November 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tasac yawataka abiria wa vyombo vya usafiri wa majini kuacha kutupa taka ndani ya ziwa,bahari

Judith Ferdinand,Timesmajira online,Mwanza

Imeelezwa kuwa miongoni mwa mambo yanayosababisha uchafuzi wa mazingira ndani ya ziwa na bahari ni pamoja na wananchi wanaotumia vyombo vya usafiri wa majini kutupa taka ndani ya maji wawapo safarini.

Hivyo wito umetolewa kwa wananchi kuacha tabia hiyo ya utupaji taka ziwani au baharini badala yake watupe kwenye vyombo vya kuhifadhia taka vilivyopo ndani ya vyombo hivyo vya usafiri wa majini.

Wito huo umetolewa na Ofisa Mwandamizi Ukaguzi wa Meli wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC),Nahodha Ghadaf Chambo wakati akizungumza na timesmajira online mara baada ya kumalizika kwa warsha ya waandishi wa habari wa Kanda ya Ziwa iliondaliwa na shirika hilo,iliyofanyika jijini Mwanza.

Nahodha Ghadaf ameeleza kuwa uchafuzi wa bahari au ziwa kuna sababu mbili moja ni uchafu unaotoka nchi kavu na pili ni ule unaozalishwa na meli ambapo uchafuzi wa meli ni abiria kutupa taka au chombo husika kumwaga mafuta au majitaka bila kuyaibu kwa mujibu wa sheria na masharti.

Ofisa Mwandamizi Ukaguzi wa Meli wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC),Nahodha Ghadaf Chambo kushoto wakati wa warsha ya waandishi wa habari wa Kanda ya Ziwa iliondaliwa na shirika hilo,iliyofanyika jijini Mwanza.

Ambapo amesema abiria wanaotumia vyombo hivyo vya usafiri wa majini wamekuwa na tabia ya kutupa taka ndani ya ziwa au bahari ikiwemo
chupa za plastiki au maganda ya peremende ambayo ni plastiki pia.

Ameeleza kuwa licha ya kutupa taka hizo pia wamekuwa wakitupa mabaki ya chakula ambayo kwa kiasi kikubwa yanaliwa na samaki mengine yanaoza.

“Mabaki ya chakula viumbe maji ikiwemo samaki wanaweza kumengenya na hayana madhara lakini plastiki zinakaa muda mrefu na wakila zinakuwa sehemu ya mmengenyo wa chakula wa samaki na matokeo yake baadhi ya sumu zinabaki kwa samaki mwenyewe au akafa kabla ya kuvuliwa hivyo inakuwa ni madhara makubwa kwa viumbe maji,”ameeleza Ghadaf.

Pia ameeleza kuwa sheria imewataka wawe wanatunza mazingira ya bahari na ziwa kwa kuhakikisha takataka zote zinakusanywa ndani ya chombo cha usafiri wa majini ili wakifika nchi kavu basi takataka hizo zinaenda kutupwa nchi kavu kwa kuchomwa au kwenye maeneo ambayo yanastahili kutupwa.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa uchafuzi wa baharini na ziwani vilevile unaweza kusababishwa na shughuli za kwenye chombo ikiwemo umwagaji wa maji taka bila kutibiwa.

“Kama ni meli ya abiria kuna abiria ambao wanazalisha maji taka ambayo yanatakiwa yatibiwe kisha yamwangwe ndani ya ziwa au bahari lakini yanamwagwa kwa utaratibu siyo pale pale ambapo meli imesimama bali yanamwagwa wakati meli inatembea tena umbali fulani kutoka bandarini ina kuwa mwaga huku inatembea baada ya maji taka hayo kuwa yameisha tibiwa,”ameeleza.

Vilevile ameeleza kuwa kuna uchafuzi wa mafuta yanayozalishwa na mitambo ya kwenye meli watu wakiwa wazembe wakati wanasafisha injini au injini inaweza kuwa inavujisha mafuta kwa sababu ya ubovu.

Baadhi ya washiriki wa warsha ya waandishi wa habari wa Kanda ya Ziwa iliondaliwa na shirika hilo,iliyofanyika jijini Mwanza.

“Kwaio hayo mafuta yakikusanywa na kumwangwa kwenye maji yanaleta madhara kwa madharia ya viumbe maji kwaio meli zote zihakikishe wana tibu majitaka kisha ndio wamwage ziwani au baharini na mafuta yanayokuwa yamebaki basi yahifadhiwe kwa ajili ya matumizi ya nchi kavu,”.

Amesisitiza kuwa takataka zisitupwe kwenye maji na abiria wapatie elimu juu ya kutupa taka katika vyombo vya kuhifadhia taka vilivyopo ndani ya vyombo vya usafiri vya majini na wasitupe takataka ndani ya maji zenye asili ya plastiki zinakaa zaidi ya miaka 50.

“Tukizembea katika hili tukianzia kwa mwaka huu hadi miaka 50 ijayo plastiki ambazo zitakuwa hazijaoza ndani ya ziwa zitakuwa ni nyingine sana bora chakula ukitupa kinaliwa na samaki na kingine kinaoza kinapotea hivyo tukihesabu miaka 50 ijayo kila siku watu wakitupa takataka maana yake ziwa au bahari zitaharibika samaki watapotea na sisi vilevile tutakuwa tunahatarisha maisha yetu hivyo umwagaji wa mafuta,utupaji wa taka za plastiki na vitu vingine ambavyo haviozi vina hatarisha mazingira na maisha yetu,”amesisitiza Ghadaf.

Aidha amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini kufuata sheria na masharti yaliopo kwenye leseni kwani kukuika sheria Kuna adhabu kwa ajili ya uchafuzi wa mazingira na wanafanya hivyo kwa maendeleo ya taifa na vizazi vijavyo.

“Wenye vyombo wanafahamu kuwa tasac inatoa leseni kwa chombo kilicho kikidhi ubora na masharti ya leseni ambapo miongoni mwa masharti ni utunzaji wa taka hivyo wamiliki wote wahakikkishe vyombo vyao vinakuwa na vyombo vya kutunzia taka kama walivyokubaliana katika msharti ya leseni na mtu akikiuka masharti hayo anaweza kunyanganywa leseni,kupinga faini au kufunguliwa mashitaka hivyo nawasisitiza wafuate masharti,”ameeleza.

Ikumbukwe kuwa majukumu ya TASAC ni pamoja na kuzuia uchafuzi wa mazingira ndani ziwa na bahari, udhibiti wa usalama na ulinzi wa usafiri majini, ukaguzi na usajili wa vyombo vya majini, kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji majini, utoaji vyeti kwa mabaharia, utoaji wa elimu ya usalama majini, kufanya sensa ya vyombo vya majini.