September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF ilivyobadili historia Sekondari Oldonyowas, yapaisha ufaulu kwa kasi

Na Reuben Kagaruki, TimesmajiraOnline Arusha

KATI ya vikwazo vinavyosababisha watoto wengi wa Tanzania kutofikia ndoto zao za kupata elimu ni pamoja na miundombinu ya shule kutokuwa rafiki.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha wanafunzi wengi kukatisha masomo kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule na wakati mwingine kukumbana na vishawishi njiani vinavyosababisha wanafunzi wa kike kupata ujauzito.

Lakini pia shule nyingine kutokuwa na mabweni imekuwa ikilazimisha wanafunzi wakiwemo wa kike kuishi kwenye nyumba za kupanga, ambazo mazingira yake sio rafiki, hivyo ndoto zao kuishia njia.

Vikwazo vingine ni shule hasa za sekondari kutokuwa miundombinu rafiki ya kujifunzia, ikiwemo upungufu wa madarasa,  kutokuwepo kwa maabara, upungufu wa matundu ya vyoo na uzio kwa ajili ya usalama wa wanafunzi na mali za shule.

Kwa kutambua vikwazo hivyo vinavyosababisha wanafunzi wengi kushindwa kufikia malengo yao, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha shule zinakuwa na miundombinu rafiki inayowawezesha wanafunzi kupata elimu bora.

Jitihada hizo za Rais Samia zinadhihirishwa na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya shule katika mikoa mitano.

Mikoa hiyo ambayo inajengwa miradi ya miundombinu kwa fedha  kutoka OPEC ni Arusha, Njombe, Simiyu, Mwanza na Geita. Wananchi wa mikoa hiyo ni mashuhuda wa dhamira ya Rais Samia ya kuinua kiwango cha elimu. 

Wiki iliyopita wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini walishuhudia jitihada zinazofanywa na Rais Samia kupitia TASAF za kuhakikisha watoto wa Watanzaia wanapata elimu katika mazingira rafiki, ambayo yanarahisisha safari ya kuelekea kufikia ndoto zao.

Mfano mzuri ni miundombinu iliyojengwa na TASAF katika Shule ya Sekondari Oldonyowas ambayo iliyopo katika Kata ya Oldonyowas yenye vijiji vinne.

Katika shule hiyo TASAF imejenga jengo la utawala, matundu manne ya choo,  madarasa mawili, ofisi na nyumba moja ya walimu mbili kwa moja yenye choo pamoja na bafu yake.

Aidha, katika shule hiyo TASAF katika shule hiyo imejenga maabara mbili za masomo ya fizikia na jiografia, imejenga mabweni mawili ya wavulana zikiwa na matundo ya vyoo pamoja na bafu.

Aidha, TASAF katika shule hiyo imejenga hosteli mbili za wanafunzi wake zikiwa na matundu manne ya vyoo pamoja na bafu zake. Pia imejenga hosteli mbili za wavulana zikiwa na matundu manne ya choo na bafu zake pamoja na uzio wa kuzunguka sekondari. Shule hiyo ipo katika Halmashauri ya Arusha DC, mkoani Arusha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyowas, Samson Martin, anasema miradi yote imetekelezwa na TASAF kwa kuchangia asilimia 90 na kijiji asilimia 10 ya nguvu kazi na vifaa vya ujenzi.

Martin anasema miradi ya ujenzi wa miundombinu hiyo katika Sekondari ya Oldonyowas imelata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi kupata  hosteli nzuri ambazo zimepunguza umbali wa wanafunzi kutembea kwenda shuleni.

“Miundombinu hii imeongeza ufaulu kwenye mitihani ya ndani na ya kitaifa, kuimarika kwa usalama wa shule pamoja na mali,” anasema Martin.

Anazidi kufafanua kwamba kwa ujenzi wa miundombinu hiyo,  sekondari hiyo imekuwaya mfano katika maeneo ya wafugaji. “Kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Oldonyowas tunamshukuru Rais Samia kwa kuwezesha TASAF kutekeleza miradi hii kwa fedha za OPEC.

Tunaomba Serikali iendelee kushirikiana na wafadhili ili wananchi wazidi kupata miundombinu itakayowakwamua kwenye umaskini na kuinua kiwango cha elimu.”

Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Oldonyowas, Juma Bukwimba, anasema kwa niaba ya wananchi anaishukuru TASAF kupitia Rais Samia kwa kubadilisha historia ya shule hiyo. 

