December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA kujenga barabara zenye urefu wa Km 100 Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Wilaya ya Tabora anatarajia kutengeneza mtandao wa barabara zenye urefu wa km 100.03 katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala huo Wilaya ya Tabora Manispaa Mhandisi Subira Manyama alipokuwa akitoa taarifa katika kikao cha baraza la madiwani jana.

Alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024 wanatarajia kuzifanyia matengenezo barabara za Vijijini na Mijini zenye urefu wa km 100.03 ikiwemo ujenzi wa makalvati 29, vivuko 20 na mifrereji 3620.

Alifafanua kuwa jumla ya sh bil 2.3 zinatarajiwa kutumika katika mpango wa utekelezaji matengenezo hayo, fedha za bajeti hiyo zitahusisha zile za Mfuko wa Barabara (Road Fund), Jimbo na Tozo ya Mafuta.

Alibainisha kuwa katika bajeti hiyo fedha kutoka Mfuko wa Barabara (Road Fund) kiasi cha sh bil 1.3 zinatarajiwa kutumika kwa matengenezo ya kawaida ya barabara zenye urefu wa km 83.32 kwa gharama ya sh mil 319.3Kazi nyingine ni matengenezo ya barabara korofi zenye urefu wa km 7.54 zitakazogharimu mil 67.8, matengenezo ya muda maalumu ya barabara zenye urefu wa km 9.7 kwa gharama ya sh mil 185.4, ujenzi wa makalvati 29, boksi kalvati 3, mifereji mita 3620 na vivuko kwa gharama ya sh mil 644.5.

Kiasi cha sh mil 86.2 za mfuko huo kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya usimamizi wa matengenezo ya barabara hizo na ujenzi wa makalvati na kiasi cha sh mil 500 za tozo za mafuta kikitarajiwa kutumika kwenye ujenzi wa barabara ya Nyerere (Kidongo Chekundu) yenye urefu wa km 0.8, ya Viseko km 3.22 na Mwilu km 0.5.

Mhandisi Manyama alibainisha kuwa katika bajeti hiyo wanatarajia kujenga barabara ya Warangi yenye urefu wa km 1 kwa kiwango cha lami kwa gharama ya sh mil 500 za Mfuko wa Jimbo.

Alifafanua kuwa Wilaya hiyo ina Mtandao wa barabara wenye jumla ya km 775.6 ambapo km 481.3 ni za mjazio (feeder roads) na km 294.3 ni za mkusanyo (collector roads) na kubainisha kuwa hadi sasa barabara za lami ni km 54.34, za changarawe km 88.6 na za udongo km 633.15.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Tabora Mjini, Mhandisi Subira Manyanya akitoa taarifa ya mipango ya utekelezaji miradi ya barabara katika kata zote wilayani humo juzi katika kikao cha madiwani. Picha na Allan Vicent.