November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANROADS yamaliza changamoto ya barabara korofi Shinyanga kupitika mwaka mzima

Na Suleiman Abeid
TimesmajiraOnline,Shinyanga

WAKALA wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Shinyanga imefanikiwa kumaliza changamoto ya maeneo korofi ya barabara katika maeneo mengi nakufanya barabara zote kupitika kwa kipindi chote cha mwaka mzima.

Hayo yamesemwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Mwabomba wilayani Kahama ambao wanatembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Shinyanga kuangalia kazi ya matengenezo ya barabara zinazotekelezwa na Wakala huo.

Mha. Ndirimbi ametaja miongoni mwa maeneo ya barabara korofi ni eneo la Mwabomba wilayani Kahama lililopo mpakani mwa mkoa wa Geita na Shinyanga ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa halipitiki vizuri hasa kipindi cha masika.

Eneo hilo ambalo kwa sasa limetengenezwa lilikuwa ni moja ya maeneo korofi na mara nyingi vipindi vya masika wananchi walilazimika kuvushwa kwa mitumbwi kutoka eneo moja kwenda eneo la pili lakini kwa sasa changamoto hiyo haipo tena baada ya kujengwa daraja imara na kuboreshwa kwa barabara.

Mha. Ndirimbi amesema Tanroads mkoani Shinyanga inasimamia barabara zenye urefu wa kilometa 1,178 ambazo zimegawanywa kwenye makundi makubwa matatu ikiwemo barabara za mikoa, barabara kuu na zile ambazo zimekasimiwa kutoka halmashauri chini ya TARURA.

Amesema kuna kilometa 277 za barabara zimetengenezwa kwa kiwango cha lami na zinazobaki ni barabara za vumbi na kwamba malengo ya Tanroads ni kuhakikisha barabara zote zinapitika kwa kipindi chote cha kiangazi na masika.

“Na kwa juhudi tunazozifanya kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mfuko wa barabara na mfuko mkuu wa Serikali tunatengeneza barabara zetu na tunaweza kujivunia mkoa wa Shinyanga hakuna mahala ambapo hapapitiki iwe wakati wa masika ama kiangazi,”

“Hata hizi barabara ambazo tumekasimiwa karibu kilometa 270 bado zinapitika vizuri, awali zilikuwa katika hali mbaya, mfano ni hili eneo la Mwabomba mpakani mwa mikoa ya Shinyanga na Geita lilikuwa halipitiki kabisa, lakini kwa sasa mtu mwenye gari anaweza kuendesha kilometa 160 kwa saa pasipo shida,” ameeleza Mha.Ndirimbi.

Mha.huyo ameendelea kufafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 2.69 kutoka mfuko wa miradi ya maendeleo kupitia kilipokelewa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 na kufanya matengezo yote ambayo yamefanyika hadi hivi sasa kufikia shilingi bilioni 15.1 na kuwezesha barabara zote kupitika vipindi vyote.

Ameendelea kueleza kuwa hivi sasa kazi zinazoendelea ni pamoja na kuinua barabara sehemu za mabonde na kuweka makalavati ili barabara zipitike kwa urahisi na pia kazi nyingine inayofanyika ni kupasua barabara mpya inayotoka eneo la Ulowa Ushetu na kuunga mpakani mwa mkoa wa Shinyanga na Tabora.

Mha. wa matengenezo TANROADS mkoa wa Shinyanga, Midara Yaredi ameeleza kuwa barabara inayofunguliwa kutoka Ulowa hadi mpakani mwa mikoa ya Shinyanga na Tabora eneo la mto Igombe yenye umbali wa kilometa 25 ni barabara muhimu kwa upande wa kiuchumi kwa wakazi wa mikoa yote miwili.

“Hii barabara haikuwepo awali ilikuwa ikitumika kama njia za watembea kwa miguu, kwa hiyo ni barabara mpya kabisa ambayo tunaifungua, awali ilikuwa na urefu kama kilometa 30 lakini baada ya kuifanyia usanifu itapungua itakuwa kilometa 25 na zote zimeishafunguliwa mpaka mwisho,” ameeleza Mhandisi Yaredi.

Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Mwabomba, Elisha Mashauri, Japhet Daud, Amos Matata mkazi wa kijiji cha Songambele Mwenge na Godfrey Joseph mkazi wa kijiji cha Sirambo kata ya Utapizya wilayani Kaliua Tabora wameipongeza Serikali kwa jinsi inavyotenga fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya barabara muhimu.

“Binafsi namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anazotufanyia sisi watanzania kiasi cha kujiona ni wamoja na tunaishi katika nchi yenye amani, tunachoomba sasa atuboreshee zaidi eneo la pale mto Igombe ili barabara iweze kupitika vizuri hadi huku kwetu, kwa sasa tunalazimika kuzunguka kufuata huduma muhimu kule Ushetu Kahama,”

“Tunaamini barabara hii inayounganisha wilaya za Kahama, na Kaliua mkoani Tabora ikikamilika, Rais wetu atakuwa ametukomboa sisi wananchi wake, kwa sasa ni tunapata shida kwa kutembea tunapofanya shughuli zetu za kibiashara, mimi nakosa kitu cha kumpatia Rais Samia, lakini nimuahidi tu kwamba Kura yake mwaka 2025 ipo mikononi mwangu,”ameeleza Godfrey.