Na Mwandishi wetu,Timesmajira
USHIRIKIANO wa kiuchumi kati ya Tanzania na India unaendelea kushamiri, huku India ikijikita kama moja ya wawekezaji wakubwa nchini Tanzania.
Takwimu za hivi karibuni kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) zinaonyesha kuwa hadi sasa miradi 793 kutoka India imesajiliwa rasmi, ikiwa na thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 2.5.
Miradi hiyo imeelekezwa zaidi katika sekta muhimu kama viwanda, usafirishaji, na miundombinu ya kibiashara, jambo linaloashiria imani kubwa ya wawekezaji kutoka India katika mazingira ya biashara nchini Tanzania.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya India, Mkurugenzi Mtendaji wa TISEZA, Gilead Teri, amehimiza wawekezaji kutoka India kuendelea kushirikiana na kampuni za Kitanzania kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani, Afrika, na hata masoko ya kimataifa kama Ulaya na Marekani ambako bidhaa kutoka Tanzania zinaingia bila ushuru wala vikwazo.

“Kituo cha Uwekezaji kimejipanga kutoa msaada na taarifa zote muhimu kwa wawekezaji. Tunawakaribisha wawekezaji kutembelea banda letu la TISEZA katika maonesho haya, ili wajifunze kwa undani fursa zilizopo nchini Tanzania,” amesema Teri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade,Latifa Khamis, amesisitiza dhamira ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na India, hasa na wadau kutoka Jimbo la Haryana jimbo ambalo limeonyesha nia ya dhati ya kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya teknolojia, kilimo na viwanda vidogo.
“Maonesho ya mwaka huu yamevutia zaidi ya washiriki 4,000, jambo ambalo linadhihirisha Tanzania ni kitovu cha kibiashara cha kuaminika Afrika Mashariki. TanTrade itaendelea kusaidia biashara ndogo na za kati kupitia ushauri wa chapa, matumizi ya teknolojia rahisi, na urahisishaji wa usafirishaji wa bidhaa,” amesema Latifa.

Naye Mkurugenzi wa FCD Haryana, Amna Tasneem, ametoa wito kwa wafanyabiashara wa India na Tanzania kuendelea kushirikiana kwa karibu, ili kufanikisha makubaliano yaliyokwisha anzishwa na kuhakikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi kwa pande zote mbili.
Katika maonesho hayo, kampuni mbalimbali kutoka Jimbo la Haryana India zimeonesha nia ya kushirikiana na sekta binafsi ya Tanzania. Mfano wa hilo ni Shirika la Uhifadhi wa Mazao la Jimbo la Haryana (HSWC), ambalo limeonyesha mafanikio katika sekta ya ununuzi na uhifadhi wa mazao nchini India, kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kuhifadhi mazao yenye upotevu mdogo wa asilimia 0.2 pekee.

Amesema kampuni yao, ambayo ina mapato ya zaidi ya dola milioni 588 kwa mwaka, ina nia ya kusaidia Tanzania katika ujenzi wa maghala ya kisasa, kutoa mafunzo kwa wakulima na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Katika upande wa teknolojia, Shirika la Maendeleo ya Elektroniki la Haryana (HATRON) pia lilishiriki maonesho hayo na kutangaza kusaini makubaliano ya ushirikiano na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kuanzisha vituo vya mafunzo ya TEHAMA nchini Tanzania.
Mwakilishi wa HATRON ameeleza kuwa, shirika hilo lina mtandao mpana wa vituo vya mafunzo ya IT nchini India, na lina nia ya kuleta uzoefu huo Tanzania ili kuwajengea vijana uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri kupitia teknolojia ya kisasa.
“Tuko tayari kushirikiana na serikali, vyuo na sekta binafsi nchini Tanzania ili kuharakisha maendeleo ya kidijitali na kuijengea nchi msingi imara wa uchumi wa kisasa unaojumuisha wote,”

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi