Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Njombe
MSISITIZO wa Rais Samia Suluhu Hassan umekuwa ni kuboresho ya miundombinu katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu inayowapatia ujuzi katika mazingira rafiki.
Tangu atoe ahadi hiyo Serikali imeendelea kutekeleza kwa vitendo anadi ya Rais Samia kwa kuhakikisha inaboresha miundombinu ya elimu nchini ili kila mtoto wa kitanzania apate elimu bila kikwazo cha umbali, upungufu wa walimu, uchache wa madarasa pamoja na thamani.
Utekelezaji wa ahadi hiyo unazidi kutekelezwa kwa vitendo katika shule mbalimbali nchi zikiwemo zile ambazo wanafunzi walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kutembelea umbali mrefu kwenda shuleni, kusongamana darasani na wakati mwingine kushindwa kufikia malengo yao kutokana na mazingira ya shule kutokuwa rafiki.
Ili kudhibitisha utekelezaji wa dhamira hiyo ya Rais Samia, mwandishi wa makala haya alitembelea baadhi ya shule mkoani njombe ambazo zilikuwa zikikabilia na changamoto za wanafunzi kutembea umbali, msongamano, kukosa chakula na changamoto zingine zinazosababisha utoro zinavyopatiwa ufumbuzi.
Miongoni mwa shule ambazo tayari zimeonja radha ya dhamira nzuri ya Rais Samia ni Shule ya Msingi Umago iliyopo Halmashauri ya Mji Njombe, mkoani Njombe, Shule ya Sekondari Mlowa iliyopo Halmashauri ya Mji Makambako na Shule ya Msingi Makatani. Katia shule hizo tatu miundombinu yake ambayo imepunguza adha mbalimbali kwa wazazi na wanafunzi imejengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku wananchi wakichangia sio chini ya asilimia 10 ya nguvu kazi.
Mtanzania yeyote akifika kwenye shule hizo na kuona kazi kubwa iliyofanywa na TASAF ni wazi kwamba atakuwa balozi nzuri wa kusimuliza mafanikio ya utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia.
Mfano, katika Shule ya Msingi Umago, iliyopo Halmashauri ya Mji Njombe zimetumika zaidi ya milioni 300 kujenga madarasa nane, nyumba ya walimu, uzio, jiko na bwalo la chakula kwa wanafunzi.
Ujenzi huo umewezesha wanafunzi kuondokana adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule ya Wemba walipokuwa wakisoma awali.
Aidha, ujenzi huo umewezesha tatizo la msongamano wa wanafunzi uliokuwa ukiikabili Shule ya Msingi Wembe kupata ufumbuzi.
Mafanikio hayo yanathibitishwa na Mtendaji wa Mtaa Wemba, Christina Njogela, wakati akizungunza na Majira kuhusiana na mikakati inayochukuliwa na Serikali kutimiza dhamira ya Rais Samia kupitia TASAF.
Anasema anapongea Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia, kwani imesaidia kuboresha sekta ya elimu katika shule ya Umago kwa kuendelea kusimamia vema mfuko huo wa TASAF.
Anasema waliomba mradi huo kutokana na wingi wa wananfunzi na umbali, kwani watoto wanaosoma Wemba wengine wanatoka mbali kwenye kitongoji cha Majengo na wengine wanaishi Madati.
“Kwa hiyo kutokana na umbali huo wananchi waliibua mradi huo ili kupunguza umbali ambao watoto walikuwa wakitembea,” anasema Njogela.
Anasema hadi sasa shule hiyo ina wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la saba ambao walimegwa kutoka Wemba kwa kuangalia ujirani wa watoto kufika shuleni hapo.
Aidha anasema mwaka jana waliibua miradi mingine ya ujenzi wa madarasa matano, vyoo matundu sita, ujenzi wa jiko, bwalo la chakula na uzio.
Kwa mujibu wa Njogela miradi hiyo bado inaendelea ikiwa umefikia hatua za kukamilishwa. Anasema wanaishukuru TASAF kwa kuona shida za wananchi, kwani wananchi peke yao wasingefanikisha ujenzi wa shule hiyo.
