Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Sudan Kusini zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati hususan biashara, utalii, utamaduni na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa maslahi ya pande zote mbili.
Ahadi hiyo imeafikiwa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini Mhe. James Morgan Jijini Roma, Italia tarehe 27 Januari 2024.
Waziri Makamba amesema kuwa ushirikiano wa sekta za kimkakati baina ya Tanzania na Sudan Kusini utasaidia mataifa hayo mawili kukuza na kuimarisha uchumi wake kupitia sekta za biashara, utalii, utamaduni pamoja na kubidhaisha lugha ya Kiswahili.
Viongozi hao wamekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), kuimarisha masuala ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na ulinzi na usalama na kuendeleza ushirikiano wa kihistoria baina ya mataifa hayo uliodumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudan Kusini, Mhe. James Morgan amesema ushirikiano wa Sudan Kusini na Tanzania ni wa kihistoria kwani Tanzania na Sudan Kusini siyo tu majirani bali ni ndugu.
Kadhalika, Mhe. Morgan amesema Sudan Kusini itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya bishara hususan biashara ya mazao ya chakula kama vile mahindi.
Mhe. Morgan aliongeza Sudan Kusini itaendela kuimarisha na kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya biashara, utalii, utamaduni pamoja na kuendelea kukitangaza Kiswahili nchini humo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua