January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA wajivunia mafanikio makubwa

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKALA wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoani Tabora wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea fedha za utekelezaji miradi ya barabara kutoka sh bil 8 hadi bil 29.1 katika kipindi cha miaka 2.

Akizungumza na gazeti hili jana Meneja wa Wakala huo Mkoani hapa Mhandisi Edward Lemelo alisema miaka 2 ya utawala wa Rais Samia imeleta neema kubwa katika Mkoa huo kwani wameweza kujenga mtandao wa zaidi ya km 790 za barabara za changarawe Vijijini na km 25 za lami Mijini.

Alisema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 walipata kiasi cha sh bil 8 za matengenezo ya barabara, mwaka 2022/2023 wakapata sh bil 29.1 na mwaka huu 2023/2024 wanatarajia kupata zaidi ya kiasi hicho ili kuboresha barabara zote.

Alibainisha kuwa kupitia fedha hizo wamejenga jumla ya madaraja makubwa 6 yanayounganisha vijiji na kata mbalimbali na makalvati makubwa ya boksi yapatayo 206 huku makalvati madogo yakiwa ni zaidi ya 300.

Mhandisi Lemelo alieleza kuwa ongezeko la bajeti ya Ofisi yake limewezesha kufunguliwa kwa barabara nyingi katika maeneo yasiyo na barabara, kuboreshwa barabara za udongo kuwa za changarawe na kujenga barabara nyingi za lami.

‘Juhudi za Mhesh Rais zimewezesha barabara zote zilizokuwa kero kwa wananchi kuanza kupitika hata kipindi hiki cha masika hamna tatizo la kusafirisha mazao yao kama ilivykuwa huko nyuma’, aliongeza.

Jonas Mkebezi (45) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Ng’wande, Kata ya Ng’wande Wilayani Kaliua, alimshukuru Rais Samia kwa kuwapatia TARURA zaidi ya sh mil 900 kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa linalounganisha vijiji vya kata hiyo.

Alisema daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 90 ni mkombozi kwa uchumi wa wakazi wa kata hiyo na kata jirani za Kashishi kwani awali walikuwa wanashindwa kuvuka mto huo punde tu mvua zinaponyesha.

 Awali Meneja wa Wakala huo Wilayani humo Mhandisi Kisanda Robert alisema daraja hilo lina urefu wa mita 30 na upana wa mita 11 na makalvati madogo 3 na limejengwa kwa gharama ya zaidi ya sh mil 900 na sasa limefika asilimia 90.

Alibainisha kuwa eneo hilo lilikuwa hatarishi sana kwa watoto, akinamama  hususani wajawazito na wazee ikiwemo magari kwani wakati wa masika hali ilikuwa mbaya zaidi

Alimshukuru Rais Samia kwa kuwapatia zaidi ya sh bil 3 katika mwaka wa fedha uliopita kwa ajili ya miradi ya barabara ikiwemo ujenzi wa km 1 ya barabara.

Mkazi wa Kijiji cha Nsenda, Wilayani Urambo Masanilo alipongeza serikali ya awamu ya 6 kwa kupeleleka zaidi ya sh mil 294 ili kujenga barabara ya changarawe inayotumiwa na wakazi wa kata 3 za Imalamakoye, Nsenda na Urambo.

Moja ya madaraja yaliyojengwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoani Tabora likiwa katika hatua za mwisho za ujenzi, daraja hilo linaungaisha vijiji vya Ng’wande na Ichemba katika kata ya Ng’wande Wilayani Kaliua Mkoani Tabora, limejengwa kwa gharama ya sh mil 900. 
Picha na Allan Vicent