Anasema wamejipanga kulinda miundombinu yote katika shule hiyo kwa sababu wananchi wanatambua umuhimi wake. “Kwa hiyo kwa kushirikiana na walimu na wananchi tunatoa elimu kwa wanafunzi kuhusiana na umuhimu wa kulinda miundombinu ya shule hiyo,” anasema.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Umago, Happy Kawogo, anasema shule hiyo ina wanafunzi 334 na kupitia tathimini ya mitihani ndani inafanya vizuri kitaalam. Kwa upande wa mitihani ya Taifa, alisema kwa mwaka jana wanafunzi hao hawakufanya mitihani kwa sababu bado walikuwa shule mama ya Wemba.
Alisema ujenzi wa madarasa umesaidia sana kwa sababu awali wanafunzi walikuwa ni wengi katika shule ya msingi Wemba na uwezo wa walimu kutoa maarifa kwa watoto ulikuwa ni mdogo ikilinganishwa na idadi yao.
“Kwa hiyo ujenzi wa miundombinu hii ya TASAF wanafunzi wameweza kupata maarifa vizuri na bila kusongamana darasani, hivyo tunampongeza Rais Samia kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kufanya katika sekta ya elimu,” anasema.
Kwa upande wa nyumba za walimu anasema zimeweza kusaidia kutatua tatizo la walimu wote kukaa mbali na shule. Anasema walimu wanapokuwa wanatoka mbali inapelekea ufanisi wao wa ufanyaji kazi kuwa mdogo.
Anafafanua kwamba kwa sasa wana walimu wawili wanaokaa karibu na shule. Kwa upande wa uzio, Mwalimu Mkuu Kawogo anasema unasaidia kuthibiti utoro wa wanafunzi.
“Kabla ya uzio mwanafunzi alikuwa anaenda chooni na wakati mwingine kupotelea huko huko, lakini kwa uwepo wa huu uzio wanafunzi wote wanaweza kuwathibiti hawawezi kutoroka,” alisema mwalimu Kawogo.
Mwalimu Abu Jonasy, anashukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kwa ujenzi wa shule hiyo pamoja na ununuzi wa thamani, ambao umefanya mazindira ya kufundishia wanafunzi hao kuwa rafiki.
Mmoja wa wananchi wanashiriki ujenzi wa bwalo la shule hiyo kwa kujitolea, Salah anasema aliamua kuchangia nguvu kazi kufanikisha ujenzi wa shule ya Umago ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia kuwaletea maendeleo Watanzania.
“Najikia vizuri kwa sababu shule hii itatusaidia watoto wetu na ndugu zetu. Nawaomba Watanzania waendelee kumuunga mkono Watanzania katika juhudi zake za kuwapatia wananchi elimu bora.
Aidha juhudi hizo za Rais Samia Shule ya Sekondari Mlowa ambapo zimejengwa nyunba za mbili za walimu (two in one) sawa na nyumba nne, hosteli ya wanafunzi, jengo la utawala, jiko na bwalo.
Ujenzi wa miundombinu hiyo katika Shule ya Sekondari Mlowa katika Halmashauri ya Mji Makambako mkoani Njombe imepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikikabili shule hiyo na kukwamisha utolewaji wa elimu bora.
Miundombinu katika shule hiyo imejengwa TASAF kwa sh. 355,433,812.5 na wananchi kuchangia nguvu kazi kwa asilimia zisizopungua 10.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea shule hiyo mwishoni mwa wiki kujionea miumdombinu hiyo ilivyotatua changamoto zilizokuwa zikikabili hiyo Mwalimu Mkuu, Raymond Kyando anaishukuru Serikali akisema sasa kiwango cha taaluma katika shule hiyo kimepanda ikilinganishwa na kipindi ambacho haikuwa na miundombinu hiyo.
Kyando anasema kwa ujenzi wa hosteli ya wanafunzi 72 wanaishi hosteli, huku nyumba hizo zikiwezesha familia nne za walimu kuishi jirani na shule.
“Kabla ta Serikali kutujengea hosteli wanafunzi walikuwa wanatembea mbali kilometa kilometa 24 kwenda na kurudi. Tulibaini watoto wanapata shida ilitulazimu kuweka kambi ambapo tulitenga madarasa mawili ambayo walikuwa wanalala wanafunzi wa kiume na kike,” anasema Kyando.
Anasema kutokana na changamoto ya uhaba wa hosteli kuwa kubwa wananchi kupitia mkutano wa kijiji waliomba TASAF iwajengee hosteli ambayo imekuwa mkombozi mkubwa tangu ilipojengwa.
Kyando anatoa mfano kwamba kabla ya ujenzi wa hosteli hiyo kila mwaka wanafunzi kati ya wanne hadi watano walikuwa wakipata ujauzito. “Lakini tangu tujengewe hosteli hii hatujawahi kuwa na changamoto hiyo kwa sababu hosteli hiyo imelenga wanafunzi wa kike.”
Aidha, anasema tangu kujengwa kwa hoteli hiyo kiwango cha taaluma kimepanda ambapo kwenye mitihani ya ndani na ya nje kwenye kata wanaoongoza ni watoto wa kike wa shule hiyo.
“Hivyo tunaamini kabisa uwepo wa hii hospteli umesaidia watoto wa kike na imewabadilisha kitaaluma na kuwawezesha kuelekea kutimiza ndoto zao, lakini pia vikwazo vingine vimeondoka.
“Ndiyo maana Serikali kuanzia ngazi ya mitaa na kata wakaamua sekondari hii iwe shule ya wasichana na lengo letu ni kuifanya iwe shule teule ya wanafunzi wa kike,” anasema.
Anataja sababu nyingine iliyochangia utoro ilikuwa ni kukosekana kwa chakula cha mchana. Alisema tangu shule hiyo ilipoanza kutoa chakula cha mchana kwenye bwalo ambalo limejengwa na TASAF nayo imekuwa chachu ya kupunguza utoro.
“Watoto wanaondoka shuleni saa 11 jioni sasa kama hawapati chakula cha mchana kunachangia utoro, hivyo tulianzisha kampeni ya kuwa na chakula cha mchana ambayo pia imepunguza utoro,”alisema.
Kwa upande wa nyumba za walimu zilizojengwa na TASAF, Kyando anasema zimejengwa mbili (Two in one sawa na nyumba nne) ambazo ambapo zimewezesha walilimu kuishi karibu na shule na wamekuwa wakisaidia wanafunzi wakatia wakujisomea usiku.
“Muda wote walimu wanakuwa shuleni wanasaidia wanafunzi wakati wa kujisomea usiku na muda wote wanaweza kuwafundisha,” alisema Kyando. Kuhusu jengo la utawala amesema limesaidia shughuli za kiutawala na walimu wana ofisi nzuri ikilinganishwa na hapo nyuma,”anasema.
Naye mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, Irene Mgunda anaishukuru TASAF kwa kuwajengea hosteli hiyo, kwani imewasaidia kumaliza changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo kabla ya ujenzi huo.
Alitoa mfano kwamba wazazi wake wanaishi Makambako hivyo bila kuwepo kwa hosteli hiyo asingemudu kutembea kwa miguu kwenda shuleni hapo. Alisema ujenzi wa hosteli hiyo umekuwa mkombozi kwani watoto wa kike wanaoishi nyumbani wanakumbana na changamoto nyingi wakati wa kwenda na kurudi shuleni.
Naye Esther John anasema ujenzi wa hosteli hiyo unawasaidia wakati wa usiku kupata muda wa kujisomea tofauti na yule mwanafunzi anayetokea nyumbani kwani anakuwa na majukumu mengi, hivyo anakosa muda wa kujisomea.
“Tunapotaka msaada kutoka kwa mwalimu tunaupata kutoka kwa walimu maana wapo hapa shuleni ni tofauti na mwanafunzi anayetoka nyumbani kuja shule na mara nyingi wanakumbana na vishawishi vingi,” anasema.
Kuhusu nyumba za walimu zilizojengwa na TASAF mwanafunzi huyo amesema nazo zimekuwa mkombozi, kwani wanapokuwa wanajisomea wanapata msaada kwa urahisi kutoka kwa walimu kwa sababu wanakuwepo shuleni.
Naye mlezi wa wanafunzi katika hosteli hiyo, Upendo John (24) alisema ujenzi wa hosteli hiyo umekuwa msaada mkubwa kwa jamii ya Mlowa, hasa ikizingatiwa watoto wanatoka sehemu mbalimbali na wengine wanakopita sio salama na kuna vishawishi vya aina nyingi.
Ametoa mfano wakati mwingine shuleni kuna vipindi vya ziada ambavyo vinawafanya watoke shuleni wamechelewa hivyo vinaweza kuwafanya wafike nyumbani usiku.
“Lakini wanapokuwa hosteli wanakuwa sehemu salama hivyo ni vigumu kupata vishawishi. Hosteli hii imefanya wanafunzi kuwa salama,” anasema Pendo.
Kwa kwa ujenzi wa madarasa sita, vyoo pamoja na miundombinu ya maji kumewezesha Shule ya Msingi Makatani kuanza kutoa elimu kwa wanafunzi wa Kata ya Makatani waliokuwa wakikabiliwa na adha ya kutembelea umbali mrefu.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makatani, Zawadi Salehe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na jinsi miundombinu hiyo iliyojengwa na TASAF ilivyosaidia kutatua changamoto ya wanafunzi kupata elimu mbali na wanakoishi.
Mwalimu Salehe amesema kutokana na wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda kusoma Shule ya Msingi Kiumba, Lyamkene na Ilangamoto, wazazi waliona hiyo ni kero kubwa hivyo waliibua mradi wa ujenzi wa shule.
Anasema wananchi walianza ujenzi wa shule hiyo kwa kuanza na madarasa matatu na ofisi na ujenzi wake waliufikisha hatua ya boma.
Baada ya kufikia hatua hiyo amesema walipeleka maombi TASAF ili iwasaidia kujenga shule.
Kwa mujibu wa Mwalimu Salehe, wamejengewa vyumba sita vya madarasa, vyoo na miundombinu ya maji ambavyo vyote vimekamilika na kuanza kutumika.
Anasema shule hiyo imeanza kufanyakazi kuanzia Januari, mwaka huu ikiwa na wanafunzi wa darasa la awali hadi la nne jumla wakiwa 167 wakiume 81 na kike 86.
Anasema watoto hao wamehamishiwa shuleni hapo kutoka shule ya msini Kiumba, Lyamkene na Ilangamoto na kwamba watoto walioanzia shuleni hapo kwa sasa ni wale wa darasa la awali.
Anasema ujenzi wa miundombinu hiyo unasaidia maendeleo ya kitaalum kwenda vizuri, kwa sababu shule ina walimu sita na kulingana na Ikama ya walimu na idadi ya wanafunzi inajitolesheza vizuri.
Kuhusu mwamko wa wazazi kupeleka watoto kusoma shuleni hapo, Salehe anasema ni mkubwa kwa sababu idadi ya wanafunzi inazidi kuongezeka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Makatani, Samson Lukogera (62), amesema waliamua kuomba TASAF iwasaidie ujenzi wa shule hiyo baada ya kuona watoto wanatembea umbali mrefu kwenda shule ya Kiumba na Lyamkena.
“Kwa hiyo tuliona wanafunzi hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu, hivyo tuliona tuanzishe ujenzi wa shule na tunashukuru Serikali tuliwaomba watusaidie,” alisema Lukogera.
Anasema baada ya TASAF kukubali na wananchi waliunga mkono uamuzi huo kwa kuchangia asilimia 10 ya nguvu kazi ili kufanikisha ujenzi huo.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Esther John (9) amesema anaishukuru Serikali kwani kupitia TASAF imefanikisha kuanza kwa shule na wameondokana na adha ya utembea umbali mrefu kwenda kusoma Kiumba.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika