September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,EAC kulinda rasilimali Ziwa Victoria

Na Penina Malundo, timesmajira

SERIKALI imesema kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhakikisha rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria zinalindwa ili zinufaishe jamii zinazozunguka ziwa hilo na mataifa husika kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tano wa Baraza la Mawaziri la Sekta ya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe Maji wa Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa Victoria (LVFO) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ngazi ya Makatibu Wakuu uliofanyika jijini Kampala, Uganda.

Prof. Shemdoe ameuhakikishia mkutano huo kuwa, Tanzania itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia ziwa hilo kama nchi wanachamawa LVFO zilivyokubaliana. Alisisitiza pia kuwa Tanzania inaendelea kudhibiti matumizi ya zana haramu za uvuvi, kupiga marufuku uvuvi wa samaki wachanga, kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi na kuhamasisha ufugaji wa samaki kwa vizimba katika Ziwa Victoria bila kuathiri mazingira.

Alisema pia, Tanzania imeimarisha udhibiti wa uingizaji wa zana za kuvulia samaki ili kuzuia uingizaji wa zana haramu nchini na kuendesha ukaguzi wa kina ili kuhakikisha uvuvi endelevu unafanyika kwa tija.

Pia Profesa Shemdoe alisema kuwa mchango wa Sekta za Uvuvi katika uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo sana kwakuwa mchango wake unahesabiwa katika maeneo ya uvuvi na ukuzaji bila kujumuisha mapato yanayotokana na shughuli zote zinazofanyika katika minyororo yake ya thamani.

“Mchango wa Sekta za Uvuvi katika uchumi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni mdogo sana kwakuwa mchango wake unahesabiwa katika maeneo ya uvuvi na ukuzaji bila kujumuisha mapato yanayotokana na shughuli zote zinazofanyika katika minyororo yake ya thamaniBadala yake thamani hiyo inajumuishwa katika sekta zingine na hivyo kutokutoa picha halisi ya Sekta ya Uvuvi,” alisema.

Katika mkutano huo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima, alimwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alisema Tanzania utaendelea kushirikiana na nchi wanachama katika kulinda rasilimari za ziwa hilo.

Kikao hiki kimehudhuriwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizopo katika Taasisi ya Uvuvi ya Ziwa