December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS Kanda ya Ziwa kuendelea kuelimisha jamii

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS),limesema litaendelea kuelimisha jamii umuhimu wa shirika hilo ili waweze kuthibitisha ubora wa bidhaa zao wanazozalisha.

Hayo yameelezwa na Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa,Joseph Mwaipaja wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Nanenane na sherehe za wakulima kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi.

Ambapo ameeleza kuwa,kazi kubwa ya Tbs ni kutengeneza viwango na kuthibitisha bidhaa zote za wajasiriamali pamoja na wazalishaji wakubwa hivyo wataendelea kuwaelimisha wananchi ili wafahamu umuhimu wa kuthibitisha ubora wa bidhaa.

Mwaipaja ameeleza kuwa mkulima anaweza kuwa na njia nzuri ya kilimo,lakini asipokuwa na mnyororo sahihi wa kuthibitisha ubora wa bidhaa inakuwa ngumu kufikia malengo.

“Wajasiriamali wengi wamekuwa wakiogopa sana Tbs wakati ni taasisi ya umma ambayo tunatoa huduma kwa utaratibu wa Serikali,wanachotakiwa kujua ni kuwa tuna utaratibu wa kutoa punguzo kwa wajasiriamali wote wanaotengeneza bidhaa,”ameeleza Mwaipaja.

Pia ameeleza kuwa, shirika hilo linafanya udhibiti wa bidhaa zote za sokoni zinazoingia na kuzalishwa ndani ya nchi ili Watanzania wapate bidhaa zinazokidhi ubora.

Aidha ameeleza kuwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Mwanza wakipata nembo ya Tbs itawasaidia sana kuuza bidhaa zao bila kukaguliwa katika nchi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tbs tunapotoa leseni ya ubora katika inatengeneza thamani kwa kuwa na nembo ya ubora kwenye inamuhakikishia mteja kuwa bidhaa ni salama,”ameeleza.

Kwa upande wake mmoja wa wananchi walipotembelea maonesho hayo,Roseline Athuman ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya bidhaa bandia(feki) zinazouzwa na wananchi wanazutumia bila kujua.

Hivyo ameliomba shirika hilo kuendelea kutoa elimu kuhusiana kwa jamii ili iweze kuwa na uelewa wa kutambua ipi ni bidhaa bora na ipi ni feki.

Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa,Joseph Mwaipaja wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Nanenane na sherehe za wakulima kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi.(Picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya wananchi walipotembelea banda la TBS katika maonesho ya nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika katika viwanja vya Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wakimsikiliza Ofisa wa TBS.(Picha na Judith Ferdinand)