November 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania kuwa mwenyeji mkutano wa TECS 2024

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

TANZANIA inajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa tano wa mwaka wa kimataifa, Tanzania Energy Cooperation Summit (TECS), utaofanyika kuanzia Januari 31 mpaka Februari mosi, 2024 jijini Arusha.

Katika mkutano huo wawekezaji kutoka sekta mbalimbali, fedha na serikali zitakutana kuonyesha uwezo ilionao Tanzania.

Uwezo ambao unaonyeshwa na nchi ambayo kwa sasa imeorodheshwa kuwa ya tatu kusini mwa Jangwa la Sahara kwa uwekezaji siku za mbeleni.

Pia, inatarajiwa kuona ukuaji wa Pato la Taifa kwa 6% ifikapo 2025, huku ikishuhudia mamia ya mamilioni, kama sio mabilioni, ya uwekezaji wa dola, unaolenga kuelekezwa kwenye miundombinu, umeme wa maji, gesi asilia (LNG) na miradi ya nishati ya jua katika miaka ya hivi karibuni.

Ikiwa imeorodheshwa na KPMG, nyuma ya nchi za Afrika ya Kusini na Nigeria, Tanzania imejithibitishia hadhi yake yanapokuja masuala ya biashara na uwekezaji.

Mbali na hivyo, pia ni taifa lilitajwa kwa eneo lake la kimkakati mashariki mwa bara la Afrika, wingi wa maliasili, na ongezeko la uwekezaji hivi karibuni, haswa katika sekta ya nishati.

Kiwanda cha kwanza cha umeme wa jua cha 50MW kwenye gridi ya taifa, uwekezaji wa dola za Marekani milioni 300 katika nishati ya maji, mradi wa gesi asilia wa dola bilioni 42 ulioanzishwa na Shell, Equinor na Exxon Mobil, na takribani dola za Marekani bilioni 7 zilizoingizwa kwenye miundombinu,inathibitisha mvuto wake barani Afrika na kimataifa.

Ukiwa umeratibiwa na EnergyNet, mkutano huo hautoainisha mafanikio haya ya kujivunia pekee bali itaangazia fursa zijazo za biashara na miradi ya uzalishaji inayotarajiwa kubadilisha nchi na ukanda huu zaidi.

Changamoto zinazohusiana na fedha na dhamana pia zitajadiliwa, ili kuchochea ari zaidi ya majadiliano na kuhakikisha sekta ya umeme nchini inaendelea kuimarika zaidi.

Pamoja na wawekezaji wakubwa, wadau watakaohudhuria ni pamoja na mawaziri wa kitaifa kutoka Tanzania, Malawi, na Ethiopia, pamoja na viongozi wa makampuni ya utoaji huduma ya kitaifa, ikiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO wa Tanzania, Gissima Nyamo-Hanga.

Wasemaji kutoka Electricidade de Moçambique (EDM) na ZESCO ya Zambia pia watakuwepo. Wao, pamoja na wawakilishi kutoka sekta za umma na binafsi, wakurugenzi kutoka taasisi za kifedha ikiwa ni pamoja na AfDB, BII, World Bank Group na ATIDI na mashirika ya kikanda, wote watakuwepo Arusha, kwa ajili ya mkutano huo.

Kwa kuzingatia nafasi ya Tanzania kama mhimili wa nishati kikanda, mada zitakazojadiliwa ni pamoja na mtazamo wa kiuchumi wa Tanzania na uwezo wa maendeleo ya nishati, pamoja na kupanga njia bora ya kujenga soko la umeme la kikanda.

Ushirikiano wa sekta za umma na binafsi katika miradi ya usafirishaji pia utakuwa kwenye ajenda, pamoja na wakurugenzi kutoka taasisi za kifedha, utawala na kanuni, na nafasi muhimu ya nishati mbadala.

Washiriki watapewa fursa ya kutoa mawazo kuhusu kutengeneza uunganisho bora wa kikanda, mifumo imara zaidi kwa biashara na uwekezaji, na hatimaye kuunda ramani ya ufikiaji wa nishati kikanda kwa siku za usoni.

Akizungumzia mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa EnergyNet, Simon Gosling amesema Tanzania imejitengenezea nafasi muhimu kwa biashara barani Afrika.

“Kwa kuwa na uhusiano baina ya kusini na mashariki na pia ulimwenguni kote, nchi hii siku zote imekuwa na uwezo wa kuwa mwanzilishi wa ukuaji wa viwanda na sasa tunashuhudia jinsi adhma hii itakavyotimizwa.

“Hivyo nina shauku kubwa kuonyesha ukuaji wa Tanzania kuhakikisha fursa na kasi hii inaendelea,”

“Pia tunafurahi kuandaa mkutano huu Arusha, ukitoa muda na nafasi kwa kila mtu kujadili kwa kina masuala muhimu zaidi kuhus sekta mbalimbali,” amesema Gosling.

Kwa upande wake Mchambuzi na Kaimu Mratibu wa Regional Liquidity Support Facility (RLSF) katika taasisi ya African Trade and Investment Development Insurance (ATIDI), Obbie Banda amesema Tanzania ni nchi mmojawapo waanzilishi wa Jumuiya hiyo.

“Tuna nia ya dhati kuiunga mkono zaidi kusaidia malengo yake kwenye sekta ya nishati. Tukiendeleza mafanikio yaliyopatikana katika mkutano wa mwaka jana uliofanyika Dar es Salaam.

“Tunatumai kuwa TECS24, itatoa ufafanuzi zaidi kuhusu nafasi ya sekta binafsi katika sekta ya nishati na jinsi wakurugenzi kutoka taasisi za kifedha, hasusani watoaji wa bima na dhamana wa kikanda kama vile ATIDI, wanaweza kusaidia juhudi hizo na mabadiliko makubwa ya nishati kwa ujumla,” amesema Banda.

Naye Aleem Tharani, Mkuu mwenza wa Infrastructure Sector Group (Afrika), Bowmans na Mkuu wa Miradi, Nishati na Miundombinu (Afrika), wamehitimisha kwa kusema;

“Mkutano wa 5 wa kimataifa wa Tanzania Energy Cooperation Summit unaweka alama muhimu kwa sekta ya nishati barani Afrika. Kwa kuwaunganisha wawekezaji, taasisi za serikali na wataalamu wa sekta.

“Tunachochea majadiliano muhimu kwa ajili ya kukuza ramani ya nishati ya Tanzania, kutoa kipaumbele kwa gesi na nishati mbadala, na kuboresha usafirishaji wa kikanda.

“Bowmans inajivunia kudhamini mkutano huu, ikiona umuhimu wake katika kuunda mustakabali wa nishati wa Afrika na kuzidisha ushirikiano wa umma na binafsi.”