Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
TANZANIA imeishauri Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), kutumia kikamilifu fursa ya kiti cha uwakilishi wa Umoja wa Afrika katika Kundi la nchi Ishirini Tajiri Duniani (G20), kutetea maslahi ya nchi za Afrika ili ziweke kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya nchi hizo ikiwemo madeni makubwa, maradhi, kilimo kisicho na tija, mabadiliko ya tabia nchi, uharibifu wa mazingira pamoja na matumizi hafifu ya teknolojia.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za nchi za Afrika, uliofanyika Kando ya Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyoanza rasmi jana Jijini Washington D.C nchini Marekani.
Dkt. Mwamba alisema kuwa Tanzania inaona kuwa nafasi hiyo ni muhimu kwa kuwa itachangia kutimiza malengo yake pamoja na ya nchi za Afrika kutekeleza na kusimamia vipaumbele vyake vya kuimarisha uchumi na huduma za kijamii kwa wananchi.
Aliyataja maeneo manne ya kimkakati yanayotakiwa kupewa msukumo mkubwa katika G20, ikiwemo maendeleo endelevu ya kiuchumi, uhimilivu wa madeni na Sekta ya fedha, Ulinzi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, Maendeleo ya kilimo, Usalama wa chakula, afya, biashara na uwekezaji.
Dkt. Mwamba alifafanua kuwa nchi za Afrika zinahitaji kusaidiwa kuwa na miundombinu ya kijani, nishati jadidifu, matumizi ya teknolojia za kidigiti vitakavyochochea ukuaji wa uchumi jumuishi utakaozinufaisha nchi zote za Bara la Afrika.
Aidha, alisema kuwa nchi Tajiri Duniani (G20), ziangalie uwezekano wa kuzifutia ama kuzipunguzia madeni nchi za Afrika ambazo nyingi, uchumi wake umeyumba kutokana na majanga mbalimbali ya kidunia ikiwemo Uviko 19, mizozo ya vita pamoja na mabadiliko ya Tabianchi ili kiasi cha fedha kinachopatikana ama kukusanywa ndani ya nchi hizo kiweze kitumika kuendeleza nchi zao badala ya kulipa madeni.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja