February 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, Uholanzi zazindua mpango wa utambuzi na usimamizi wa magonjwa ya kuku

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dar

TaANZANIA kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ubalozi wa Uholanzi nchini kwa pamoja wamezindua mradi wa utambuzi na usimamizi wa magonjwa ya kuku ambao unalenga kubadilishana maarifa na teknolojia ili kudhibiti changamoto zinazohusiana na magonjwa ya kuku hapa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo juzi jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe alisema kuwa Wizara kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mifugo ya Tanzania (TVLA) ina lengo la kushughulikia
changamoto na upungufu wa maabara na utaalamu wa kupima magonjwa yanayosumbua kuku kama ndege na mifugo mengine kwa nia ya kuboresha afya ya wanyama.

“Huu ni hatua muhimu kwa serikali na Ubalozi wa Uholanzi hapa Dar es Salaam kwa kushirikiana katika kuboresha na kudhibiti utambuzi wa magonjwa ya kuku ili kuhakikisha usalama wa chakula nchini,” alisema na kuongeza;

“Mradi huu hauta harakisha tu vita dhidi ya magonjwa mbalimbali katika sekta ya kuku, bali pia utafungua njia kwa maboresho ya maabara na matumizi ya teknolojia mpya kwa ajili ya afya endelevu ya wanyama nchini nzima,”

Profesa Shemdoe alisisitiza kwamba sekta ya kuku ni muhimu kwani ni nguzo muhimu kwa changamoto za ajira kwa vijana wengi wa kiume na kike lakini pia kwa fursa za kiuchumi zilizopo kwenye sekta husika.

Alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan iliruhusu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuzindua kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wa chanjo za mifugo kwa bajeti inayokadiriwa kuwa sh. 28.1 bilioni ili kuongeza biashara za mifugo na bidhaa zake, ndani na nje ya nchi.

Profesa Shemdoe alieleza zaidi kwamba maendeleo haya ni sehemu ya mipango endelevu baada ya uzinduzi rasmi wa Mikakati ya Kitaifa ya Chanjo za Mifugo, mpango wa miaka mitano (2024-2029), utakaotekelezwa kwa awamu mbalimbali.

“Si tu haya bali pia nataka kuwahamasisha Watanzania hasa vijana wa kiume na kike kujiunga na mpango wa Kujenga Kesho Bora (BBT) unaolenga kuwainua vijana kuingia katika biashara ya kilimo ufugaji kama vile kuku.” alisisitiza.

Kwa upande wake, Balozi wa Uholanzi hapa nchini , Wiebe de Boer alisema wanapoanzisha ushirikiano katika utambuzi na usimamizi wa magonjwa ya kuku, mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Ujasiriamali la Uholanzi na kutekelezwa na TVL na Royal
GD ya Uholanzi.

“Nashukuru Wizara na TVLA kwa juhudi kubwa za kusaidia maendeleo ya sekta ya kuku, hata hivyo bado kuna mengi ya kufanywa,” alisema na kuongeza;

” Royal GD Animal Health ni kampuni ya Uholanzi , maabara maarufu yenye utaalamu mkubwa katika utambuzi wa magonjwa ya wanyama, ina uwezo wa kufanya uchambuzi wa maabara milioni 5 kila mwaka, ikihudumia nchi mbalimbali duniani,” Balozi de Boer alisisitiza usimamizi wa magonjwa kwa ufanisi kama jambo muhimu kwa mafanikio na uendelevu wa sekta ya kuku na kwa kuboresha uwezo wa TVLA katika kutambua magonjwa ya kuku kwa usahihi na haraka.

Alieleza kwamba mashirikiano haya pia yatanufaisha na maeneo mengine ya ushirikiano kupitia Makubaliano ya Pamoja (MOU) na afya ya kuku ikiwa ni mojawapo ya maeneo muhimu ya ushirikiano.

“Kwa mfano, Septemba 2024, vikundi viwili kutoka Uholanzi, vilivyoshirikisha zaidi ya kampuni 11 za kuku, zilitembelea Tanzania kwa lengo la kutoa mafunzo maalum ya kuku na kuchunguza fursa za ushirikiano kupitia mikutano ya biashara.”

Mtaalamu kutoka Royal GD wa kampuni ya Uholanzi, Robert Molenaar alisema sekta ya kuku ni nguzo muhimu kwa kilimo endelevu na ustawi wa kijamii wa watu katika jamii
yoyote.

“Uholanzi kwa takwimu ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa wa bidhaa za kilimo duniani baada ya Marekani, kutokana na uwekezaji wetu katika teknolojia na nyanja nyingine muhimu katika sekta ya kilimo.” Alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Mfaume Simbah, Meneja Uzalishaji wa Kampuni ya uzalishaji wa kuku (Vifaranga ) Silverland alisema kwamba wafugaji wengi katika sekta ya kuku hawajui namna bora ya kutumia dawa na jinsi ya kutumia chanjo.

“Kuna matatizo mbalimbali katika utunzaji wa chanjo kama vile ubora wa maji (yanayotumika kwa chanjo), kiasi cha maji kinachotumika kwa chanjo na matumizi mabaya ya dawa za kuua vijidudu na chanjo au kabla na baada ya chanjo,” alisema.

Alisema uzalishaji wa kuku kwa wakulima wadogo ni mchango mkubwa kwa usalama wa chakula na maisha ya vijijini katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Hata hivyo, magonjwa ya kuambukiza yanazuia maboresho katika uzalishaji wa kuku kwa wakulima wadogo na ukosefu wa maarifa kwa wakulima juu ya matumizi ya chanjo unazuia
uzalishaji.