March 31, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yaimarisha upatikanaji miundombinu barabara za Wilaya

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline

WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umesema umeimarisha upitikaji wa miundombinu ya barabara za wilaya zenye  urefu wa kilometa 5,057.765 kwa asilimia 55 kitaifa na asilimia 52 Kimkoa huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 60 ifikapo Juni, mwaka huu.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam mapema leo Machi 27,2025 na Meneja  wa TARURA Mkoa wa Dar es salaam,Mhandisi Geofrey Mkinga wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari.

Amesema mafanikio hayo yametokana  na ongezeko kubwa la bajeti ya TARURA kutoka shilingi bilioni 25.431 hadi shilingi bilioni 52.334 sawa na ongezeko la asilimia 205.79 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2024/25.

“Mtandao wa barabara za lami katika kipindi hichi umeongezeka kutoka Kilometa  469.47 hadi Kilometa 636.519, na changarawe kutoka Kilometa 1,327.55 hadi Kilometa 1,686.706 huku
barabara za udongo zimepungua kutoka Kilometa 3,260.75 hadi Kilometa 2,731.54 kwa mapato ya ndani,”amesema Mhandisi Mkinga

Mhandisi Mkinga ameweka wazi kuwa katika ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA wameendelea  kufanya majaribio
kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja ya mawe ‘stone arch bridges’ pamoja na teknolojia nyingine katika kuboresha barabara wanazozisimamia.

Pia amesema wamekuwa wakitumia matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya madaraja, huongeza ufanisi, huokoa muda,
hutunza mazingira kwa gharama nafuu.

“Matumizi ya teknolojia mbadala na malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja imeweza kupunguza gharama zaidi ya 50% ambapo TARURA imeweka kipaumbele cha kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi.”ameongeza Mhandisi Mkinga

Hata hivyo amesema TARURA inaendelea na  matumizi ya malighafi za ujenzi wa barabara zinazopatikana maeneo ya kazi na utafiti wa teknolojia mbadala za ECOROADS,Ecozyme, na GeoPolymer kwenye ujenzi wa barabara kwa lengo la kupata ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kulinda mazingira.

Aidha amesema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 TARURA imeidhinishiwa jumla ya shilingi 68,009,203,651.18 kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya Barabara Kilometa 1,151.987 ambapo lami ni  kilometa 26.04 na madaraja na kalavati 38.

“Maendeleo ya utekelezaji kwa mipango ya mwaka 2024/2025 yanahusisha utekelezaji wa kimaumbile na kifedha ambapo utekelezaji hadi kufikia Disemba 2024 wa kimaumbile ni asilimia 53
Miradi ya Fedha za Mapato ya ndani (Own source -LGA) Mkoa wa Dar es Salaam unatekeleza miradi ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara inayogharamiwa na fedha za mapato ya ndani ya Wakurugenzi (Own source -LGA) ambapo utekelezaji wake umefikia katika hatua mbalimbali”amesema.

Aidha amesema kuwa Barabara  ni nguzo muhimu katika sekta ya usafiri na usafirishaji ambayo kwa
kiwango kikubwa hutumiwa na watu wote kuanzia wenye vipato vya chini, kati na juu.