Na Martha Fatael, TimesMajira Online
Tanzania inaendelea na maandalizi ya kina ya mpango wake wa Kitaifa wa Kuchangia Kupunguza Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (NDC), kufuatia maazimio ya mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), wakati nchi 80 duniani tayari zimewasilisha mipango yao mapema.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Hassan Mjemah amesema Tanzania imeamua kuchukua muda wa kutosha ili kuhakikisha mpango huo unazingatia vipaumbele vya kitaifa na maslahi ya wananchi.
“Tanzania inaandaa NDC itakayokuwa jumuishi, inayotekelezeka na inayoendana na hali halisi ya uchumi, jamii na mazingira yetu. Lengo letu ni kupata mpango wenye tija kwa maendeleo ya taifa na ustahimilivu wa wananchi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Dkt. Mjemah.
Ameongeza kuwa maandalizi hayo yanaenda sambamba na kuoanisha ajenda ya tabianchi na mipango ya maendeleo ya taifa, ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi wa kijani, kulinda rasilimali asili na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na uwajibikaji.
Kwa upande mwingine, jumla ya nchi 80 kati ya wanachama 197 wa UNFCCC zimechangamkia fursa ya kuwasilisha NDC zao mapema, hatua inayodhihirisha dhamira ya haraka katika utekelezaji wa maazimio ya COP30.
Akizungumzia mwenendo huo wa kimataifa, Mtaalamu wa Masuala ya Tabianchi, Kenya, Grace Mwangi amesema uwasilishaji wa mapema unazipa nchi faida ya kimkakati katika kupata rasilimali.
“Nchi zinazowasilisha NDC mapema hujiweka katika nafasi nzuri ya kunufaika na ufadhili wa tabianchi, teknolojia rafiki kwa mazingira na ushirikiano wa kimataifa,”amesema Mwangi.
Hatua ya nchi hizo 80 inaonekana kuwa funzo muhimu kwa nchi zinazoendelea, hususani barani Afrika, kuhusu umuhimu wa maandalizi ya mapema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Programu za Tabianchi, Ethiopia,Samuel Bekele, maandalizi ya NDC yanaweza kuwa chombo cha kuharakisha maendeleo endelevu.
“NDC si nyaraka za mazingira pekee, bali ni nyenzo za kuvutia uwekezaji katika nishati safi, kilimo kinachostahimili tabianchi na miundombinu endelevu,”amesema Bekele.
Kwa Tanzania, mchakato wa maandalizi ya NDC unaelekezwa pia katika kuzingatia masuala ya kijamii ikiwemo haki za binadamu, usawa wa kijinsia, ushiriki wa vijana na ulinzi wa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Akifafanua hilo, Mhadhiri wa Sera za Mazingira, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam (UDSM), Profesa Asha Mwakalila amesema mpango huo ukitekelezwa vyema utaleta mabadiliko chanya kwa wananchi.
“NDC bora itasaidia Tanzania kulinda mazingira, kukuza uchumi wa kijani na kujenga ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Profesa Mwakalila.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani