Na Bakari Lulela,TimesMajira Online
MGOMBEA Udiwani kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Tandale jijini Dar es Salaam, Abdallah Abdul aziz amesema, akipata ridhaa ya kuchaguliwa kushika nyadhifa atatoa huduma za kisheria kwa wakazi wa eneo hilo bure.
Amesema, kupitia serikali yake ya CCM ameahidi kujenga kituo maalumu cha watoto wenye vipaji mbalimbali kitakachoitwa ‘out of talent ‘ kitakacho wasaidia kufikia malengo yao sambamba na kuwa kitovu cha mafanikio kwa kizazi kijacho.
Akizungumzia mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa kampeni ya CCM, iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Tandale Magharibi, mgombea huyo amesema, serikali ya awamu ya tano imefanya mambo mengi katika kipindi cha miaka mitano na kuahidi kufanya makubwa zaidi katika miaka mitano ijayo.
“Kila mtanzania ameweza kujionea bila kupepesa, serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuboresha miundombinu ya barabara kubwa na zile za mitaa katika eneo letu la Tandale kwa kiwango cha juu, isitoshe imejenga kingo za mito ambazo huwa korofi hususan vipindi vya mvua nyingi na kuleta madhaa makubwa kwa wananchi,” amesema Abdul Aziz.
Aidha mgombea huyo amesema, kupitia elimu bila malipo serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kuboresha miundombinu ya majengo ya shule za msingi kwa kiwango kikubwa na kufanikiwa kuongeza ufaulu wa shule hizo ambapo watoto wengi huchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Abdul Azizi amesema, akipewa ridhaa ya kuongoza kila mwanafunzi wa shule ya msingi wa kata hiyo atatakiwa kuwa na bima ya afya kwa ajili ya kupata huduma bora za matibabu sambamba na kuboresha Zahanati ya Tandale kiasi ambacho baadhi ya huduma ziwe zinapatikana ikiwemo upasuaji.
Kwa upande wa vijana wa bodaboda Abdul Aziz amesema, wamekuwa na changamoto kubwa kwenye kuandikiana mikataba mibovu na waajiri wao, hilo ameahidi kulisimamia ili waweze kunufaika na kazi hiyo.
Hata hivyo, amewasihi wakazi hao kuacha tabia ya kushawishika kirahisi na baadhi ya wagombea wa upinzani ambao hawana nia njema na Taifa hili, hivyo amewataka waichague CCM kwa kumpigia kura za ndio mgombea Urais Dkt. John Magufuli na kumpa kura za uhakika Abass Tarimba katika nafasi ya Ubunge sambamba na yeye kumpigia kura za kishindo katika nafasi ya udiwani.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM