January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF inavyofanikisha dhamira ya Samia ya kuwaondoa Watanzania kwenye umaskini

Na Reuben Kagaruki,Timesmajiraonline,Kilimanjaro

SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha inawakwamua Watanzania kwenye umaskini.

Juhudi hizo zinaonekana kwa macho ya Watanzania wengi, ambapo hatua mbalimbali za kuwaondoa kwenye umaskini zinachukuliwa kila kona ya nchi yetu.

Miongoni mwa jitihada hizo ambazo zimeleta matokeo chanya ni kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao unatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa. Tangu Rais Samia aingie madarakani mwaka 2021, mafanikio makubwa kupitia TASAF yamezidi kupatikana.

Tumeshuhudia Mfuko huo ukitekeleza miradi mingi kwa kujenga miundombinu ya maji, madarasa, nyumba za walimu, vituo vya afya, zahanati na nyumba za watumishi wa kada ya afya.

Kujengwa kwa miundombinu hiyo kumewezesha wananchi kupata huduma za sekta husika karibu na wao ikilinganishwa na kipindi ambacho TASAF ilikuwa haijaanzishwa.

Lakini pia baada ya kuanzishwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unaotekelezwa na TASAF, walengwa wengi hali zao za maisha zimebadilika, ambapo wengi wana uwezo kumudu kuendesha maisha yao kuliko hata walioko nje ya mpango huo.

Walengwa wa mpango huo waliozungumza na wahariri pamoja na waandishi wa habari mkoani Kilimanjaro, wanakiri maisha yao kubadilika na wapo tayari hata kuondolewa kwenye mpango huo ili kupisha wengine anaoishi kwenye umasiki.

Baadhi ya walengwa hao katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro wanasema kupitia fedha ruzuku ambayo wamepata kutoka TASAF imewasaidia kuanzisha miradi ambayo imewawezesha kujenga nyumba, kuwa na uhakika wakusomesha watoto, kuwapatia huduma za afya na kuwa na uhakika wa chakula.

Wanasema wakati wanaingizwa katika Mpango huo walikuwa na hali ngumu kiuchumi, kwani hata uwezo wa kula mlo mmoja kwa siku ilikuwa ngumu.

Lakini wanasema kupitia ruzuku wanayopata TASAF na mafunzo ambayo wamekuwa wakipatia kuhusiana na namna ya kutumia ruzuku hiyo kujiletea maendeleo, maisha yao yamebadilika.

ambapo sasa wanaweza kuendesha maisha nje ya Mfuko, kwani wengi wao wamekuwa wajasiriamali pamoja na kujiunga kwenye vikundi vya kuweka akiba na kukopa.

Mbali ya ruzuku, wanapongeza elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha ambayo kwa sehemu kubwa imewafanya kuwa na uwezo wa kumudu maisha yao.

Shufaa Hassan (56) Mkazi wa Kata ya Karoleni, Mtaa Kilimani Manispaa ya Moshi, akiwa kwenye duka lake alilolianzisha baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF ambapo kwa siku mauzo yake ni kati ya sh. 40,000 hadi 50,000. kwa siku.

Walengwa wanampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondoa kwenye umaskini na kwamba wanastahili kuondolewa kwa sababu wanajimudu tena kuliko wale ambao hawapo kwenye mpango kwa sasa.

“Kwa kweli tunamshukuru Rais Samia kwa kuendeleza mpango huu, ameweza kutuondoa kwenye umasikini.

Ninaweza kujimudu nipo tayari kuondolewa kwa hiari ili nipishe wengine,” alisema mlengwa wa TASAF, Valeria Teti (56) mkazi wa Kata ya Boma Mbuzi, Mtaa wa Relini Halmashauri ya Manispaa Moshi na kuongeza;

Anasema anaishukuru TASAF kwa msaada mkubwa ambao wamempatia, kwani amefaidika na uwepo wa Mfuko huo huku akisimulia hali ngumu ya maisha aliyokuwa akiishi kabla ya kuingizwa katika mpango wa Mfuko.

Pia anasema elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa fedha ambayo ameipata kutoka TASAF imemuwezesha kuwa na uwezo mkubwa wa kutunza fedha, kufanya biashara ndogo ndogo, kufuga kuku hadi kujenga nyumba nzuri ya kuishi.

Akielezea zaidi, Teti anasema alianza kupata ruzuku ya TASAF mwaka 2015 akianza na ruzuku ya sh. 46,000 kiasi ambacho kilimwezesha kuanzisha mradi na kusomesha watoto.

“Baadaye kadiri nilivyokuwa nikipata ruzuku nilikuwa naigawa, fedha kidogo natumia kununua chakula na zingine kuanzisha mradi wa kufuga kuku wa kienyeji,”anasema Teti na kuongeza;

“Kupitia ruzuku ya TASAF nimeweza kufuga kuku, nikaanzisha mradi wa kuuza maandazi ya kutembeza mtaani, baadae nikajiunga kwenye kikundi ambacho tulisaidiwa na wataalam wa TASAF ambapo tunawekeza hisa, tunakopeshana na baadaye tunagawana faida, hii imenisaidia sana kumudu maisha yangu tofauti na mwanzo.”

Pia anasema amejenga nyumba yenye choo na bafu ya kisasa na ameweka umeme, hatua inayomwezesha kuona yanayofanywa na Serikali kupitia televisheni yake, ambayo kabla ya TASAF alikuwa hana.

Anasema hivi karibuni alipokea ruzuku ya 350,000 kutoka TASAF ambapo anatarajia kutumia fedha hiyo kuanzisha mradi mkubwa wa kufuga kuku wa kisasa ambao utamuweza kumuingizia fedha nyingi zaidi.

“Namshukuru sana Rais Samia kwa namna ambavyo TASAF imekuwa wakiwezesha kaya masikini kwa kuzipatia ruzuku ambayo imeweza kutuinua kiuchumi, ruzuku ya TASAF imebadilisha maisha yangu.

“Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais Samia kwa kutupatia fedha kwa hali niliyonayo niko tayari kuondolewa ili wengine nao wasaidiwe.

Naye Fredelina Swai, alisema hana cha kumueleza Rais Samia kwa sababu TASAF imesomesha watoto wake wawili na sasa wapo vyuo vikuu. Anasema amejiandaa kuondoka kwenye mpango huo kwa sababu ameanzisha miradi yake ambayo inamuingizia kipato.

Swai ambaye ni mmoja ya wanufaika wa TASAF Mkazi wa Boma Mbuzi katika Manispaa ya Moshi anasema kabla ya kuingizwa katika mpango wa Mfuko huo alikuwa anaishi maisha magumu.

“Ugumu wa maisha ulinifanya nifikirie tofauti kwa sababu nilishakata tamaa ya maisha, lakini baada ya kuingizwa TASAF maisha yangu yalianza kubadilika kidogo kidogo.

Nikaanza kufanyabiashara ndogo ndogo na kufuga ng’ombe. Nikaanza kuona naanza kumudu maisha, napata hela ya kuweka na kula na watoto wangu,”anasema.

Ansema kabla ya kuingia kwenye Mpango maisha yake yalikuwa magumu hadi ilifikia hatua ya kukata tamaa kabisa hali iliyokuwa inamfanya kufikiria mambo mengi sana, lakini baada ya kupata uwezeshwaji na Mafunzo kupitia kwa waratibu wa TASAF Manispaa ya Moshi na kuazia kufanya shughuguli za ufugaji maisha yaliaza kubadilika .

“Kupitia ruzuku ya TASAF nikaanza kufuga ng’ombe, kuku, bata na baadaye sungura. Nina uhakika wa chakula na mahitaji mengine.

Nasomesha watoto wangu wawili Chuo Kikuu . bila TASAF watoto hao wasingefika kiwango hicho cha elimu, nasema ahasante Rais Samia, kwa kweli nawashukuru sana TASAF kwani wamebadilisha maisha yangu.

Niko tayari kuondolewa kwenye mpango maana wako wengine wenye uhitaji.”

Nyumba mpya aliyojenga, Valeria Teti (56) mkazi wa Kata ya Boma Mbuzi, Mtaa wa Relini Halmashauri ya Manispaa Moshi baada ya kuanza kupata ruzuku ya TASAF na kuanzisha miradi.

Naye Sarah Shengwatu ambaye ni fundi cherehani na Mkazi wa Mtaa wa Kilimani katika Kata ya Karoleni Mtaa wa Kalimani anasema kabla ya TASAF mambo yake yalikuwa magumu sana na ilifika wakati alikuwa anakula hadi mlo mmoja kwa siku, lakini kwasasa anakula milo mitatu.

Anasema awali shughuli zake za kushona alikuwa anazifanyia nyumbani, lakini kutokana na kunufaika na TASAF hivi sasa amefungua ofisi yake ya ushonaji na anamudu kulipa Kodi.

Kwa upande wake Shufaa Hassan (56) Mkazi wa Kata ya Kaloleni, Mtaa Kilimani Manispaa ya Moshi, anasema hata sasa akiambiwa aondolewe TASAF, yuko tayari, kwani ana biashara zake ambazo zinamuingizia kipato cha kati ya sh. 40,000 hadi 50,000 kwa siku.

“Nipo tayari kuondolewa TASAF ili wengine waingie nina duka langu linaniingizia kipato, kwa kweli tunamshukuru sana Rais Samia,” alisema Hassan.

Mafanikio ambayo wamepata walengwa hao na kutamani kuondolewa kwenye Mpango kwa hiari ni kielelezo cha mafanikio ya dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kuwaondolea umaskini wa Tanzania.

Kutokana na dhamira ya Serikali ya Rais Samia kuwaondolea umaskini, kwa sasa walengwa 400,000 wa Mpango wa Kunusuru Kaya wataondolewa kwenye mpango huo baada ya kujimudu kimaisha wakiwa wameanzisha miradi ya kuwaingizia kipato pamoja na kujenga makazi bora ikilinganishwa na huko nyuma.

Idadi ya walegwa 400,000 wanaotarajiwa kuondolewa kwenye mpango huo baada ya kujimudu ilitangazwa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Shedrack Mziray, wakati akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Arusha.

Mziray anasema kwa sasa tayari wameishafanya tathmini ambapo wamebaini wana walengwa 400,000 ambao sasa wanaweza kujimudi kimaisha na wanaweza kutoka katika mpango .

“Nia yetu ni kuziondoa kaya kwenye hali ya umaskini uliokithiri na baadaye ziweze kujimudu kimaisha. Tathimini yetu inaonesha walengwa 400,000 wanatakiwa kuondolewa,” alisema Mziray na kuongeza;

“Utaratibu unatutaka tunapozitambua hizi kaya na kuziingia kwenye mpango na kuanza kuzihudumia baada kipindi fulani zifanywe tathmini
ili zile kaya ambazo zimeboreka kimaisha ziweze kuondoka na kupisha kaya nyingine.”

Akieleza TASAF ilipotoka, ilipo na imefanya nini Mziray anasema TASAF ilianza mwaka 2001, ambapo imekuwa ikiendeshwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilianza mwaka 2001 hadi 2005.

Wakati huo, anasema TASAF ililenga katika kuendeleza miundombinu katika maeneo ya afya, elimu na maji.

Anasema kipindi hicho, TASAF ilijielekeza kwenye ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, vituo vya afya pamoja na zahanati. Kwa mujibu wa Mziray awamu ya kwanza ya TASAF ilitekelezwa katika halmashauri 42.

Kati ya halmashauri hizo, anasema 40 zilikuwa za Tanzania Bara na mbili za Unguja na Pemba.

“Baada ya mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza Serikali iliamua mpango huo uende nchi nzima,” anasema Mziray.

Anafafanua kwamba 2006 hadi 2012 walianza utekelezaji wa mpango wa TASAF awamu ya pili vile vile wakilenga uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya afya, elimu na maji.

“Tulijenga miundombinu mingi sana na baadaye kuanzia 2012 mwishoni ndipo Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulizinduliwa na ulikuwa utekelezwe katika kipindi cha miaka 10 iliyogawanyika katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano,” anasema Mziray.

Anasema kipindi cha kwanza cha miaka mitano kilitekelezwa kuanzia mwaka 2012 hadi 2019 ambapo waliweza kuzitambua na kuzifikia kaya maskini sana takribani milioni 1.1 nchi zima.

Hata hivyo, anasema mpango huo haukuweza kufikia maeneo yote, bali walifikia asilimia 70 ya vijiji na mitaa ikiwemo Unguja na Pemba.
“Kwa kweli tulipata mafanikio makubwa, tuliweza kupunguza umaskini uliokithiri kwa asilimia 10 ambapo walengwa waliweza kumudu kujihudumia gharama za kila siku za matumizi.

Kaya nyingi ziliweza kupeleka watoto wao shule. Kuna mafanikio mengi ambayo yalipatikana na walegwa wengi waliweza kuanzisha miradi midogo midogo ambayo iliweza kuwasaidia kujikumu na kuendelesha maisha yao,” anasema Mziray.

Kwa mujibu wa Mziray, umaskini nchini Tanzania upo wa aina mbili, wa kwanza ni wananchi kukosa matumizi ya msingi ambapo kwa sasa hivi asilimia 26 ya Watanzania wote anakabiliwa na umaskini wa mahitaji ya msingi.

Kundi lingine ni umaskini wa kukosa chakula, ambao ndiyo umaskini uliokithiri ambapo asilimia nane ya Watanzania wote wanakabiliwa na umaskini uliokithiri ambao ni wa chakula na sio wa mahitaji ya msingi.

“Asilimia 8 ya Watanzania wote wapo kwenye umasikini wa kukosa chakula, hata kupata mlo mmoja kwa siku wanashindwa. TASAF kwa vipindi vyote viwili imekuwa ikilenga umaskini wa aina hiyo,” anasema.

Anafafanua kwamba kipindi cha pili cha Kunusuru Kaya Maskini kilianza 2020 na wanaendelea nacho kwa sasa. Anasema awamu hiyo ilikuwa ikamilike mwaka 2023, lakini kutokana na umuhimu wa mpango huo, imeongezwa hadi 2025.

“Nia yetu ni kuziondoa kaya kwenye hali ya umaskini uliokithiri na baadaye ziweze kujimudu kimaisha.”Anasema Mziray na kuongeza; “Utaratibu unatutaka tunapozitambua hizi kaya na kuziingia kwenye mpango na kuanza kuzihudumia baada kipindi fulani zifanywe tathmini.

Zile kaya ambazo zimeboreka kimaisha ziweze kuondoka na kupisha kaya nyingine.”

Nyumba ya zamani aliyokuwa akiishi Valeria Teti (56) na watoto wake kabla ya kuingizwa kwenye Mpango wa TASAF. Teti ni miongoni mwa wanufaika wa TASAF ambao anatamani kuondolewa kwenye mpango huo ili kupisha wengine wanaoishi kwenye mstari wa umaskini.

Hata hivyo, Mziray anasema katika eneo hilo ndipo kunakuwa na ugumu, kwani mtu akishazoea kupata kitu fulani hasa kupewa ruzuku,halafu akaambiwa ruzuku imesimama na kutakiwa kuendelea na maisha ya kawaida,kidogo kunakuwa na changamoto.

“Lakini huo ni utaratibu na tunapoingiza kaya siku ya kwanza kwenye mpango tunawambia wahusika wanaingia kwenye mpango huo, lakini, lakini siku moja watatoka.

Hata hivyo, anasema kuna aina ya kaya wanazoziingiza kwenye Mpango hata wakae nazo milelele haziwezi kutoka kwenye umaskini kutokana na uhalisia wa zile kaya.

“Unaweza kukuta umeingiza kwenye Mpango mzee sana, hautegemei huyo akishapata ruzuku aanzishe mradi aweze kuuendesha na ukamtoa kwenye kiwango fulani cha umaskini akaweza akaendelea na shughuli zake.

Kwa hiyo watu wa namna hii wakiingia kwenye mpango hata ukae nao muda gani hauwezi kuwatathimini kuona wametoka kwenye umaskini, kwa hiyo hao lazima uendelee nao,” anasema Mziray.

Alisema watu kama hao kwenye nchi za wenzetu wamekuwa wakiingizwa kwenye pensheni, ambapo wanapata ruzuku ya kilamwezi hadi maisha yao yatakapokwisha.

“Kwa hiyo hata kwenye mpango tuna watu wa namna hiyo ambao hawategemei kwamba watahitimu, hao tutaendelea kuwa nao, lakini kuna watu ambao tumewaingia kwenye mpango wana uwezo wa kufanyakazi na tunapowapata ruzuku tunawapata mafunzo, basi haoa tunategemea wataanzisha shughuli zao za kiuchumi na baadaye zikawatoa katika umaskini,” anasema Mziray na kuongeza;

“Kwa hao, ndiyo tunawafanya tathmini na tukiwabaini kwamba amevuka kile kiwango tulichokiweka mwanzoni kwamba wamevuka kwenye umaskini basi huwa tunawapa taarifa na kuwatoa kwenye mpango.”

Anasema kwa sasa tayari wameishafanya tathmini ambapo wamebaini wana walengwa 400,000 ambao sasa wanaweza kujimudi kimaisha na wanaweza kutoka katika mpango .

Anasema kwa jinsi wanavyoanza kutekeleza uamuzi huo inawezekana wakasikika maneno maneno kwa sababu mtu alishazoea kupata ruzuku na unakuta ameanzisha mradi ana uwezo kuliko wengine ambao wako kwenye mpango.

“Lakini ukishamwambia kwamba unasitisha kumpa ruzuku waendelee na maisha yao ya kawaida, wengine wanakubali hiyo, lakini wengine wanakuwa na malalamiko.”

“Zoezi hili tunalifanya katika kipindi muhimu cha kuelekea uchaguzi, na unajua na wananchi kikifika kipindi cha uchaguzi na wenyewe wanakanyagia chini .

Kwa hiyo mkikuta hilo linajitokeza huko ujue huo ni utaratibu wa kawaida wa mpango, kwamba kaya hazitakiwe zikae kwenye Mpango milele, zinafikia kipindi ambacho zinatakiwa kujitegemea ili ziweze kuendelea na maisha yao ili kutoa nafasi kwa kaya nyingine kuingia.”

Anasema katika kipindi cha pili gharama za mpango mzima kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 ni karibia shilingi trilioni 2 na sasa hivi wameishapata ahadi ya wadau wa maendeleo.

Anasema fedha hizo zinachangiwa sehemu mbili, ambapo Serikali inachangia kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) na kutoka taasisi nyingine za kifedha, lakini sehemu kubwa ni kutoka WB.

“Kwa hiyo ukisema mkopo ina maana ni mchango wa Serikali, hizo ni fedha za Serikali itakuja kuzilipa Benki ya Dunia, Serikali imechukua mkopo Dola milioni 650 na sehemu iliyobaka ni msaada kutoka nchi marafiki wa Tanzania SIDA (Swiden) Highland, Norway na misaada kutoka Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya (EU).

Kuna mkopo kutoka nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi OPEC ambapo tulichukua mkopo wa dola milioni 50,” anasema na kuongeza;

“Huu mkopo wa OPEC umelenga katika miradi ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya elimu, maji na inafanyika kwenye mikoa mitano.” Anataja mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Njombe, mwanza, Geita na Simiyu.