November 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,Nigeria kuandaa mkutano afya ya wanawake

Na mwandishi wetu

TANZANIA na Nigeria zimeungana kuandaa Mkutano wa Kwanza wa Afya ya Wanawake Afrika (Women’s Health Africa Summit 2026), utakaofanyika Desemba 1, 2026, jijini Abuja, Nigeria, kwa lengo la kuimarisha uwekezaji katika sekta ya afya, kuongeza rasilimali watu na kuboresha huduma za afya zinazotolewa katika jamii.

Akizungumza hivi karibuni jijini Addis Ababa, Ethiopia, wakati wa uzinduzi wa Mpango Kazi wake kama Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Mama na Mtoto, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema Tanzania inafurahi kushirikiana na Nigeria kuandaa mkutano huo.

Ameeleza kuwa nafasi za Kinara wa Umoja wa Afrika zinazoshikiliwa na nchi hizo mbili zinakamilishana katika kuendeleza ajenda ya afya ya wanawake barani Afrika.

“Mkutano huo utalenga kuimarisha ufuatiliaji wa kisiasa na uwajibikaji katika kutekeleza ahadi za kufikia malengo ya Sifuri Tatu (Three Zeros), sambamba na kuendeleza nguvu kazi ya sekta ya afya na huduma za afya zinazotolewa katika ngazi ya jamii,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake, Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika wa Rasilimali Watu katika Afya na Ushirikiano wa Utoaji wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii, anaunga mkono ajenda ya kuimarisha nguvu kazi ya afya na kuboresha utoaji wa huduma bora kwa jamii.

Mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Health Workforce for Better Women’s Health”, na utawakutanisha viongozi wa Serikali, Mawaziri wa Afya, wataalamu pamoja na washirika wa maendeleo kujadili uwekezaji na mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wanawake na wasichana barani Afrika.

Kupitia mkutano huo, Tanzania na Nigeria zinalenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuharakisha utekelezaji wa hatua zinazolenga kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma bora za afya. Aidha, juhudi za kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa akina mama na watoto zitaendelea kupewa kipaumbele.