Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online
Kampuni ya Tanzania Breweries Plc (TBL), ambayo ni kampuni tanzu ya AB InBev na kinara wa utengenezaji na usambazaji wa bia nchini, imezindua rasmi Ripoti yake ya Uendelevu ya mwaka 2024 ambapo uzinduzi huo ulifanyika chini ya kauli mbiu “Kua, Tengeneza na Dumisha” na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wa biashara, mazingira na jamii.
Ripoti hiyo imeweka bayana hatua za makusudi zilizochukuliwa na TBL katika kulinda mazingira na kuimarisha uwajibikaji wa kijamii. Hatua hizo ni pamoja na kupunguza uzalishaji unaoharibu mazingira, kutumia nishati mbadala, kuhifadhi maji, kuwaendeleza wakulima wa ndani na kuboresha ustawi wa wafanyakazi wake. Pia imeunganishwa na Ripoti ya Mwaka ya Kimataifa ya Anheuser-Busch InBev ya 2024, ikionesha dhamira ya kampuni hiyo kushiriki kikamilifu katika maendeleo endelevu.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Huyghebaert, aliipongeza TBL kwa kuendeleza misingi ya uongozi bora na uwajibikaji. Alisema kampuni hiyo imejipatia heshima kubwa barani Afrika kutokana na ubora na ubunifu wake, huku ikichangia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Alibainisha kuwa TBL ni mfano wa kuigwa si Tanzania pekee bali pia katika mataifa mengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBL, Michelle Kilpin, alisisitiza kuwa kampuni hiyo ina wajibu wa kulinda rasilimali kwa ajili ya vizazi vijavyo. Alieleza kuwa Bodi ya Wakurugenzi imesimamia ukaguzi wa matumizi ya maji, kupunguza moshi unaochafua hewa kwenye mnyororo wa usambazaji na kutumia vifungashio vinavyoweza kurejelewa, sambamba na malengo ya kidunia ya AB InBev ya kupunguza hewa ya ukaa.
Kilpin aliongeza kuwa, zaidi ya kutengeneza na kuuza bia, kampuni hiyo inatambua uhusiano wa karibu uliopo kati ya biashara yake na ustawi wa jamii. Amesema ripoti hiyo ni ushahidi wa hatua za TBL kusimamia kikamilifu wajibu huo, huku ikijitofautisha kwa kuoanisha urithi wake wa muda mrefu na mabadiliko ya kisasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, TBL imeendelea kuwa kinara katika sekta ya bia Tanzania na kuonesha kuwa ufanisi wa kibiashara unaweza kwenda sambamba na maendeleo endelevu. Kampuni hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kuwekeza katika miradi inayolinda mazingira, kuboresha maisha ya Watanzania na kuunga mkono jitihada za kimataifa za kukabiliana na changamoto za tabianchi.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro