October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yasaini mikataba ya msaada na serikali ya Uswisi

Na Beatrice Sanga, MAELEZO

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetia saini mikataba miwili ya msaada kati yake na Serikali ya Uswisi ambayo imetoa msaada wa Faranga za Uswisi milioni 15.75, sawa na Sh. bilioni 39.59 ambao unalenga kusaidia jitihada za Tanzania kufikia malengo ya kusaidia Sekta ya Afya kwa wote na kupunguza malaria nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amesema kuwa, Tanzania imesaini mikataba miwili ambapo mkataba wa kwanza ni msaada wa Faranga za Uswisi milioni 9.75, sawa na Shilingi bilioni 24.51 ambazo zimetolewa ili kugharamia mradi wa uboreshaji wa afya na uimarishaji wa mfumo wa afya (HPSS) na mkataba wa pili ni wa msaada wa Faranga za Uswisi milioni 6, sawa na bilioni 15.08 zilizotolewa kwa ajili ya kugharamia programu ya kutokomeza malaria nchini Tanzania ambapo kwa mwezi Oktoba 2020 pekee Tanzania imeweza kusaini mikataba ya jumla ya pesa za kitanzania bilioni 83.69.

“Wakati tunasaini mikataba hii, pia ikumbukwe kuwa Oktoba 6, 2020 Serikali zetu mbili zilisaini mikataba miwili ya misaada yenye thamani ya Faranga za Uswisi milioni 17.80, sawa na bilioni 44.10 kwa hiyo, kwa mwezi Oktoba 2020 pekee tumesaini mikataba ya misaada ya jumla ya Faranga za Uswisi milioni 33.55 sawa na bilioni 83.69,” amesema Doto James.

Kiongozi huyo amesema kuwa, fedha hizo zitaenda kutumika kuimarisha mifumo ya Afya hapa Tanzania kwa kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (iCHF) wenye malengo mahususi ya kuimarisha Sekta ya Afya.

Aidha ameongeza kuwa, Faranga za Uswisi milioni 6 sawa na bilioni 15.08 zilizotolewa kwa ajili ya Programu ya Kutokomeza Malaria Tanzania zitaenda kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na maralia pamoja na kutekeleza mikakati ya kisekta ya kuzuia maambukizi mapya ya Malaria.

“Tutaweka mpango wa kudhibiti Malaria Tanzania kwa lengo la kuondoa kabisa vifo vinavyotokana na malaria na kupanua wigo wa maeneo yasiyokuwa na malaria (Malaria Free Zones) hadi nusu ya nchi nzima ifikapo mwaka 2030 kupitia utambuzi wa maeneo hatarishi kwa Malaria nchini” amesema Doto James.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Didier Chassot, amesema Serikali ya Tanzania na Uswisi wana uhusiano mzuri kwa muda mrefu sasa na wametoa msaada huo ili kuisaidia Tanzania kujiimarisha katika Sekta ya Afya ikiwemo kupambana na kutokomeza ugonjwa wa malaria nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya Dkt. Leornard Sudi amesema, Wizara ya Afya itaenda kutumia fedha hizo vizuri kwa kuimarisha mifumo ya afya na takwimu kwa ujumla ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na malaria ambapo mpaka sasa vimepungua kwa zaidi ya asilimia 67.

“Kwa msaada huu ambao tumeupata wa bilioni 39.59 tutaendeleza kuimarisha mifumo ya takwimu, sisi tunaelewa kwamba takwimu ndio zitaonesha namna gani tunavyozidi kuendelea” amesema Dkt. Sudi.