Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
MRADI wa kunusuru kaya maskini (TASAF) umejenga vyumba viwili vya madarasa katika shule Shikizi ya Vumilia iliyopo katika Kitongoji cha Vumilia, Kijiji cha Kamama, Kata ya Goweko Wilayani Uyui kwa gharama ya sh mil 40.
Hayo yamebainishwa jana na Mbunge wa Jimbo la Igalula Venant Protace alipokuwa akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Sangu aliyetembelea Wilaya hiyo kujionea maendeleo ya mradi wa TASAF.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia kiasi hicho cha fedha kupitia mradi wa TASAF kwani kimesaidia sana kuboresha mazingira ya shule hiyo iliyobuniwa na wananchi na kuwezesha watoto wao kupata elimu.
‘Watoto wetu walikuwa wanatembea umbali mrefu sana kwenda shule mama ya msingi Kamama lakini baada ya wananchi kuchangishana ili kuanza ujenzi wa shule hii na serikali kuwaunga mkono, sasa watoto wanasomea hapa’, ameeleza.
Diwani wa kata hiyo Shaban Katalambula (CCM) amesema kuwa shule hiyo ambayo imeanza miaka 4 iliyopita sasa hivi ina watoto 135 wa awali hadi darasa la la 3 na imegharimu kiasi cha sh 51.2 na wananchi walichangia zaidi ya sh laki 6.
Amepongeza serikali kwa kuwapatia kiasi cha mil 40,000 kupitia mradi wa UVIKO-19 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba 2 vya madarasa vilivyoanzishwa na wananchi na kiasi cha sh mil 40,000 za TASAF kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 2.
‘Shule yetu sasa ina vyumba 4 vya madarasa, ofisi ya mwalimu na matundu 4 ya vyoo na watoto tayari wanasomea hapa hapa na tuna boma 1 ambalo halijakamilika, tunakuomba utusaidie ili shule yetu ikamilike haraka na kusajiliwa’, amesema.
Akitoa salamu za serikali Naibu Waziri Deus Sangu amepongeza wakazi wa Kitongoji hicho kwa juhudi zao kubwa za kimaendeleo, aliwahakikishia kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia inawajali sana.
‘Mheshimiwa Rais aliwaletea fedha za Uviko 19 kiasi cha sh mil 40 kwa jili ya ujenzi wa madarasa 2 katika shule yenu pia akawaletea sh mil 40 zingine za mradi wa TASAF ili kuongeza vyumba vingine 2 ili watoto waanze kusoma’, ameongeza.
Naibu Waziri ameahidi kuwachangia bati 50 kwa ajili ya kuezeka boma la darasa lililopo ili kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa, aidha aliagiza Uongozi wa halmashauri hiyo kuweka mkakati wa kumaliza majengo yanayotakiwa ili kuharakisha usajili wa shule hiyo.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria