November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wadau wa nguzo katika ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam mapema leo

TANESCO kutumia nguzo za zege kuanzia mwezi ujao, kuokoa bilioni 67

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza kutumia nguzo za umeme za zege kwenye miradi yake mbalimbali, huku ikipiga marufuku uingizwaji wa nguzo hizo za  umeme toka nje na kuruhusu wawekezaji mbalimbali kuwekeza nchini katika utengenezaji wa nguzo za zege.

Akiongea na wadau wa nguzo katika ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amesema, Serikali imeamua kuanza kutumia nguzo za zege kusambaza umeme kuanza  Julai Mosi, 2020

Mabadiliko haya yataleta tija kubwa katika sekta ya Nishati ya Umeme, ambapo moja ya faida za matumizi ya nguzo hizo ni kufanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa saa zote 24 na kuondoa kero ya kukatika kwa umeme inayosababishwa na nguzo kuanguka au kubadilishwa mara kwa mara.

Hatua hiyo itaiwezesha serikali kuokoa takribani shilingi bilioni 67 ambazo zimekuwa zikitumiwa na TANESCO katika kubadilisha na kununua nguzo kila mwaka. Dkt. Kalemani amesema, umeme unaozalishwa unatosha kwa matumizi yote kwa sasa, hivyo hakuna sababu ya msingi ya kukatika umeme kwa sababu ya kubadilisha nguzo.

“Tunao umeme wa kutosha kwa sasa, hakuna sababu ya umeme kukatika katika kwa sababu ya kubadilisha nguzo na pia hakuna sababu ya TANESCO kutumia fedha bilioni 67 kubadilisha nguzo huku ni kulipa mzigo wa gharama shirika letu,” amesema Kalemani

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni tanzu ya TANESCO inayohusika na utengenezaji wa nguzo za zege TPMC  Mhandisi Yusuph Kitivo amesema kuwa matumizi ya nguzo yamekua yakitumika katika maeneo maalum kama katika mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kuwa nguzo hizo zitaleta matokeo mazuri katika uboreshaji wa huduma ya umeme .

Naye Burton Nsemwa kutoka kampuni ya Lukolo inayotengeneza nguzo za zege  ameishukuru Serikali kwa kuona kuwa ni fursa kwa wawekezaji wazawa katika kutoa mchango wao kwa taifa lengo likiwa ni kusukuma gurudumu la maendeleo