Na Suleiman AbeidTimesmajira Online, Shinyanga
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Shinyanga umekamilisha kazi ya ujenzi wa barabara inayozunguka Makao Makuu mapya ya Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ikiwa ni moja ya ahadi zilizotolewa na Hayati Rais John Magufuli.
Baadhi ya wananchi wametoa pongezi zao kwa TARURA Mkoa wa Shinyanga ambapo wamesema wameonesha jinsi gani wamemuenzi Hayati John Magufuli kwa kutekeleza ahadi yake aliyowaahidi madiwani na wananchi wa Halmashauri ya Msalala.
Wananchi hao wamesema kukamilika kwa barabara hiyo kutawawezesha wakazi wa Halmashauri ya Msalala kwenda kwa urahisi katika Halmashauri yao pindi wanapohitaji kutatuliwa changamoto zao mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Frola Sagasaga mbali ya kuwapongeza TARURA pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyosimamia vyema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha miradi yote iliyoasisiwa na mtangulizi wake inakamilika.
Sagasaga ambaye pia ni diwani wa kata ya Mwalugulu katika Halmashauri ya Msalala amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Rais Samia Suluhu kwa kazi kubwa zinazofanyika kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Makamu Mwenyekiti huyo amesema Rais Samia pamoja na kuwa ni mwanamke ameonesha ujasiri wa hali ya juu katika kuchapa kazi na amewataka watanzania wote waendelee kumuunga mkono ili aendelee kuwatumikia na kuweza kufikia maendeleo waliyoahidiwa.
Sagasaga amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kunakwenda sambamba na kukamilika kwa jengo la Makao Makuu la Halmashauri ya Msalala hali ambayo itarahisisha utendaji kazi wa watendaji wa Halmashauri yao.
“Niishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyochapa kazi, sasa wakazi wa Msalala tunampongeza Mheshmiwa Rais Samia, maana tunaona kazi anazozifanya,”
“Lakini kwa upande wa barabara tuliyoahidiwa na Hayati Rais John Magufuli, hatuna budi kuwapongeza wenzetu wa TARURA kwa kazi nzuri waliyoifanya, sasa Makao Makuu yetu yataanza kutumika tukiwa na barabara nzuri zenye kiwango cha lami,” anaeleza Sagasaga.
Kwa upande wake Balozi wa Usalama Barabarani mkoani Shinyanga, Seif Nassor ameipongeza TARURA kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ikiwa ni katika kumuenzi Hayati Rais John Magufuli.
Nassor amesema kitendo cha TARURA kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kimeonesha jinsi gani wamemuenzi Hayati Rais John lakini pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi yote iliyoasisiwa na mtangulizi wake.
Hata hivyo Nassor amewaomba wakazi wa Halmashauri ya Msalala kuhakikisha wanazitunza barabara hizo ili ziweze kutumika kwa kipindi kirefu sambamba na kuhakikisha hawaharibu miundombinu na alama za barabara zinazowekwa.
Mhandisi Masola Juma Kaimu Meneja TARURA wilayani Kahama amesema barabara hiyo imekamilika na shughuli zilizobaki ni upakaji wa rangi mara baada ya kumalizika kwa kokoto ambazo zimewekwa juu ya tabaka la lami.
Mhandisi Juma amesema barabara hiyo ina urefu wa mita 850 na unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 509 ambapo hata hivyo kiasi cha shilingi milioni 23 kimesalia kutokana na baadhi ya kazi kupungua katika utekelezaji wake.
Naye Mratibu wa TARURA mkoani Shinyanga, Mhandisi Gilbert Mlekwa ametoa wito kwa wakazi wa Halmashauri ya Msalala kuzitunza barabara hizo ili ziweze kudumu na wajiepushe na tabia ya uharibifu wa makusudi wa miundombinu ambayo imewekwa ikiwemo upitishaji wa mifugo barabarani ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo Mhandisi Mlekwa ametoa wito kwa viongozi ambao ni wawakilishi wa wananchi kujenga tabia ya kuwasiliana na ofisi za TARURA pindi wanapobaini kuwepo kwa changamoto zozote kuhusiana na suala la ubovu wa barabara katika maeneo yao ili waweze kupatiwa ufafanuzi badala ya kulaumu pembeni.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best