Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KATIKA kusheherekea siku ya bia duniani, Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), inayoongoza kwa utengenezaji wa vinywaji hapa nchini, mwishoni mwa wiki imezindua Kampeni ya ‘Smart Drinking’ yenye lengo la kutoa elimu ya kunywa kistaarabu.
Kampeni hiyo inalenga wauzaji na watumiaji wa bia ili kuwahimiza kunywa kwa kiasi na kwa usalama, ambayo imefanyika katika kumbi mbalimbali za starehe katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, na Arusha.
Lengo kuu la Kampeni hiyo ni kuhakikisha watumiaji wa bia za Kampuni hiyo na wauzaji wanazingatia usalama wa afya zao kwa kunywa pombe kwa kiasi. Kwa kuwa wauzaji ni mabalozi wa kwanza wa bia hizo, wana jukumu kubwa la kuhakikisha wateja wao wanakunywa kwa njia salama na kistaarabu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin amesema dhamira ya TBL ni kuwahamasisha wateja wake kunywa kistaarabu.
“Kupitia kampeni hii ya ‘Smart Drinking’, tunawahimiza wateja wetu kutakaoendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia kilevi. Tunashauri pia watumiaji wapate chakula kabla ya kunywa bia na unywaji wa maji kila wanapokunywa bia,” amesema Kilpin na kuongeza.
“Lengo letu ni kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na unywaji wa pombe kupindukia na kuzuia maradhi yanayosababishwa na matumizi makubwa ya pombe. Wauzaji wa bidhaa zetu wanapaswa kuwa waangalifu na kuacha kumhudumia mteja anayekunywa kupitiliza, na kumshauri arudi nyumbani,” amesema.
Naye Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa TBL, Catherine Mabula, amefafanua kuwa kampeni hiyo imepata ushirikiano na mashirika mbalimbali ikiwemo Tanzania Red Cross Society (TRCS), maarufu kama Shirika la Msalaba Mwekundu, vilevile Polisi Tanzania pamoja na wauzaji wa bidhaa za TBL ili kuhakikisha jamii inakuwa salama.
“Kupitia Kampeni hii tunatarajia kwamba ajali za barabarani zinazotokana na unywaji wa pombe kupitiliza zitapungua kwa asilimia 10 kufikia 2025. Vilevile, tunaamini kuwa elimu hii itakua chachu ya kuboresha usalama wa wateja wetu,” amesema Mabula.
More Stories
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA
Coca-cola ‘Kitaa Food Fest’ yahitimishwa kwa mafanikio
Mzee wa Bwax afunika ‘Kitaa food Fest’ Mbagala