December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yajivunia ushirikiano imara na umoja wa Ulaya

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar

Serikali imesema inajivunia uhusiano na ushirikiano imara baina yake na Umoja wa Ulaya (EU) ambapo mpaka sasa zaidi ya kampuni 100 za nchi wanachama wa umoja huo zimewekeza Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alitoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Ulaya iliyohudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Balozi Mulamula alisema kuwa EU umesimama na Tanzania wakati wote na umeendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo.

“Serikali ya Tanzania inaushukuru Umoja wa Ulaya kwa uhusiano huu imara ambao umedumu kwa muda mrefu pamoja na msaada ambao umekuwa ukitolewa kwa miaka mingi.

“Umoja wa Ulaya ni wadau wetu wakubwa wa maendeleo, wanagusa kila sekta, mwezi Februari, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, alitembelea Umoja wa Ulaya Brussels na alikutana na wafanyabishara, tulipata ahadi ya kampuni nyingi zilionyesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania.” alisema Balozi Mulamula

Alisema kuwa hadi sasa wana kampuni zaidi ya 100 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya ambazo zimewekeza Tanzania.
Balozi Mulamula aliongeza kuwa wawekezaji wengi kutoka nchi za Jumuiya ya Umoja wa Ulaya zimeonyesha nia ya kuwekeza hapa nchini na wameridhishwa na mazingira ya biashara yaliyopo.
Nae Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Manfredo Fanti alisema wataendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha maendeleo katika sekta ya biashara na uwekezaji, utamaduni, uongozi kwa wanawake katika masuala ya siasa, elimu na afya kwa maslahi ya mataifa yote mawili.

“Tunaiona Tanzania ikiendelea kubadilika, mara kwa mara tunakutana na vijana na watu wenye vipaji wakitekeleza malengo na miradi yao, hivyo muundo wa kijamii unabadilika.

“Hii ni dhahiri kabisa kuwa Watanzania ndiyo waamuzi wa mustakabali wa jamii yao, Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono jitihada za mabadiliko katika jamii ya Watanzania kwa kuwa huo ndiyo ushirikiano na urafiki,”Balozi Fanti alisema.

Balozi Fanti pia aliipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuongeza mwanachama mpya ambaye ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa jambo hilo ni jema linaongeza nguvu ya ushirikiano katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alisema Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika kukuza na kuendeleza uchumi wa mataifa hayo kwa maslahi ya pande zote mbili.

Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui ambaye alimuwakilisha Rais wa Umoja wa Ulaya katika maadhimisho hayo, alisema Jumuiya ya Ulaya imelenga pamoja na mambo mengine, kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania, kuongeza mshikamano, amani na uhuru pamoja kukuza demokrasia.

Kwa Upande wake, Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dkt. Peter Mathuki alisema Umoja wa Ulaya umekuwa mshirika mkuu wa nchi wanachama wa EAC kutokana na uhusiano mzuri na wa kishistoria uliojengewa misingi imara tangu 1975.

“EAC tunaishukuru Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa misaada endelevu kwa miradi na programu za Jumuiya yetu ambazo zimekuwa zikiwanufaisha wananchi kwa miaka mingi,” Dk. Mathuki alisema.
Pia alizipongeza nchi wanachama wa Jumuiya Umoja wa Ulaya kwa umoja ambao umekuwa mfano wa kuigwa wa kiuchumi duniani kote