Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
KAMPUNI ya Saruji ya Tanga (Tanga Cement PLC) imezindua rasmi mauzo ya hisa stahiki (Rights Issue) zenye thamani ya sh. bilioni 204, hatua inayotajwa kuwa kubwa zaidi katika historia ya masoko ya mitaji nchini Tanzania.

Akizungumza katika uzinduzi huo jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, alisema uzinduzi huo ni uthibitisho wa ukuaji wa masoko ya fedha nchini na mchango wake katika kuendeleza sekta ya viwanda.
Alisisitiza kuwa hatua ya Tanga Cement inajenga imani ya wawekezaji na kuongeza nafasi ya wanahisa kupata thamani halisi ya uwekezaji wao.


Kwa mujibu wa utaratibu ulioelezwa, wanahisa waliopo watapatiwa fursa ya kununua hisa mbili mpya kwa kila hisa moja waliyonayo kwa bei ya sh. 1,600, bei ambayo ni punguzo la asilimia 38 ukilinganisha na bei ya sasa sokoni. Zoezi hili limefunguliwa kuanzia Septemba 29 na litafungwa Oktoba 24, 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement, Alfonso Velez, alisema lengo kuu la mauzo haya ya hisa ni kulipa madeni ya kigeni, kuimarisha mizania ya kifedha na kutoa nafasi kwa kampuni kuwekeza katika miradi mipya ya ukuaji. Aliongeza kuwa hatua hiyo pia itapunguza gharama kubwa za riba zilizokuwa zikikandamiza faida ya kampuni kwa miaka mingi.
“Tumeamua kuchukua hatua hii ili kuhakikisha kampuni inapata pumzi mpya kifedha. Tunahitaji mtaji wa kutosha ili kuwekeza katika teknolojia, kupunguza gharama za uzalishaji na hatimaye kurejesha imani ya wanahisa wetu kwa kuanza tena kulipa gawio,” alisema Velez.


Aidha, alibainisha kuwa mwaka 2025 tayari umeonyesha mwelekeo chanya wa kibiashara. Kampuni imepanda kutoka hasara ya shilingi bilioni 56 mwaka uliopita hadi faida ya uendeshaji ya shilingi bilioni 29.4, huku matarajio yakiwa karibu sh. bilioni 50 mwishoni mwa mwaka. “Huu ni ushahidi kwamba Tanga Cement sasa iko kwenye njia sahihi,” aliongeza.

Moja ya sababu kuu za mafanikio hayo ni kupungua kwa gharama za uzalishaji wa klinka, ambapo bei imeshuka kutoka dola 60 hadi dola 35 kwa tani.
Hali hiyo imewezesha kampuni kuuza zaidi ya tani milioni moja za saruji na tani 500,000 za klinka mwaka huu, kiwango cha juu zaidi katika historia ya Tanga Cement.
Pamoja na kupunguza gharama, kampuni pia inawekeza zaidi ya shilingi bilioni 30 katika maboresho ya mitambo na teknolojia rafiki kwa mazingira, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nishati mbadala na kupunguza uzalishaji wa hewa ya kaboni.
Malengo ya muda mrefu ni kufikia uzalishaji endelevu na kulinda mazingira huku ikichangia katika ajenda ya kitaifa ya mabadiliko ya kijani.
Kwa upande wake, wadau wa masoko ya mitaji wamepongeza hatua hiyo wakisema ni ushahidi wa jinsi sekta ya fedha inavyoimarika nchini. iTrust Finance, ambao ndio washauri wakuu wa muamala huo, wameeleza kuwa dhamira ya Tanga Cement ni mfano wa kampuni za ndani kutumia masoko ya mitaji kama nyenzo ya kukua badala ya kutegemea mikopo ya kigeni.
Velez alihitimisha kwa kueleza kuwa mpango huu si wa kufanikisha mauzo ya hisa pekee, bali ni safari ya muda mrefu ya kuijenga upya kampuni.
“Tunataka Simba Cement ibaki kuwa kampuni ya Kitanzania, yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa na yenye nguvu kwa vizazi vijavyo,” alisema.



https://www.instagram.com/p/DPN-KM6iJlV/?utm_source=ig_web_copy_link&igsh=MzRlODBiNWFlZA==

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama