January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF na Wadau wakutana kufanya mapitio ya awamu ya tatu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF pamoja na Wadau wa Maendeleo wanakutana kufanya mapitio ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF. Kikao hicho cha wiki mbili kimefunguliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamaga katika ukumbi wa Mikutano wa TASAF Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wadau ambao wanachangia utekelezaji wa Mpango wa TASAF ambao ni Benki ya Dunia, Mashirika ya Umoja wa Mataifa ya ILO, WFP na UNICEF. Wengine waliohudhuria ni wawakilishi kutoka SIDA, Umoja wa Nchi za Ulaya (EU), Ubalozi wa Uswisi, Ubalozi wa Norway, Bill and Melinda Gates Foundation na FSDT. Aidha wawakilishi kutoka Halmashauri za Kagera, Magu, Chunya na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar wamehudhuria.

Mwenyekiti Mwenza wa Kikao hicho ambaye pia ni Kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia nchini Tanzania, Michele Zini, aliipongeza TASAF kwa kazi nzuri ambayo imefanyika kupitia miradi ya Ajira za Muda, Kujenga Uchumi wa Kaya na Ukamilishaji Fedha. Amesema Benki ya Dunia pamoja na Wadau wengine ambao wanachangia utekelezaji wa TASAF wameridhishwa na utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu na wanajivunia mafanikio ya Walengwa ambao wamepiga hatua katika kujikwamua kiuchumi na kuwapatia watoto wao mahitaji yao ya msingi.

Wakati wa Vikao vya Mapitio, Washiriki hupata nafasi ya kwenda kwenye Maeneo ya Uekelezaji na kufanya mazungumzo na Walengwa, Watendaji na Viongozi kuhusu utekelezaji. Hata hivyo katika kipindi hiki, ziara za kwenye maeneo ya utekelezaji hazitafanyika na badala yake wawakilishi waliohudhuria kutoka maeneo ya utekelezaji watatoa taarifa za utekelezaji wa maeneo yao.

Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa TASAF utahusisha kujadili taarifa za utekelezaji, kubainisha changamoto za utekelezaji na hatimae kuja na mapendekezo ya kuboresha kipindi kilichobaki na kitakachofuata.

Akizungumzia utekelezaji wa Kipindi hiki, Michele alisema pamoja na kwamba toka kipindi cha pili cha Mfuko wa TASAF kilipozinduliwa, kulitokea matukio mengi yaliyosababisha kuchelewa kuanza utekelezaji hata hivyo kazi zote zilizopangwa zilifanyika kwa ufanisi ikiwemo walengwa wa zamani kuhakikiwa, walengwa wapya kutambuliwa na kulipwa stahili zao ndani ya dirisha la malipo lililofunguliwa mwezi Januari 2022. Kaya za Walengwa wa Kipindi cha Kwanza wamewezwa kulipwa malipo yao kwa mikupuo miwili. Walengwa wapya na Kipindi cha Pili wamelipwa mkupuo mmoja wa kwanza na kiasi cha fedha kilicholipwa ni jumla ya shilingi 51.1 bilioni.

Mbali na malipo kwa Walengwa, utekelezaji wa Miradi inayotoa Ajira za Muda kwa Walengwa na kuboresha miundombinu imetekelezwa katika Halmashauri 51 na jumla ya miradi 3,185 imeibuliwa. Miradi hii inatarajiwa kutoa ajira kwa Walengwa 195,000 ambao watalipwa jumla ya shilingi bilioni 36 kama ujira wa kushiriki katika kazi hizo kwa mwaka 2021 – 2022 katika Vijiji/Mitaa/Shehia 2,349 za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mpango mwingine ambao unatekelezwa ndani ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya TASAF ni Mpango wa Kukuza Uchumi wa Kaya. Utekelezaji wa mpango unaendelea ingawa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ikiwemo kuangalia namna bora zaidi ya kuwawezesha Walengwa kuweza kukuza uchumi wa kaya zao.

Lengo la mapitio ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF ni kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha utekelezaji na kujadili namna bora ya kukamilisha kipindi hiki ambacho kinatarajiwa kukamilika 2023. Michele amewataka washiriki kujadili namna bora ya kukamilisha kipindi cha pili huku akiwa na matumaini kwamba Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha walengwa ambao ni kaya zinazoishi katika mazingira duni wanawezeshwa ili kukidhi mahitaji ya msingi.  

Aidha Michele amegusia uwezekano wa  kuongeza muda wa utekelezaji wa Kipindi hiki cha Pili ili kukamilisha mipango iliyowekwa. Amewataka washiriki kutumia muda wa majadiliano kuja na mapendekezo ya muda utakaohitajika kukamilisha mipango ya Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu. 

Michele amesema kwa niaba ya Wadau wote wa Maendeleo ambao wamekuwa wakichangia shughuli za TASAF kwamba wameridhishwa na utekelezaji na wako tayari kuendelea kuchangia utekelezaji wa Mpango huu wa TASAF ili kuhakikisha kwamba Walengwa wanapata ruzuku zao ipasavyo. Amemalizia kwa kuwashukuru wote wanaohusika katika utekelezaji kuanzia ngazi ya Jamii, Halmashauri, Mikoa, Taifa na  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Kipindi cha Pili na pia kuja na mpango nzuri wa utekelezaji wa kukamilisha Kipindi kilichobakia na kuandaa Awamu inayofuata.

Kwa nyakati tofauti mkutano huu ulihusisha pia mazungumzo na Katibu Mkuu Ikulu Dkt. Moses Kusiluka, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa  Rais Ndugu Idarous Fairia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mpango Bwana Emmanuel Tububa


Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga akifungua kikao cha Mapitio ya Kati ya Utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF.


Kiongozi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Tanzania, Michele Zini, akifungua kikao cha Mapitio ya Kati ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF

Baadhi ya washiriki wakifuatilia ufunguzi wa  kikao cha Mapitio ya Kati ya Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF.

Watumishi wa TASAF katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo wanaochangia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF baada ya kufunguzi wa kikao cha Mapitio ya Kati ya Kipindi cha Pili cha TASAF.