March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBL yajizatiti kuinua Sekta ya Kilimo Nchini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Bia ya Tanzania (TBL) na mwanachama wa familia ya AB InBev, imetangaza kuimarisha ushirikiano wake na wakulima nchini kwa lengo la kukuza sekta ya kilimo kupitia mafunzo, ubia wa kimkakati na kuhakikisha masoko ya uhakika ya mazao yao, hatua hiyo imedhihirika kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane 2025 yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma.

Kampuni hiyo inaendelea kununua malighafi muhimu kama mtama, shayiri na mahindi kutoka kwa wakulima wa ndani kupitia mpango wake wa Local Content Sourcing, hatua inayochangia kuinua uchumi wa vijijini, kuongeza ajira na kupunguza uagizaji wa malighafi kutoka nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TBL Plc, Michelle Kilpin, amesema Wakulima kwetu si wasambazaji wa malighafi pekee bali ni wadau wetu wa maendeleo. Tunajivunia kushirikiana na maelfu ya wakulima nchini, tukiwapatia masoko, vifaa, mafunzo na msaada wanaohitaji ili kufanya kilimo kwa njia endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa TBL Plc, Neema Temba, ameongeza Tunaamini mkulima anapofanikiwa, sote tunafanikiwa. Ndiyo maana tunawekeza katika kuimarisha mfumo wa kilimo nchini. Kupitia ushirikiano huu wa kimkakati, zaidi ya wakulima 4,500 wanapata mafunzo, ushauri wa kitaalamu na masoko ya uhakika ili kuongeza uzalishaji endelevu.

Kama sehemu ya mpango huo, kampuni hivi karibuni iliandaa “Siku ya Wakulima wa Mtama”, tukio lililowakutanisha mamia ya wakulima, wataalamu wa kilimo na wadau mbalimbali kujadili mchango wa zao la mtama katika kukuza kilimo endelevu na usalama wa chakula. Shughuli hizo zilijumuisha kutambua mchango wa wakulima, kubadilishana maarifa, kukabidhi vifaa vya kilimo na kuonesha uhakika wa soko kwa mazao yao.

Mpango wa TBL Plc wa kusaidia wakulima unajumuisha:
• Mafunzo juu ya mbinu bora za kilimo, afya ya udongo na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
• Upatikanaji wa vifaa vya kilimo kupitia ubia na wasambazaji na taasisi za kifedha.
• Soko la uhakika na malipo ya wakati kwa mazao yanayotumika katika utengenezaji wa vinywaji.

Wakulima wanaonufaika na mpango huu wanatoka katika maeneo yanayokumbwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Dodoma, Arusha, Kilimanjaro Magharibi na Manyara. TBL Plc inasema mikakati yake inalingana na ajenda ya serikali ya kukuza kilimo na viwanda, na itaendelea kushirikiana na serikali za mitaa, vyama vya wakulima na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha manufaa ya muda mrefu.