March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAWA yatoa elimu Kisiwa cha Ijinga kunusuru wananchi na wanyama hatari

*Wananchi waanza ujenzi wa shule ya sekondari kuwanusuru watoto dhidi ya hatari ya viboko,

*Waiomba Serikali kusaidia kukamilisha ujenzi wa sekondari

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Magu

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA),kituo cha Mwanza ,imetoa elimu juu ya namna ya kuepukana na madhara yatokanayo na wanyamapori hatari na waharibifu kwa wanafunzi na wananchi wa Kisiwa cha Ijinga kilichopo wilayani Magu mkoani Mwanza ambako viboko wamezagaa kwa wingi.

Ikumbukwe kuwa watoto wanaoishi kisiwani humo hulazimika kuvuka maji ambayo ni hatari kwa maisha yao kutokana na uwepo wa viboko kufuata elimu ya sekondari ng’ambo kijiji cha Shinembo, Kata ya Kahangara.

Akizungumza na wananchi na wanafunzi wa shule ya msingi Ijinga,Mhifadhi kutoka TAWA Mwanza,Omary Mhando, amesema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuwajengea uwezo wananchi namna ya kujikinga na madhara ya viboko na wanyama hatari na waharibifu.

Ambapo amesisitiza kuwa kinga ni bora kuliko tiba na elimu hiyo inalenga kuokoa maisha ya watoto na wananchi kwa ujumla kwa kuwapa maarifa ya kuishi kwa tahadhari katika mazingira yenye wanyamapori.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa nyara ni sehemu ya mnyama pori aliye hai au aliyekufa, na kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi Sura ya 283 Kifungu cha 4(1), wanyamapori ni mali ya umma chini ya dhamana ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya wananchi wote. Hivyo, jukumu la kulinda rasilimali hizo ni la kila Mtanzania.

Amewahimiza wanafunzi na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa kwa njia sahihi wanapomuona mtu anamiliki nyara za Serikali bila kibali, kama ngozi ya mamba, jino la kiboko au kichwa cha mnyama pori.

Badala ya kutumia nguvu, watoto wametakiwa kutoa taarifa kwa mwalimu wao kwa siri, ambaye atawasiliana na Mwenyekiti au Mtendaji wa Kijiji ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Amefafanua kuwa sheria inamlinda mtoa taarifa ili asipate madhara yoyote. Pia amesisitiza kuwa kufuga wanyamapori kama fisi au mamba bila kibali ni kosa, na taarifa zinapaswa kutolewa kwa siri kupitia viongozi wa kijiji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ijinga, Shabani Shirikale, ameishukuru TAWA kwa elimu hiyo na kuiomba Serikali kuunga mkono juhudi za wananchi za kujenga shule ya sekondari kisiwani hapo.

Amesema wananchi wameamua kwa pamoja kujenga shule hiyo kwa nguvu zao ili kuwanusuru watoto wanaolazimika kuvuka maji kila siku kufuata masomo Kijiji cha Shinembo, Kata ya Kahangara.

Ameeleza kuwa watoto hao huamka alfajiri na kukumbana na hatari ya viboko wanapovuka maji, hali inayowalazimu wakati mwingine kuchelewa kufika shuleni kutokana na kukimbizwa na wanyama hao. Kutokana na changamoto hiyo, wananchi walikaa kikao cha kijiji na kuamua kujenga shule ya sekondari ili kupunguza umbali na hatari zinazoweza kuwakumba watoto wao.

Hata hivyo,ameiomba Serikali kusaidia kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ambao mpaka sasa upo hatua ya boma.

Naye Mtendaji wa Kijiji cha Ijinga, Kushoka Pastory, amesema elimu ya wanyamapori iliyotolewa shule ya msingi Ijinga itawasaidia wanafunzi kujikinga na wanyama hatarishi.

“Kupitia elimu hii niwaombe wananfunzi msiende kuogelea kwenye mabwawa na ziwani,muwe na tahadhari ya wanyama hawa hatari na waharibifu,”amesema Pastory.