March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARI yapongezwa kwa Ubunifu wa Mbegu Bora,Serikali yasema ni nguzo ya uhakika wa Chakula Nchini

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Edwin Mhede na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo Mhandisi Athumani Kilundumya

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma 

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Edwin Mhede na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo Mhandisi Athumani Kilundumya wametembelea  banda la  Taasisi ya Utafiti wa Mbegu (TARI)  ambapo wamonesha kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Taasisi hiyo katika kubadilisha mfumo wa kilimo kupitia tafiti mbalimbali na ubunifu wa kisayansi unaoleta mbegu Bora zenye tija kwenye uzalishaji wa mazao.

Wakizungumza katika ziara yao Agosti 4,2025 ,wamesema TARI inaendelea kufanya jitihada kubwa katika kuhakikisha inakuja na mbegu Bora Kila wakati na kutegemeana na mabadiliko ya tabianchi.

“TARI ni taasisi ya kimkakati inayopigania maendeleo ya taifa kwa kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa chakula wa kudumu kupitia mbegu bora na zilizofanyiwa utafiti wa kina,” amesema Dkt. Mhede na kuongeza kuwa 

“Kazi ya TARI ni ya kupongezwa, hasa kwa jinsi wanavyoendelea kuboresha mbegu za mazao ili ziwe na tija kwa wakulima.”

Aidha, alitoa rai kwa wataalamu wa TARI kutoridhika na mafanikio ya sasa, bali waendelee kubuni mbegu zenye uwezo wa kustahimili changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kutoa mazao mengi ambazo mkulima anaweza kuzitumia hata miaka  mitano hadi kumi na hivyo kutomlamzimu mkulima kununua mbegu Kila mwaka.

Pamoja na hayo, aliitaka TARI kutafuta suluhisho la changamoto ya wakulima kutorudi kununua mbegu mpya, kwa kuhakikisha gharama za uzalishaji zinashuka ili wakulima wengi waweze kumudu gharama na kuwekeza zaidi katika mbegu bora.

Kwa upande wake Mhandisi Kilundumya alisisitiza umuhimu wa tafiti za kisayansi katika kufanikisha kilimo chenye tija huku ajitoa wito kwa wakulima kutumia matokeo ya tafiti badala ya kuendelea na kilimo cha mazoea.

“Dunia imebadilika, mazingira yamebadilika. Tusiendelee kulima kama zamani. Kilimo cha mazoea hakiwezi kutufikisha kwenye uhakika wa chakula,tafiti za TARI zitumike kwa vitendo,” amesema Dkt. Nindi.

Ameihimiza TARI kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti zake yanafika kwa wakulima hata wa maeneo ya pembezoni mwa nchi, kwa kuwa ndio kundi linalohitaji zaidi mbegu bora na teknolojia ya kisasa.

Akizungumzia msimamo wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt. Nindi amesema serikali imeamua kwa dhati kubadilisha taswira ya kilimo nchini kwa kulielekeza katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika. Alisisitiza kuwa kila kituo cha umwagiliaji nchini kiwe na afisa wa TARI kwa ajili ya kutoa mwongozo wa kitaalamu kwa wakulima ili kuhakikisha uwekezaji wa serikali unazaa matunda.

Awali  akiwapitisha katika Banda la TARI Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt.Thomas Bwana amesema TARI imefanya utafiti kuanzia Afya ya udongo Hadi uongezajibthamani lengo likiwa ni kuongeza tija katika sekta ya Kilimo .

Maonyesho ya Nane Nane mwaka huu yametoa picha halisi ya mwelekeo wa taifa katika sekta ya kilimo, ambapo TARI imeendelea kuwa chombo muhimu kinachowezesha wakulima kupata maarifa, teknolojia na mbegu bora zenye tija – kuelekea kwenye kilimo chenye uhakika wa chakula, ajira, na maendeleo ya uchumi wa viwanda.