March 26, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASHICO ya pokea kontena tano za samani kwa ajili ya MV.Mwanza

 Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

KAMPUNI ya Meli Tanzania (TASHICO) imepokea shehena ya makontena yaliobeba samani mbalimbali zitakazofungwa ndani ya meli ya MV.Mwanza, ili kukamilisha ujenzi wake na kuanza kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.

Shehena hiyo imewasili Machi 24,2025 Bandari ya Mwanza Kusini na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.

Akizungumza baada ya kupokea kontena tano kati ya tisa, Makilagi amesema kuwa mradi wa ujenzi wa meli ya MV.Mwanza ni wa kimkakati unaotekelezwa na Serikali kupitia TASHICO, kwa gharama ya dola za Marekani milioni 51.8, sawa na shilingi bilioni 123 za Kitanzania.

Amesema kupokewa kwa samani hizo ni hatua muhimu katika kukamilisha mradi huo unaotarajiwa kukamilika  Mei mwaka huu, hadi sasa mradi umefikia asilimia 96 ya utekelezaji, na meli inatarajiwa kuanza kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo baada ya samani kufungwa.

“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani, mradi huu ulikuwa umefikia asilimia 40, na malipo ya mkandarasi yalikuwa asilimia 30. Hadi sasa, mkandarasi ameshapokea Dola za Marekani milioni 48.4, sawa na bilioni 115.9, ambayo ni asilimia 93 ya gharama alizolipwa,” amesema Makilagi.

Amesema mradi huu ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuendeleza Mkoa wa Mwanza na kuufanya kuwa kitovu cha biashara na uchumi Kanda ya Ziwa na nchi za Maziwa Makuu kwani ni Mkoa wa pili kwa kuchangia pato la taifa kwa asilimia 7.

Pia ametoa wito kwa uongozi wa TASHICO kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na ubora unaohitajika, ili kukidhi matarajio ya Serikali ya kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji.

l

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TASHICO, Amina Mtibampema, amesema ujenzi wa meli hiyo ulianza mwaka 2020 ambapo kidogo kutokana na ucheleweshaji wa vifaa kufuatia janga la Covid-19.

“MV Mwanza itazinduliwa Mei 2025, baada ya samani kufungwa kuanzia daraja la kwanza hadi la uchumi. Mitambo ya meli tayari imeshafungwa na imeshafanyiwa majaribio kutoka Mwanza hadi Bukoba na kurudi. Meli hii itaufungua uchumi wa kampuni, watumishi, wananchi, na taifa kwa ujumla,” amesema Mtibampema.

Awali, Meneja wa mradi huo, Mhandisi Vitus Mapunda, amesema makontena mengine manne yako njiani hivyo itachukua muda kidogo kufunga samani hizo na kisha kufuata taratibu za ukaguzi wa ubora wa chombo, utakaofanywa na TASAC kabla ya meli kuanza kutoa huduma.

“Meli ina sheria kali ukilinganisha na vyombo vingine. Mifumo tayari imekamilika na ilishafanyiwa majaribio kazi iliyobaki haihitaji maarifa makubwa,baada ya meli kukamilika Mei 31, 2025, kabla ya kuanza safari za kibiashara, itafanyiwa majaribio ya pili ikiwa na wataalamu wa TASAC,”.