November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yajivunia mafanikio miaka miwili ya Samia

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Mbeya

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wamemueleza Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange mafanikio ya TARURA miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ndani ya miaka miwili ya Dkt. Samia, bajeti ya TARURA imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka wastani wa bilioni 275 miaka minne iliyopita na kufikia bilioni 900 kwa mwaka 2021/2022, na trilioni 1.2 kwa mwaka 2022/2023.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Mbeya Mhandisi Lilian Kimario (kushoto)alipotembelea banda la TARURA kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Dugange alielezwa mafanikiio hayo alipotembelea banda la TARURA kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Kwenye taarifa ya Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, iliyotolewa mbele ya Dkt. Dugange na Kaimu Meneja wa TARURA Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Lilian Kimario ,amesema mafanikio hayo yamechangiwa na bajeti ya TARURA kuongezeka mara tatu kwa ajili ya miundombinu ya barabara za Wilaya.

Amefafanua kuwa ongezeko hilo la bajeti ni kutokana na ukweli kuwa takribani asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijijini,mojawapo ya changamoto ya maendeleo ni kutokuwa na mtandao wa barabara za vijijini za uhakika za kuwawezesha kutoa mazao shambani na kuingiza pembejeo za kilimo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, lakini pia kuwawezesha kufikia huduma muhimu za kijamii kama hospitali, shule na masoko.

Ujenzi wa daraja la Berega lililopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro lenye urefu wa mita 140, ni moja ya miradi ya kimkakati muonekano huo ni wakati ujenzi umefikia asilimia 75, na sasa ujenzi upo zaidi ya asilimia 85.

“Kuimarika kwa miundombinu ya barabara kuna dhihirisha adhima ya Rais Dkt. Samia aliyoitoa wakati wa kuhutubia Bunge na kubainisha kusudio la Serikali la kuelekeza nguvu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na uzalishaji kwa kuimarisha miundombinu ya usafiri zikiwemo barabara ambayo ni moyo wa ukuzaji uchumi,”amesema Mhandisi Seff

Pia amesema, Rais Dkt. Samia ametekeleza adhima hiyo kwa vitendo kwa kuipa kipaumbele sekta ya barabara kwa kuongeza bajeti ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara vijijini na mijini.

Amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, TARURA wamefanya kazi kubwa vijijini na mijini kwa kufungua barabara ili wananchi waweze kufika hata maeneo ambayo hayakutarajiwa barabara kufika.

“Kwa kweli kwa miaka hii miwili kazi iliyofanyika ni kubwa hata mrejesho tunaupata kutoka kwa wananchi na wadau wa barabara unaonesha kuwa kazi zilizofanyika ni nzuri tofauti na kipindi cha nyuma kabla ya kuanzishwa kwa TARURA,”.

Muonekano wa daraja la Mwasanga lenye urefu wa mita 20 lililopo barabara ya Mwasanga linalounganisha Kata ya Mwakibete, Tembela, Mwasanga na Swaya katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya Mkoani Mbeya.

Hata hivyo ameeleza kuwa TARURA ina jukumu la kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za wilaya wenye jumla ya kilomita 144,429.77 ambazo zimetangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 463 la Juni 25, 2021.

“Ndani ya miaka miwili ya Dkt. Samia, bajeti ya TARURA imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka wastani wa bilioni 275 miaka minne iliyopita na kufikia bilioni 900 kwa mwaka 2021/2022 na trilioni 1.2 kwa mwaka 2022/2023,”amesema Mhandisi Seff.

Mhandisi Seff anasema kuongezeka kwa bajeti, kumewezesha utekelezaji wa miradi mingi ya kimkakati inayogharimu bilioni 142.5 ukiwemo ujenzi wa daraja la Berega lililopo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

Akitolea mfano ujenzi wa daraja la Berega lenye urefu wa mita 140, ulihitaji kiasi cha bilioni 7 ambayo ndiyo ilikuwa bajeti ya Mkoa mzima wa Morogoro kwenye sekta ya barabara za TARURA.

” Hili lisingewezekana, lakini sasa inawezekana baada ya Rais Dkt. Samia kuongeza bajeti ya TARURA na sasa mradi huo upo mbioni kukamilika, huku bajeti ya Mkoa wa Morogoro ikiongezeka kutoka bilioni 7 hadi bilioni 26 kwa mwaka,” amesema Mhandisi Seff.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Ibungu-Kyobo Juu yenye urefu wa kilomita 7.3 kwa kiwango cha changarawe inayounganisha Wilaya ya Rungwe na Wilaya ya Ileje mkoani Mbeya.

Ametaja miradi mingine ya kimkakati ni ujenzi wa kilomita 58.1 za barabara kwa kiwango cha lami katika Mji wa Serikali (Mtumba) Jiji la Dodoma,ujenzi wa kilomita 12.5 za barabara ya Visiga- Zengeni kwa kiwango cha lami katika Mji wa Kibaha mkoani Pwani.

Pia daraja la Mkomazi katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga lenye urefu wa mita 40.6, na ujenzi wa Daraja Msadya lenye mita 60 katika Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kimotorok-Emang’wa yenye urefu wa kilomita nne (4) ikiwa imefunguliwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Naye Dkt. Dugange ambaye Wizara yake ndiyo inasimamia TARURA, aliwapongeza kwa kutekeleza miradi ya barabara kwa kiwango kilichokusudiwa nakusema kuwa serikali ipo pamoja nao kuona adhima ya kuwasaidia wananchi wa vjjijini kwa kuwaongezea mtandao wa barabara ili waweze kusafirisha mazao yao, huku wakiweza kufika maeneo mbalimbali kwa shughuli zao za maendeleo.