November 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mchengerwa: Kila mgonjwa ahamasishwe kujiunga na bima ya afya



Na Joyce Kasiki, Dodoma


WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amezitaka hospitali na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha kila mgonjwa anayefika kupata matibabu anahamasishwa kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kujikinga na gharama za matibabu.


Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), akiiagiza Wizara ya Afya kuhakikisha watumishi wote wa sekta hiyo wanawahamasisha wananchi kujiunga na bima. Pia ameitaka NHIF kuboresha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha usajili na upatikanaji wa vitambulisho vya bima.


Amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na mifumo ya usajili inafanya kazi kwa ufanisi. Amesisitiza kuwa kifurushi cha kaya cha Sh150,000 kwa mwaka kinamwezesha mwananchi kupata bima kwa familia ya watu sita, sawa na Sh25,000 kwa kila mwanachama.


Aidha, amesema Serikali imetenga takribani Sh98 bilioni kugharamia bima za kaya zisizo na uwezo, huku mpango huo ukilenga kupanua upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote. Amesema awamu ya kwanza imehusisha kaya 200,000 na awamu inayofuata inalenga kufikia kaya 625,000.


Kuhusu uimara wa mfuko huo, Mchengerwa amesema mafanikio ya NHIF yanategemea pia ubora wa huduma na ulipaji wa madai ya watoa huduma kwa wakati. Amesema muda wa kushughulikia madai umeboreshwa kutoka siku 120 hadi 45, hatua inayolenga kuimarisha imani ya vituo vya afya na wananchi kwa mfuko huo.


Amesisitiza pia umuhimu wa wananchi kufanya mazoezi, kula lishe bora na kupima afya mara kwa mara, akibainisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya asilimia 37 ya matumizi ya jumla ya NHIF. Ameyataja magonjwa ya moyo, kisukari na saratani kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoweza kupunguzwa kupitia kinga na uchunguzi wa mapema.


Awali, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inaendelea kuhamasisha kinga kupitia kampeni ya Jue Namba Zako, huku akiwataka wananchi kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka. Amesema pia wananchi wanapaswa kufanya mazoezi, kula chakula bora na kuepuka matumizi yasiyofaa ya pombe na sigara.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amesema maadhimisho hayo yamelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu bima ya afya na umuhimu wa kujikinga na magonjwa. Amesema mbio hizo zilishirikisha zaidi ya watu 10,000, huku washiriki wakipata fursa ya kupima shinikizo la damu, sukari, macho na meno.