January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yajizatiti kufikia 50/50 katika uongozi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN-Women) Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka kuhusu kuendeleza ajenda zinazowahusu wanawake.

Katika mazungumzo hayo ya Mei 28, 2021, Dkt. Phumzile amemshukuru Rais Samia kwa namna anavyounga mkono juhudi za kupigania masuala ya wanawake na ameahidi kuwa UN-Women itamuunga mkono katika juhudi hizo.

Amemualika kushiriki katika mkutano utakaojadilia masuala ya kijinsia uliopangwa kufanyika Juni 30, 2021 huko Paris, Ufaransa ambao madhumuni yake ni kuchagiza usawa wa kijinsia kama yalivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 baada ya kuonekana baadhi ya maazimio yanasuasua.

Kuelekea mkutano huo nchi zitakazoshiriki zimegawanywa katika maeneo sita ya kufanyia kazi na Rais Samia amekubali kuwa kiongozi katika eneo la haki za kiuchumi.

Aidha, Dkt. Phumzile ameeleza kufurahishwa kwake na sekta binafsi ya Tanzania ambayo imekubali kushirikiana na Serikali kusaidia juhudi za kuleta usawa wa kijinsia katika masuala ya kiuchumi kwa wanawake.

Kwa upande wake,Rais Samia ameipongeza UN-Women kwa juhudi kubwa za kupigania masuala ya wanawake ikiwemo maazimio ya Beijing na ameeleza kuwa Tanzania ipo tayari kuungana na UN-Women katika kuongeza msukumo wa utekelezaji wake.

Amebainisha kuwa japo Tanzania bado haijafikia kiwango cha usawa wa kijinsia cha 50/50 katika uongozi, katika kipindi chake atahakikisha anaongeza jitihada za kufikia usawa huo.

Rais Samia ameishukuru UN-Women kwa utayari wake wa kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19).