January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania wapania makubwa Kabaddi Afrika

Na Hamisi Miraji, TimesMajira Online

KIKOSI cha nyota 28 wa timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa Kabaddi kipo kambini kikiendelea na mazoezi ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano ya mchezo wa Kabaddi ya Afrika ambayo yataanza kutimua vumbi rasmi kuanzia Juni 29 hadi Julai 5, 2021 katika viwanja vya Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Awali mashindano hayo yalipangwa kufanyika Desemba mwaka jana lakini yakasogezwa mbele hadi Februari, kisha Aprili ambapo pia yalibadilishwa tena hadi Juni baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Shirikisho la Kabaddi Afrika kilichofanyika Machi, 2021 kupitia Zoom ambacho walikubaliana kubadili tarehe kutokana na masuala ya janga la Corona kuendelea kuzikabili baadhi ya wanachama wake ambao watashiriki katika mashindano hayo.

Katika mashindano hayo ya Afrika nchi zote zitawakilishwa na timu za wanawake na wanaume na hadi sasa nchi zilizothibitisha kushiriki ni Kenya, Cameroon, Misri, Zimbambwe, Mauritania pamoja na Algeria ambao bado hawajataja idadi ya timu zitakazokuj huku Nigeria na Tunisia zenyewe zitatoa wawakilishi wao kuja kushuhudia mashindano hayo kwakuwa timu zao hazitashiriki.

Katika mashindano hayo Kenya itaongeza timu ya Circle Kabaddi ambayo itachuana na timu ya Magereza kutokana hapa nchini ambapo mchezo huo hautakuwa sehemu ya mashindano bali utachezwa katika mashindano kama sehemu ya onyesho.

Akizungumza na TimesMajira, Katibu Mkuu wa Chama cha Mchezo wa Kabaddi Tanzania (TKSA) Kahema Fimbo amesema, hadi sasa maandalizi ya kikosi chao kilichoweka kambi katika shule ya Sekondari Nguva iliyopo Kigamboni huku wakijinasibu kuibuka na ushindi ili kuipeperusha vema bendera ya Taifa.

“Tunalishukuru Shirikisho la Kabaddi Afrika kwa kuipa nafasi Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano haya jambo ambalo litachangia kukuza mchezo huu hapa nchini pamoja na kupata fursa ya kuutangaza utalii wetu Kimataifa kwani ni mchezo mkubwa unaotambulika zaidi katika bara la Asia,” amesema Fimbo.

Fimbo amesema, hadi walipofikia wamekuwa wakipata msaada mkubwa kutoka kwa washirika wake ambao ni Ofisi ya Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Baraza la Michezo la Tanzania, Kamishna Mkuu wa India nchini Tanzania na Patroni wao ambaye amewapa msaada mkubwa hata katika kuiweka kambini timu ya Taifa.

Kutokana na msaada huo mkubwa wanaoupata kuhakikisha wanajiandaa vyema kuelekea kwenye mashindano pamoja na kushiriki kikamilifu ili waweze kunyakuwa ubingwa watahakikisha hawafanyi makosa.

Lakini pia amewataka wadau wa michezo hapa nchini kujitokeza kwa wingi kushuhudia mashindano hayo ili kuwapa nguvu vijana wa Tanzania, kuwachangia kwa hali na mali ili waweze kufanikisha mashindano ikiwa wao kama waandaaji, hivyo kama kuna mtu anahitaji kutoa mchango wake afike kambini Kigamboni ambapo timu yao ya Taifa imepiga kambi.