January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yapokea umeme KWh Mil. 21 kutoka Maporomoko ya Rusumo

Na Penina Malundo,Dar es Salaam

MRADI wa umeme megawati 80 uliopo kwenye maporomoko ya Mto Rusumo mpakani mwa Tanzania,Rwanda na Burundi, umeanza kuipatia Tanzania KWh Milioni 21.

Novemba 3,2023 mradi huo ulifikisha jumla ya KWh Milioni 66 za umeme kwa nchi tatu za Rwanda ,Burundi na Tanzania.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Meneja wa Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo, Mhandisi Aloyce Oduor, wakati akizungumza waandishi wa habari kutoka nchi saba zilizotembelea mradi huo kati ya Januari 31 hadi Februari 1,2024.

Amesema mbali na Tanzania kupokea KWh hizo, pia nchi ya Rwanda nayo ilipokea Kwh milioni 21, huku Burundi ikipata mgao wa juu zaidi wa KWh milioni 22.

Amesema Tanzania ina mahitaji ya juu ya nishati ya umeme zaidi ya 1,000 MW,lakini kwa kiasi hicho kilichopata kinaweza kuwa kidogo kikasaidia kwa kiasi kikubwa.

“Kiasi hicho cha umeme kitaweza kuimarisha upande wa Kaskazini- Magharibi mwa Tanzania na kufanya ubora wa umeme katika ukanda huo kuwa bora na wa kutegemewa zaidi,”amesema Mhandisi Oduor.

Amesema mradi huo unatekelezwa na Mpango Tanzu wa Nile Equatorial Lakes, (NELSAP-CU) kwa niaba ya Kampuni ya Rusumo Power(RPCL) ambayo iliundwa na nchi tatu za Burundi, Rwanda na Tanzania kwa ajili ya kuendesha mradi huo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kanda kutoka Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program Coordination Unit,(NELSAP-CU),Mhandisi Isaac, Alukwe amesema hadi kufikia Januari 31,2024, mradi huo umefikia asilimia 99.9, ambapo mradi una mitambo mitatu, kila moja ikiwa na uwezo wa kuzalisha umeme kiasi cha MW 27.

“Baada ya kukamilisha vipimo vyote vinavyohitajika, NELSAP imesaini vyeti vya kukamilika na kukabidhi mitambo miwili kati ya mitatu kwa Kampuni ya RPCL,’amesema na kuongeza;

“Mitambo yote mitatu (Turbine) imejaribiwa na inaonekana kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa asilimia 105,”amesema.

Amesema majaribio ya mwisho kwenye mitambo hiyo ya turbine yanaendelea na mara tu wahandisi watakapokamilisha majaribio hayo, NELSAP na RPCL watatia saini ya cheti cha mwisho kabla ya kuzinduliwa rasmi na wakuu wa nchi hizo tatu Aprili 2024.

Mategemeo ya umeme kutoka katika maporomoko hayo ambayo yataweza kuingizwa katika gridi za taifa za nchi hizo na kuleta unafuu kwa nchi zote hasa zile zinazotumia genereta yanayotumia mafuta.

Bei ya gharama ya umeme itaweza kuwa chini kwa watumiaji wa mwisho.

Aidha mradi utasaidia kukuza uchumi wa nchi hizo tatu na kuchochea ukuaji wa viwanda, kuboresha utoaji wa huduma kama vile maji, afya, na elimu, kusaidia shughuli za kiuchumi kama vile viwanda na kuboresha maisha ya watu kupitia upatikanaji wa umeme kwa gharama nafuu.