza kuwakagua, hivyo ni vema wakatelekeza hilo mapema iwezekanavyo,” amefafanua Andusamile.
Alipoulizwa kuhusu mwitikio wa wafanyabiashara wakubwa katika hilo, Andusamile amesema hao hawana shida nao, kwani mwitikio wao ni mkubwa.
More Stories
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme