December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusiana na mafanikio ya kituo hicho ndani ya miaka mitano.

Tanzania yarekodi mafanikio ya kihistoria kupitia Kituo cha Uwekezaji

Na Irene Clemence, TimesMajira Online, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe amesema, tangu kuingia madarakani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kumekuwa na mafanikio makubwa nchini ambayo ni ya kujivunia kwenye Sekta ya Uwekezaji ikiongozwa na viwanda.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya miaka mitano ya kituo hicho.

Amesema,miradi 1,312 imesajiliwa na TIC katika kipindi cha Januari 2016 hadi Juni 2020 huku sekta ya uzalishaji na usindikaji wa viwanda ikiongoza kwa asilimia 54 na imetoa ajira kwa Watanzania 67,992.

Pia amesema, miradi hiyo ina mtaji wa thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 20 (zaidi ya shilingi Trilioni 46 za Kitanzania) na imetoa ajira kwa Watanzania 178,101.

Mwambe amesema, pia kituo kimeboresha na kuongeza huduma za mahala pamoja, ofisi za kanda za kituo cha uwekezaji,kufanikisha uanzishwaji wa kamati ya taifa ya uwezeshaji,mifumo ya kuchakata na kutoa vibali.

Amesema,uwekezaji huo wa viwanda unakwenda sambamba na malengo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo imejipambanua katika kujenga uchumi wa viwanda ili kufikia uchumi wa kati.

Amesema, katika kipindi cha miaka mitano, TIC imeongeza ofisi kutoka tatu mwaka 2015 hadi saba mwaka 2020 katika kanda.

Amesema, pia kituo kimewezesha kuanzishwa kwa Kamati ya Taifa ya Uzalishaji Uwekwezaji (NIFC) inayoundwa na wakuu wa taasisi zinazotoa vibali na leseni mbalimbali kwa wawekezaji.

“Kamati hiyo ina jukumu la kusaidia kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji kwenye maeneo yanayosimamiwa na taasisi za Serikali,”amesema.

Amesema,TIC imefanikiwa kukamilisha mifumo ya kuchakata na kutoa vibali kwa njia ya kielekroniki ikiwemo utoaji wa cheti cha vivutio, usajili wa kampuni, kibali cha kazi na ukaazi.

Pia taasisi zote zilizopo katika kitengo cha huduma za mahali pamoja zinapokea malipo ya huduma zao kwa mfumo wa GePG jambo linalorahisisha malipo.

“Taratibu na kanuni za kuanzisha biashara na uwekezaji zimeainishwa waziwazi katika tovuti za kila taasisi na pia katika tovuti ya TIC kwa kutumia mfumo wa eRegulations,”amesema Mwambe.

Ameongeza kuwa, katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani TIC kwa kushirikiana na wadau iliweza kufanya makongamano ya kuhamasisha uwekwzaji katika mikoa ya Morogoro, Tanga, Ruvuma, Songwe, Lindi, Dodoma, Tabora, Pwani, Iringa, Mbeya na Mtwara kwa ajili ya kuibua fursa mbalimbali za uwekezaji katika mikoa hiyo.

“Katika kuhamasisha uwekezaji kutoka nje TIC kwa kushirikiana na balozi kutoka nje ya nchi, imefanikiwa kufanya uhamasishaji wa kuvutia uwekezaji katika nchi ya Vietnam, India, Korea Kusini,Uswisi, Uingereza, Hispania na Italia. Nchi zigine ni Uholanzi, Misri, China,Canada, Morocco, Nigeria, Kenya pamoja na Afrika Kusini,”amesema.

Amesema,kipindi hicho kituo kimeweza kupokea wawekezaji waliokuja kutafuta fursa mbalimbali za uwekezaji kutoka nchi za Finland, India, Misri, Indonesia, Singapore,Italia, Iran, China, Vietnam, Marekani, Ujerumani, Poland, Korea, Czech, Uingereza, Oman, Uturuki, Kenya, Malaysia, Hongkong, Ethiopia, Uganda, Pakistan, Urusi, Ukraine, Belarus, Sudan, Japan, Ghana, Canada, Syria, Tunisia na Afrika Kusini.

Mwambe ameongeza kuwa, kituo kimeendelea kufanya tafiti kuhusu mwenendo wa mitaji ya uwekezaji kutoka nje na kufanya tafiti za kisekta ili kubaini hali halisi ya ukuaji,fursa na changamoto za kisekta na kutoa mapendekezo ya maboresho katika sekta husika.