December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yatoa msaada nchini Malawi kukabiliana na kimbunga Tropiki Freddy

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua ujirani mwema ,ushirikiano na udugu na nchi ya Malawi imetoa Misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa nchi hiyo kukabilina na janga la dhoruba ya kimbunga kiitwacho “Tropiki Freddy” kilichoikumba hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Machi 18,2023 Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania,Luteni Kanali Gaudentius Ilonda amesema kuwa misaada huo ni kutokana na kimbunga hicho kilichotokea Machi 13,2023 katika nchi hiyo kilichoambatana na mvua kubwa na upepo mkali kiliikumba nchi hiyo kiasi cha kutisha cha maji yaliyotiririka katika vitongoji na kusomba nyumba na kuleta maafa.

“Kimbunga hicho kimesababisha maafa makubwa kaisi cha kutangazwa kuwa janga nchini humo baada ya kusababisha vifo ,kuharibu miundombinu,nyumba,mazao na athari nyingine kadhaa wa kadhaa,”ameeleza Luteni Kanali Ilonda.

Ameeleza kuwa kutokana na hilo Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania limepewa jukumu kushiriki bega kwa bega kupeleka msaada huo.

Luteni Kanali Ilonda amesema kuwa kufuatia jukumu hilo Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda ametoa maelekezo yanayoratibiwa na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ  Luteni Jenerali Salum Haji Othman,magari ya JWTZ zaidi ya 37 yataondoka Dodoma muda wowote kupeleka misaada nchini Malawi.

Ameeleza kuwa baadhi ya magari hayo yanayopelekwa Malawi ni pamoja na Gari la wagonjwa(Ambulance),karakana ya magari inayotembea(mobile Workshop) na Malori makubwa yenye uzito wa tani 30 idadi 20 na malori yenye uzito wa tani zaidi ya 18  yakiwa 10.

“Magari hayo yatasafirisha msaada wa Mahema,Mablanket,Chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu yanayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”amesema.

Vilevile amesema JWTZ linapeleka Helikopta mbili ikiwa ni sehemu ya msaada unaotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusaidia katika janga hilo nchini humo.

“Hivi punde helikopta hizo zimeruka kutokea Dar es Salaam  kuelekea Malawi tayari kuanza utekelezaji wa majukumu hayo,”amesema.

Hata amesema kuwa zitapelekwa Tani 1000 za Unga ambazo zitakuwa zinaenda kwa Tani 90 kila siku kutokea Mkoa wa Dodoma huku Tani 60 zitakuwa zinaenda kupitia Mkoa wa Iringa.

Pamoja na hayo Luteni Kanali Ilonda amewataka wananchi kuwa watulivu bila taharuki wanapoyaona magari ya Jeshi yanapita katika maeneo yao kuelekea mipaka ya Malawi kwani yanapita kwa amani kwajili ya kupeleka misaada nchini Malawi.