December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF yarahisisha upatikanaji
huduma za afya wananchi Kitisi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajiraOnline, Makambako

WANANCHI wa Kata ya Kitisi katika Halmashauri ya Mji Makambako, mkoani Njombe waeondokana na changamoto ya kupata huduma za afya mbali baada ya zahanati ya Kitisi iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuanza kutoa huduma.

Hayo yalisemwa na wananchi wa kata hiyo pamoja na wauguzi walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea zanahati hiyo ili kujionea jinsi ilivyoweza kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili wananchi hao.

Muuguzi Daraja la Pili wa zahanati hiyo, Grace Ngule amesema mwishoni mwa wiki kwamba zahanati hiyo ilianza kutoka huduma mwaka jana na kwamba imetatua changamoto nyingi kwa sababu kabla ya kujengwa wananchi walikuwa wanapata huduma mbali na makazi wanayoishi.

“Kwa hiyo baada ya zahanati kujengwa imesaidia sana wananchi, kwani wanapata huduma jirani na makazi wanayoishi na inahudumia wananchi wengine wanaotoka nje ya Kata ya Kitisi,” amesema Ngelu.

Muuguzi Daraja la Pili wa Zahanati Kitisi, Grace Ngule, akihudumia wagonjwa kwenye zanahati hiyoa ambayo imejengwa na TASAF

Ametaja huduma zinazotolewa kwenye zahanati hiyo kuwa ni huduma za mama na mtoto, huduma ya kliniki kwa watoto chini ya miaka mitano, huduma endelevu kwa wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na zile za uzazi wa mpango kwa wanawake na wanaume.

Aidha, amesema wanatoa chanjo kwa watoto. Kuhusu wagonjwa wanahudumiwa kwa wingi kwenye zahanati hiyo, Ngelu alisema ni watoto chini ya miaka mitano kwa sababu katika Halmashauri ya Mji wa Makambako hali ya hewa ni ya baridi , hivyo wengi wanasumbuliwa na nimonia.

Amesema kwa siku wanahudumia wagonjwa 15 hadi 20 mbali na wale wanaofika kwa ajili ya kupata dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na wale wa uzazi wa mpango.

Amesema tangu Zahanati ya Kitisi ianze kutoa huduma imesaidia wanaotumia dawa za kufubaza VVU, kwani hawazifuati mbali kama ilivyokuwa awali na kwamba wametengewa siku maalum kwa ajili ya kuwahudumia.

Naye Diwani wa Kata ya Kitisi, Navy Sanga ameishukuru TASAF kwa ujenzi wa zahanati hiyo akisema umesaidia wananchi kupata uhakika wa matibabu jirani na makazi yao.

Diwani huyo ameshauri zahanati hiyo iwe inatoa huduma kwa saa 24 ili wananchi wanaopata changamoto usiku waweze kupata huduma bila usumbufu.

Baadhi ya waandishi wa habari na maofisa wa TASAF wakijadiliana jambo baada ya kujionea jinsi Zahanati ya Kitisi ilivyorahisisha utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Mmoja wa wananchi, Rehema Ndomba, ameishukuru Serikali kupitia TASAF kwa ujenzi wa zahanati hiyo, kwani imekuwa mkombozi kubwa kwao ikilinganishwa na kipindi haijajengwa.

Naye Hoseah Kyando (62), amesema tangu zahanati hiyo imeanza kutoa huduma yeye amekuwa mmoja wa wanufaika kwa kupata huduma, na ile kero ya kwenda nje ya kata hiyo kufuata matibabu haipo tena.