November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF yatoa waraka wasio na sifa
miradi ajira za muda waondolewe

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

UONGOZI wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umetoa waraka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Maafisa Ufuatiliaji kupitia orodha za watu walioandikishwa kufanya kazi kwenye miradi ya ajira za muda na kuwaondoa wale ambao hawaruhusiwi kufanya kazi kwenye miradi hiyo.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha TASAF imeeleza kwamba kwenye utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya ajira ya muda wazee, watu wenye ulemavu, wakina mama wajawazito na wenye watoto wadogo ambao hawajatimiza miaka miwili hawaruhusiwi kufanya kazi za ajira za muda kwa walengwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo washiriki wa kazi zinazotoa ajira ya muda kwa walengwa ni watu wenye uwezo wa kufanya kazi wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 65.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba utaratibu wa utekelezaji wa miradi ya ajira ya muda huchukua miezi sita, ambapo walengwa hufanya kazi kwa siku kumi kwa kila mwezi.

“Kila kaya ambayo inashiriki katika ajira za muda kwa walengwa inaandikisha watu wawili, ambapo mtu mmoja kutoka kwenye kaya ndiye atashiriki kazi- kwa wakati mmoja,” imefafanua taarifa hiyo na kuongeza;

“Utekelezaji wa miradi ya ajira ya muda huchukua miezi sita, ambapo walengwa hufanya kazi kwa siku kumi tu kwa kila mwezi. Kwa siku mlengwa anatakiwa kufanya kazi kwa muda usiozidi saa nne ili aweze kupata muda wa kufanya shughuli nyingine.”

Muonekano wa barabara inayounganisha Mtaa wa Majengo na Kijiji cha Makanjaula, Katika Halmashauri ya Wilaya Njombe iliyotengenezwa na wanufaika takribani 70 wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Walengwa hao walinufaika na sehemu ya sh. milioni 66 zilizotolewa na mfuko huo kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. Walengwa walioshiriki kwenye mradi huo walipongeza TASAF kutokana na taratibu huo kusaidia kuwaingizia kipato ambacho kimewawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ya kuwaingizia kipato.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wasimamizi wanaopanga kazi za walengwa hawatakiwi kuwapangia kazi watu hao na wanapaswa kutoa taarifa kwa wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Mradi (CMC) na Waratibu ili majina ya watu hao yaondolewe kwenye orodha ya watu walioandikishwa kufanya kazi za ajira ya muda.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba kaya yenye watu ambao hawaruhusiwi kufanya kazi za ajira ya muda watapokea ruzuku ya msingi.

Aidha, waraka huo wa TASAF umesisitiza utoaji wa elimu kwa viongozi wa jamii, wasimamizi na walengwa kuhusu taratibu za utekelezaji wa miradi ya ajira za muda kwa kaya za walengwa utaendelea kutolewa katika kipindi chote cha utekelezaji.

Miradi ya ajira ya muda kwa walengwa wa TASAF ni utaratibu wa utekelezaji miradi ya jamii yenye kutumia nguvu kazi, inayoshirikisha walengwa kufanya kazi na kulipwa ujira.

Miradi hiyo inawezesha jamii kupata rasilmali /miundombinu inayotoa huduma na ujuzi kwa jamii kupitia ushiriki wao katika kutekeleza miradi hiyo.