November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANESCO yazindua Mpango wa jinsia,yatakiwa kuwa na kitengo maalumu cha kushughulikia kero za kijinsia

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SHIRIKA la Umeme Tanzania(TANESCO)limetakiwa kuweka kitengo maalumu kitakachoshughulika na kusikiliza kero za kijinsia ili kuweka usawa wa kijinsia katika shirika hilo.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 30,2023 na Naibu Waziri wa Nishati,Stephen Byabato katika uzinduzi wa Programu ya Mpango wa Jinsia wa miaka minne(2023-2027)wa TANESCO kwa kusirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa umeme wa Tanzania hadi Zambia(Tanzania-Zambia Transmission Interconnector Project-TAZA).

Naibu Waziri Byabato amesema kuwa Shirika hilo limekuwa likishughulikia masuala ya jinsia kwa namna mbalimbali hivyo kwasasa ni wakati muafaka wa kuwa na kitengo kitakachokuwa na bajeti,uongozi wa kitengo chenye uelewa na uweledi wa kusikiliza kero za kijinsia mbalimbali zitakazojitokeza.

“Changamoto mbalimbali zinaweza kujitokeza lakini kukiwepo na kitengo mtu atakapopata Changamoto anaweza kuwa amefanyiwa jambo ambalo siyo sawa awe na sehemu ya kwenda kusema na kupata msaada 

“Na kwenye hivi vitengo siyo kwajili ya kukamata mwizi na kukamata aliyetukosea bali kuwapa ushawishi,kuwaelimisha,kuwapanguvu kwa ujumla ambao wamepata matatizo mbalimbali ili waweze kuwa sasa na imani katika jamii na kuendelea kufanyakazi,”amesema Byabato.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,Maharage Chande amesema kuwa lengo la programu hiyo kuwa ni kutatua changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanawake katika maeneo yao ya kazi kwa lengo la kukuza ajira zao ili kuongeza idadi ya wanawake wanaoajiriwa.

Mkurugenzi Chande ametaja maeneo ya kimkakati yatakayopewa kipaumbele kuwa ni kuiboresha sera ya Shirika na kujenga uwezo ili sera iende sambamba na masuala ya kijinsia,kuwepo na taarifa sahihi zinazohusu masuala ya unyanyasaji wa kijinsia kwenye Taasisi,kuruhusu fursa ya ukuzaji wa taaluma kwa wafanyakazi wanawake hasa wanaofanyakazi kwenye miradi na kuwepo kwa nafasi ya mafunzo kwa vitengo kwa wafanyakazi wanawake waliopo kazini ili kuwajengea uwezo kuelekea kwenye ajira kamili.

Akieleza kuhusu mradi wa kusafirisha umeme wa Tanzania hadi Zambia (TAZA),Chande ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO wanatekeleza ujenzi wa mradi wa upanuzi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 400 kutoka katika kituo cha kupokea,Kupoza na kusafirisha umeme mkubwa cha Tagamenda Iringa kwenda kwenye nchi zilizopo kusini mwa Tanzania(Southern African Power Pool)kupitia Kisada Iringa,Iganjo Mbeya na Nkangamo Tunduma Songwe.

“Mradi huu unafadhiliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Maendeleo (IDA) ya Benki ya Dunia kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 455,Mfuko wa Maendeleo wa Ufaransa (AfD) kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 115,umoja wa Nchi za Ulaya(EU)kwa Dola za Kimarekani milioni 30 pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Dola za Kimarekani milioni 10,”amefafanua.

Chande amekitaja kituo hicho cha Tagamenda kuwa ni kitovu cha kusafirisha umeme mkubwa wa kilovoti 220 kwenda kwenye mikoa takribani 18 nchini.

“Na kwa upande mwingine kituo hiki kimeunganishwa na kituo cha umeme cha zuzu Dodoma ili kusafirisha umeme mkubwa kwenda kwenye nchi zilizopo Mashariki mwa Tanzania ambazo ni Kenya,Uganda na Ethiopia kupitia mradi wa kuunganisha umeme baina ya Kenya na Tanzania(Kenya-Tanzania Power Interconnection Project-KTPIP)