November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF inavyoongeza kipato kwa kaya maskini Namtumbo

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

TAFITI zinaonesha kuwa, watu tofauti tofauti hufasiri maana ya umasikini kwa njia mbalimbali. Wengine kwa kawaida hufikiria juu ya umasikini kwa kuangalia uwezo wa watu katika kununua mahitaji yao na kuuza bidhaa zao. Ingawa wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanabainisha kuwa, fasiri ya umasikini ni kubwa zaidi.

Kuna fasiri ya kuzingatia matatizo ya kuwa na mgawanyo sawa katika kupata elimu na afya bora, kuwa na heshima na hadhi katika jamii, kujisikia kuwa una uwezo wa kutatua tatizo lolote linalotokea katika maisha yako na hivyo kuwa na matumaini ya maisha.

Kwa hiyo kuna mengi ya kufikiria wakati unapotaka kuondoa umasikini. Kwa hakika fikra nyingi haziko wazi mpaka unapofikiria kwa makini yanayotendeka katika jamii.

Baada ya tafiti nyingi kwa nyakati tofauti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea na jitihada zake za kuhakikisha inatafiti, inashirikisha na inatoa jawabu la changamoto ya umaskini ikiwemo kuzijengea uwezo wa kitaalam na kifedha kaya maskini ili ziweze kujitegemea.

Kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha uchumi kwa kaya zote, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika zote Tanzania Bara ,Unguja na Pemba.

Dhumuni la mpango huo ni kuziwezesha kaya maskini kuongeza kipato na fursa za kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu katika kaya.

Lengo la Serikali la kuziwezesha kaya maskini kuongeza kipatao na fursa kwa kuzipatia kaya ruzuku ya fedha taslimu ili ziweze kumudu mahitaji ya msingi limeanza kuonesha mafanikio baada ya kaya zilizokuwa katika hali mbaya ya kutomudu hata kupata mlo mmoja kwa siku zimeanza kupata milo mitatu na kuweza kuboresha maisha yao.

Wilayani Namtumbo Mkoa wa Ruvuma katika Kijiji cha Litola, Asia Luambano ni mmoja wa akinamama anayenufaika na mpango huyo ambaye anaboresha maisha yake kupitia ruzuku ya fedha ya kunusuru kaya maskini kwa kuanza na kujijengea nyumba yake aliyoizeka mabati na hivi sasa anajikita katika biashara ndogondogo za kuuza ndizi katika kijiji hicho.

Katika Kijiji cha Namahoka wilayani Namtumbo, Awetu Ngonyani anatumia ruzuku ya kunusuru kaya maskini anayopata kwa ajili ya kufuga mbuzi,kuku na mabata huku akiwa ana nyumba ambayo ameijenga kupitia ruzuku ya kunusuru kaya maskini na anafanya kazi ya kuuza dagaa kijijini hapo.

Maisha ya akina mama hao kabla ya mpango wa serikali wa kunusuru kaya maskini ,maisha yao yalikuwa magumu hata ya kumudu mlo mmoja kwa siku hali iliyoweza kubadilisha maisha yao kwa kupitia mpango wa serikali wa kunusuru kaya hizo.

Katika vijiji vya Wilaya ya Namtumbo vinavyonufaika na mpango huu ,kaya maskini zimebadili maisha yao kutoka mlo mmoja hadi kufikia milo mitatu.

Pia pamekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na elimu ya msingi kutoka katika kaya ambazo awali zilikuwa hazina uwezo wa kupeleka watoto wao shule kwa kushindwa kumudu kuwahudumia watoto kwa kuwanunulia mahitaji ya msingi ya shule.

Kupitia mpango huo kaya maskini zinaweza kuwanunulia watoto sare za shule madaftari ,kalamu,peni viatu kwa watoto wao huku wakipata huduma za matibabu ya afya kupitia mfuko wa hifadhi ya jamii CHF.

Mpango huu wa kunusuru kaya maskini unatoa ruzuku za aina mbili yaani ruzuku ya msingi ambapo kaya inayoandikishwa kwenye mpango hupata kiasi cha shilingi 10,000 kwa mwezi na ruzuku ya pili ni ile inayotegemea kutimiza masharti ya elimu na afya.

Mchakato wa malipo kwa walengwa hufanyika kila baada ya miezi miwili kwa kutoa fedha taslimu kwa uwazi na uhakika na kigezo kikuu cha malipo haya ni uhakika wa malipo kutolewa kwa waliokusudiwa kulingana na orodha ya malipo.

Taratibu za maandalizi malipo huanza kwa kuandaa orodha ya malipo kwa halmashuri zote za wilaya,miji na manispaa na majiji kufanya maandalizi ya malipo,kufanya uhawilishaji na kisha kutoa taarifa ya malipo kwa walengwa na pia kufanya usuluhishi wa marejesho ya malipo.

Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashuri ya Wilaya ya Namtumbo inasaidia kaya maskini kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii,huelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutumia fedha vizuri kuleta maendeleo na kupunguza umaskini wa kipatao.

Perez Kamugisha ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo anasimamia utoaji wa mikopo kwa kaya maskini 5,555 ambapo jumla ya shilingi 3,639,896.00 katika vijiji 42 vya mradi zinawanufaisha.

Mkuu huyo anabainisha, uundaji wa vikundi visivyo rasmi vya kuweka na kukopa VICOBA husimamiwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kuna jumla ya VICOBA 52 vyenye wanachama 708.

Vikundi ambavyo vina mtaji wa shilingi 14,858,000 na jumla ya shilingi 11,954,000 hutumika kukopeshana kwa wanachama wapatao 387 kutoka katika VICOBA hivyo.

Mratibu wa TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Raphael Mponda anaendelea na uhamasishaji kwa wanufaika wa fedha za kunusuru kaya maskini ilikuendelea kuboresha maisha yao.

Mponda anawahamasisha wanufaika kuwekeza fedha hizo wanazopata katika kuimarisha kilimo,mifugo na kufanya biashara ndogondogo na kuwekeza katika maisha yao.

Fedha za ruzuku ya Serikali kunusuru kaya maskini zinaboresha maisha kwenye kaya maskini kwa kuongeza kipato na fursa katika kaya mbalimbali huku kaya hizo zikiiomba serikali kuendelea kuwapa ruzuku hiyo waendelee kuboresha maisha yao kuwa mazuri zaidi.