February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANROADS yaanika mafanikio ya Rais Samia

Na Joyce Kasiki,Timesmajiraonline, Dodoma

UONGOZI wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umefunguka kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuanzia Machi 2021 hadi Februali mwaka huu.

Kwa mujibu wa TANROADS katika kipindi hicho mtandao wa barabara chini ya awamu sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia, umeongezeka na kufikia urefu wa kilometa 37,435.72.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Dkt.Samia, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Ephatar Mlavi, alisema kati ya kilomita hizo, barabara za lami kwa upande wa barabara kuu ni kilometa 9,566.50 na barabara kuu za changarawe ni kilometa 2,960.94 na madaraja 4,367.

Kwa upande wa barabara za lami za mikoa alisema zimefikia kilometa 2,636.18, changarawe ni kilometa 22,271.41, huku madaraja yakiwa 5,196 na kufanya jumla ya mtandao wa barabara kufikia kilomita 37,435.04 na madaraja 9,563.

Amesema katika kipindi hicho kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025, Serikali imepata mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini, ambapo katika kipindi hicho, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 15,625.55 zimekuwa katika hatua mabalimbali za utekelezaji .

“Barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha, amesema barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,052.94 na madaraja mawili , zimefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami.

“Vilevile, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja kumi unaendelea.

Amesema miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami. “Amesema Mhandisi Mlavi.

Kuhusu madaraja amesema ,katika kipindi tajwa madaraja makubwa 9 yamekamilika kujengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 381.301 kama ifuatavyo;

Gerezani Dar es Salaam, Daraja jipya la Tanzanite Dar Es Salaam , Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida).

Aliyataja Madaraja kumi ambayo ni Kigongo Busisi (Magufuli Bridge – Kilometa 3.0), Lower Mpiji (Meta 140), Mbambe (Meta 81), Simiyu (Meta 150), Pangani (Meta 525), Sukuma (Meta 70), Kerema Maziwani (meta 80), Kibakwe (meta 30), Mirumba (Meta 60) na Jangwani (Meta 390) ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya sh. Bilioni 985.802.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mlavi, jumla ya madaraja makubwa 19 yako kwenye maandalizi ya kujengwa ambayo ni: Godegode (Dodoma), Ugala (Katavi), Kamshango (Kagera), Bujonde (Mbeya), Bulome (Mbeya), Chakwale (Morogoro), Nguyami (Morogoro), Mkundi (Morogoro), Lower Malagarasi (Kigoma), Mtera (Dodoma), Kyabakoba (Kagera), Mjonga (Morogoro), Doma (Morogoro), Sanga (Songwe), Kalebe (Kagera), Ipyana (Mbeya), Mkondoa (Morogoro), Kilambo (Mtwara) na Chemchem (Singida).

“Katika kipindi cha miaka minne (Juni 2021- Desemba 2024) hali ya barabara kuu na zile za mikoa imeendelea kuimarika ambapo barabara zilizo katika hali nzuri na wastani zimekuwa karibu asilimia 90 ya jumla ya mtandao wote wa barabara wenye kilometa 37,225.72,” amesema na kuongeza;

“Hali hii ya kuimarika kwa mtandao wa barabara imesababisha kupungua kwa muda wa usafiri katika barabara, kuimarika kwa bei za usafirishaji ambapo nauli hazipandi kiholela na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotumia barabara.”

***Viwanja vya ndege

Kwa upande wa viwanja vya ndege, amesema, ujenzi umekamilika kwa miradi Saba ya Julius Nyerere (Terminal Three), Mwanza, Mtwara, Songea, Songwe (Runway), Songwe (Supply and Installation of Airfield Ground Lights (AGL) na Geita.

Mhandisi Mlavi ametaja mafanikio mengine kuwa ni kumalizika kutekelezwa kwa Miradi ya Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Pili,kilometa 20.3 (Mbagala – Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu Kariakoo, Sokoine Zanaki, Barabara ya Kawawa Barabara ya Morogoro (Magomeni).

Pia kuendelea kutekelezwa kwa Miradi ya Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Awamu ya Tatu kilometa 23.3 katikati ya Jiji hadi Gongo la Mboto ambao umefikia asilimia 74, awamu ya nne ya mradi huo kilometa 30.1 kutoka katikati ya Jiji hadi Tegeta ambao umefikia asilimia 22 ambapo awamu ya tano kutoka Ubungo Bandarini na Segerea-Tabata-Kigogo, kilometa 25.4 upo katika hatua za mwisho za manunuzi.

***Kupunguza msongamano Jiji la Dodoma

Mhandisi huyo alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Mzunguko wa Nje katika Jiji la Dodoma kwa kiwango cha lami yenye jumla ya urefu wa Kilometa 112, kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji.

Alisema ,hadi kufikia Februari, 2025, ujenzi umefikia asilimia 91 Sehemu ya Kwanza ya Nala- Veyula- Mtumba – Ihumwa Bandari Kavu kilometa 52.3 na asilimia 85 kwa Sehemu ya Pili ya Ihumwa Bandari Kavu -Matumbulu Nala- Kilometa 62.

Katika hatua nyingine alisema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi kwa ufadhili wa Benki ya Dunia inayohusisha upanuzi wa barabara zinazoingia na kutoka katika Jiji la Dodoma kuelekea Chamwino Kilometa 32 katika Barabara Kuu ya Morogoro – Dodoma, kuelekea Mkonze kilometa 4.5 katika Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma, na kuelekea Zamahero kilometa 8.5 katika Barabara Kuu ya Arusha – Dodoma kupitia mradi wa Dodoma Integrated and Sustainable Transport (DIST).

Katika hatua nyingine Mhandisi Mlavi amesema Serikali inaendelea na upanuzi wa Barabara Kuu ya TANZAM sehemu ya Uyole – Ifisi – Songwe Airport Jijini Mbeya yenye urefu wa kilometa 36 kutoka njia mbili kuwa njia nne kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo ambapo hadi kufikia mwezi Februari, 2025 utekelezaji umefikia asilimia 22.

Pia imesema inaendelea kufanya Upanuzi wa Barabara Kuu ya Mwanza – Usagara – JPM Bridge kwa njia nne kilometa 37 kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Mwanza na kufanya Usanifu wa miradi ya Upanuzi wa Barabara za Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwenye sehemu ya Barabara Kuu ya Tengeru – USA River, ujenzi wa mchepuo wa Kwa Sadala ikijumuisha daraja la Kikafu na sehemu ya Kibosho Shine hadi Kiboroloni.