Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dodoma
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limepongezwa kwa utekelezaji thabiti wa miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo midogo midogo na mikubwa ya kimkakati ambayo inawezesha usambazaji wa nishati hiyo nchini kote.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alipotembelea banda la TANESCO katika maonesho ya Teknolojia yanayoendelea katika Uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma.
Sambamba na pongezi hizo, Mtaka ameshauri wataalamu wa Tehama wa TANESCO kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu ili kuboresha mifumo ya utoaji huduma ikiwemo huduma za ununuzi wa umeme wa LUKU ili kuwezesha wateja kununua umeme kisha umeme huo kuingie katika mita bila kumlazimu mteja kwenda kuweka umeme katika mita yake.
Mtaka alisema pamoja na mambo mengi mazuri ambayo TANESCO imekuwa ikiyafanya, ni vyema Shirika likafanya ushirika na taasisi za elimu ya juu ili kukuza ubunifu na kuwezesha wataalamu wa ndani kutumika katika kutekeleza miradi mbalimbali bila kuhitaji wataalamu kutoka nje ya nchi na ikiwezekana wataalamu wa Shirika waweze kufanya na kusimamia hata miradi mingine mikubwa inayotekelezwa katika nchi jirani.
“Hii nikutokana na uzoefu ambao wataalam wa TANESCO watakuwa wameupata baada ya kukamilisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati,” amesema Mtaka
Mtaka ameongeza kuwa, miradi ya umeme vijijini inatekelezwa kwa weledi wa hali ya juu, hivyo ni vyema sasa TANESCO ikawezesha wataalam wake kwa kushirikiana na Taasisi zingine za Serikali kuanza kupeleka wataamamu katika kandarasi za usimamizi wa miradi nje ya nchi.
More Stories
Dkt.Mathayo:Dkt.Samia,Dkt.Mwinyi wanastahili,ajivunia mafanikio jimboni
Jokate achangia milioni 3 mfuko wa bodaboda
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji