Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online, Shinyanga
MADEREVA wa magari makubwa mkoani Shinyanga yenye uzito wa kuanzia tani tatu na nusu na kuendelea wameonywa kuacha tabia ya kupakia mizigo na kuzidisha uzito unaotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Onyo hilo limetolewa na Meneja wa Wakala wa barabara (TANROADS) mkoani Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi wakati akitoa mafunzo juu ya matumizi sahihi ya barabara kwa madereva wa magari makubwa ikiwa ni katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Mhandisi Ndirimbi amesema moja ya chanzo kikuu cha barabara nyingi kuharibika katika kipindi kifupi husababishwa na magari yanayopakia mizigo inayozidi uzito halisi wa gari husika na hivyo kuharibu barabara.
Amesema kila dereva anapaswa kuelewa kuwa kupakia mizigo na kuzidisha uzito wa gari ni kosa na pindi mtu atakapobainika kufanya hivyo anastahili kuchukuliwa hatua kali za kisheria na hulipishwa faini kubwa.
“Changamoto kubwa ipo kwa madereva wa malori yanayobeba vifaa vya ujenzi ikiwemo mchanga, kokoto na mawe ambao mara nyingi hawazingatii uzito wa magari yao wanapopakia mizigo kwenye magari yao, hii ni hatari kwa barabara zetu,”
“Tunaomba muelewe kuwa barabara zetu zina kiwango cha mwisho kabisa cha tani 56 kwa ujumla, sasa magari yanayozidisha uzito tofauti na tani hali za gari ni kosa na utasababisha uharibifu wa barabara mapema kabla ya muda wake, hivyo tunaomba kila mtu azingatie hilo,” ameeleza Mhandisi Ndirimbi.
Mhandisi huyo amewapa mfano madereva wanaozidisha uzito kwenye magari yao kwamba ni sawa na mtu kumbembesha mtu mwenye uzito wa kilo 50 ukambembesha mzigo wenye uzito wa kilo 100 jambo ambalo hawezi kumudu na kwamba magari yanayozidi uzito huchangia barabara kutitia na kupasuka.
Ameeleza kuwa kila mtu anapaswa kuelewa kuwa fedha zinazotumika katika matengenezo ya barabara si za Serikali bali ni za wananchi wenyewe hivyo kila zinapotumika katika eneo ambalo halikupangwa ni wazi wanaoumia ni wananchi wenyewe.
“Wapo madereva wa malori yanayobeba mchanga ambao hukubaliana na wateja wao kuzidisha ujazo kwa lengo tu la dereva huyo kuongezewa fedha kidogo ambazo hazipelekwi kwa tajiri lakini hata hivyo hawaelewi uzito unaozidi unaharibu kwa kiasi kikubwa barabara,”
“Leo wewe dereva unakula njama na mteja wako, unapakia mchanga ama kokoto kuzidi uzito halisi wa gari lako ili mradi tu upate shilingi elfu ishirini ya juu bila kujali uharibifu utakaousababisha, barabara ikiharibika inakarabatiwa kwa maelfu ya shilingi, ambazo watoaji ni mimi na wewe, acheni tabia hii,” anaeleza mhandisi Ndirimbi.
Katika hatua nyingine watumishi wa Wakala wa barabara (Tanroads) mkoani Shinyanga wanaadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuchangia damu na kuwasaidia wagonjwa ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Mhandisi Ndirimbi amesema mbali ya kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara pia watatumia maadhimisho ya wiki hiyo ya utumishi wa umma kwa kufanya shughuli za kijamii ambapo watatoa misaada kwa wagonjwa yenye thamani ya shilingi milioni moja.
“Tumekubaliana na wenzangu kwamba tuitumie wiki hii kwa kufanya shughuli za kijamii ambapo mbali wa utoaji wa elimu juu ya matumizi sahihi ya barabara pia tuchangie damu kwa ajili ya kuongeza akiba ya damu katika hospitali zetu na tutatoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa ambao wamelazwa hospitali,” anaeleza Mhandisi Ndirimbi.
More Stories
Serikali kuwezesha CBE kuwa kituo mahiri
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA
Mwanafunzi apoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba