November 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania mwenyeji mkutano wa Vyuo vya Ulinzi wa Amani Duniani

Na Penina Malundo,TimesMajira

TANZANIA imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa 30 wa Shirikisho la Vyuo vya Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Duniani, utakaowakutanisha viongozi wa kijeshi, polisi, wataalamu wa masuala ya usalama na wadau wa amani kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 4, mwaka huu, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika kukabiliana na changamoto za ulinzi wa amani duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Kunduchi, Kanali Deogratius John Mulishi, amesema Tanzania inajivunia kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria tangu ilipojiunga na shirikisho hilo mwaka 2022.

Amesema shirikisho hilo lilianzishwa mwaka 1995 nchini Canada, likiwa na dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vya mafunzo ya ulinzi wa amani duniani.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo ni ā€œTulinde Amani Pamoja, Tujenge Mustakabali wa Operesheni za Ulinzi wa Amani Kupitia Mafunzo, Ubunifu na Ushirikiano.ā€

Ameeleza kuwa mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kujadili mabadiliko yanayohitajika katika mafunzo na operesheni za ulinzi wa amani, kutokana na kuongezeka kwa changamoto za kiusalama katika maeneo yenye migogoro.

Kwa mujibu wa Mulishi, mkutano huo utawakutanisha viongozi waandamizi kutoka mataifa mbalimbali, Umoja wa Afrika, wakuu wa vyuo vya mafunzo ya ulinzi wa amani duniani, wataalamu wa kijeshi, polisi na wawakilishi wa kikanda pamoja na wadau kutoka taasisi za Serikali na zisizo za Serikali.

Amesema baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na mbinu za kisasa za mafunzo katika kukabiliana na changamoto mpya za kiusalama, matumizi ya teknolojia na ubunifu katika operesheni za ulinzi wa amani na namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya wanajeshi, polisi, magereza, uhamiaji na raia.

Mada nyingine ni nafasi ya wanawake katika ulinzi wa amani na usalama, eneo ambalo linahitaji kuendelea kupewa kipaumbele katika juhudi za kimataifa za kudumisha amani.

Amesema mkutano huo utahitimishwa kwa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani Kunduchi kukabidhiwa urais wa shirikisho hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja, kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Ameeleza kuwa jukumu hilo litatoa fursa kwa Tanzania kuendelea kuchangia katika kuimarisha mafunzo, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya ulinzi wa amani.

Katika mkutano huo, pia kutafanyika maadhimisho ya Siku ya Polisi wa Umoja wa Mataifa (UN Police Day), yanayotarajiwa kufanyika Novemba 29, mwaka huu.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Naibu Kamishna David Misime, amesema Tanzania imepata fursa kubwa ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa kwa mara ya kwanza tangu ijiunge na shirikisho hilo mwaka 2022.

Amesema ushiriki wa Tanzania katika shughuli hizo ni nafasi muhimu ya kuonesha mchango wa nchi katika juhudi za kimataifa za kulinda na kudumisha amani.

Maadhimisho na mkutano huo unatarajiwa kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za ulinzi na usalama, kubadilishana maarifa na uzoefu pamoja na kuimarisha uwezo wa wataalamu wanaoshiriki katika operesheni za kulinda amani duniani.