October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo

TANESCO kuwekeza Bilioni 1.2 Umeme wa kiwanda cha sukari Mtibwa

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema Serikali kupitia TANESCO imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati)akifuatana na Kaimu Meneja wa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Leilah Muhaji(kulia) pamoja na wataalam wa shirika hilo. Na Mpigapicha Wetu

Dkt. Kalemani amesema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi kukagua hali ya upatikanaji wa umeme katika kiwanda cha Mtibwa kilichopo Mkoani Morogoro.

Kalemani ameongeza kuwa, njia ya umeme itakayojengwa ni ya umeme mkubwa yenye urefu wa takriban kilomita 100 na itakuwa maalum kwa ajili ya kiwanda cha sukari cha Mtibwa.

Aidha, ujenzi huo utaanza ndani ya siku mbili zijazo. Dkt Kalemani amesema ujenzi wa njia hiyo ya umeme utakwenda sambamba na ongezeko la kiasi cha umeme ambacho kitafikishwa kiwandani hapo ikiwa ni megawati 27 hadi 40, ili kukidhi ongezeko la mahitaji yoyote ya umeme yatakayojitokeza kiwandani hapo kwa kipindi cha miaka mitano hadi kumi ijayo.

Mahitaji ya umeme katika kiwanda hicho kwa sasa ni megawati 5 hadi 8 lakini kutokana na maboresho makubwa ambayo yanatarajia kufanyika kiwandani hapo katika kipindi cha miaka mitano, inatarajiwa kuwa mahitaji ya umeme yataongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia takribani megawati 27 ifikapo mwaka 2025.