Bukwimba anasema kabla ya ujenzi wa miundombinu hiyo, idadi ya wanafunzi ilikuwa haifiki 300 katika shule hiyo. “Lakini baada ya TASAF kutujengea miundombinu hiyo pamoja hosteli tukawa tunapata wanafunzi wengi na wengine wanatoka nje ya kijiji cha Oldonyowas,” anasema na kuongeza;

“Uwepo wa mabweni umetuletea maendeleo makubwa katika taaluma, idadi ya wanafunzi imeongezaka hadi kufikia 647 wasichana wakiwa 353 na wavula 294.”

Anasema kabla ya ujenzi wa miundombinu hiyo pamoja na mabweni, matokeo ya kwanza ya kidato cha nne wanafunzi waliopata daraja 0 walikuwa saba na daraja la kwanza mmoja.

“Lakini kwa wakati huu wamiundombinu iliyojengwa hapa shuleni pamoja na mabweni katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana, ufaulu umeongezeka kwa asilimia kubwa. 

Tulikuwa na daraja la kwanza wanafunzi watatu, daraja la pili 19, daraja la tatu 32 na daraja la nne 35, hatukuwa na daraja 0 katika madarasa yote mawili ya mitihani ya kidato cha pili na kidato cha nne,” anasema Bukwimba.

Anasema matokeo hayo yalifanya halmashauri kuwapa pongezi kwa kuwapatia vyeti vya kutambua shule hiyo kuwa ya kwanza katika halmashauri kwa kupandisha ufaulu kwa kasi.

Mkurugengezi wa Halmashauri ya Arusha DC, Selemani Msumi, anasema kwa Arsuha TASAF kwa Arusha ina mkono mrefu sana. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TASAF, Shedrack Mziray, anasema walifanya ujenzi huo kwa kushirikiana na halmashauri pamoja na wananchi.

Anasema ujenzi wa miundombinu hiyo imesaidia sana kuondoa changamoro zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi ikizingatiwa kwamba hayo ni maeneo ya wafugaji, hivyo wanafunzi wanakaa mbali na walikuwa wakitembea umbali mrefu kuwahi shuleni.

“Lakini kwa kujenga mabweni wanakaa shuleni katika mazingira mazuri,” anasema Mziray.

Anasema miundombinu imetekelezwa kwenye mikoa mitano katika halmashauri zote. Anataja mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Njombe, Simiyu, Mwanza na Geita. 

Menyekiti wa Kamati ya Mradi,  Anael Obed Salakikya, anaipongeza TASAF kwa ujenzi wamiundombinu katika shule hiyo ambayo imeongeza hamasa ya elimu katika jamii ya wafugaji.

Anasema kabla ya shule hiyo, watoto walikuwa wanatembea umbali mrefu wa kilometa nane kwenye sekondari. “Kwa hiyo ilipotokea fursa ya TASAF wananchi tuliomba kujengewa miundombinu hiyo ambayo ilianza kujengwa mwaka 2018,” anasema. 

Anasema hatua hiyo ya TASAF iliwamasisha wananchi kujenga madarasa machache na nyumba moja ya awali.

Anasema mbalimbali ya kujenga miundombinu hiyo wananchi wa Kijiji cha Oldonyowas wenye utaalam kama mafundi walipata kazi na wale ambao hawakuwa na utaalam walipata kazi za kusaidia mafundi.

Mwanakijiji wa Oldonyowas, Urassa Samuel, anasema ujenzi wa shule hiyo umewafanya wananchi kuzidi kuwa na mwamko wa elimu, kwa sababu wameona jenzi Serikali ya Rais Samia inavyothamini Watanzania wote ikiwemo jamii ya wafugaji. 

Mwanafunzi, Esther Abeid, anasema mabweni yaliyojengwa kwenye shule hiyo yamewasaidia sana kusoma kwa uhuru. Anasema kipindi cha nyuma walipokuwa wakienda shuleni wakati mwingine wanapita kwenye makorongo, kwenye misitu wanaweza kubakwa, lakini sasa wanakaa shuleni na kusoma kwa uhuru.

Mwanafunzi huyo anampongeza Rais Samia kwa juhudi zake na kuboresha elimu nawenyewe wanaahidi kujitaidi kwenye masomo ili kuthamini mchango wake kwenye elimu.

Ujenzi ulipokuwa unaanza mwaka 2018
Hali ya majengo ya sasa yaliyojengwa na TASAF