Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za fedha na uchumi, kilimo, madini, maji, utalii, siasa na diplomasia, mawasiliano na uchukuzi, teknolojia ya habari, uchumi, nishati, elimu, wiwanda, biashara na uwekezaji, ujenzi, utalii, kilimo, uvuvi, afya, elimu na utamaduni.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Bi-National Cooperation) kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaofanyika tarehe 13 16 Machi 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Mkutano huu uliofunguliwa katika ngazi ya Maafisa Waandamizi unafanyika tarehe 13 na 14 Machi 2023 pia ni mkutano wa awali kwa ajili ya kuandaa taarifa zitakazopitiwa na kujadiliwa na mkutano ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 15 Machi 2023.
Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini unalenga kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa kwanza wa BNC uliofanyika mwezi Mei 2017 jijini Dar es salaam.
Akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huu, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, ngazi ya Maafisa Waandamizi, Balozi Fatma Rajab ameeleza kuwa mkutano huu unatoa nafasi ya kupitia hali halisi ya utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano yaliyokubaliwa katika kikao cha kwanza na kuweka mikakati imara ya kusonga mbele kimaendeleo.
Kikao hiki kitahusisha majadiliano yatakayowezesha kufikiwa kwa makubaliano katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano ya kisekta yatakayo rasimishwa kwa ajili ya utekelezaji na kuruhusu maeneo mapya ya ushirikiano alisema Balozi Fatma.
Vilevile, akaeleza kuwa mkutano huu ni muhimu kwakuwa ushirikiano wa nchi zetu umejengwa katika misingi imara iliyopiganiwa kwa jasho na damu tangu enzi za ubaguzi wa rangi na hivyo BNC hiyo ni chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo yatakayokubaliwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini na Mwenyekiti mwenza za kikao hicho Bw. Zane Dangor, alieleza kuwa BNC inatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji.
Jukumu letu ni kuimarisha ushirikiano katika masuala yenye maslahi makubwa kwa mataifa yetu na kufungua fursa ya maeneo mapya ya ushirikiano alisema Bw. Dangor.
Matarajio ya Wenyeviti wa Mkutano huu ngazi ya Maafisa Waandamizi ni kuhakikisha wajumbe wanawasilisha michango yenye tija ya kisekta katika majadiliano ili kuifikia hatua ya juu ya kimaendeleo kupitia ushirikiano uliopo.
Pia viongozi hao wamesisitiza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zinauchukulia kwa upekee ushirikiano huo kwakuwa nchi hizo zina masuala mengi ya kushirikishana kupita uanachama wake katika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC na kwa lengo la kujenga uchumi wa kanda hiyo na Afrika kwa ujumla.
Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential Economic Commission-PEC) mwaka 2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini Tume ya Ushirikiano wa Pamoja (Bi-National Commission) ambayo ilichukuwa nafasi ya PEC.
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili